Habari za Punde

ZECO kuanza kubadilisha nguzo mbovu

Shirika la Umeme Zanzibar, Jumatatu ijayo litaanza kazi ya kubadilisha nguzo mbovu katika laini za umeme mkubwa, Unguja na Pemba.

Ofisa Uhusiano wa Shirika hilo Salum Abdalla Hassan, amesema kazi hiyo itaanza kwa laini za Kusini mpya na Kusini Kongwe Unguja, na hivyo kusababisha umeme kuzimwa kwa maeneo yanayotumia laini hizo.

Amefahamisha kuwa, umeme utazimwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni ili kupisha kazi za ubadilishaji wa nguzo mbovu pamoja na vifaa vyengine.

Kwa laini ya Kusini mpya, Ofisa huyo amesema umeme utazimwa siku za Jumatatu hadi Jumatano, na Kusini Kongwe, utazimwa siku za Alkhamisi hadi Jumamosi kuanzia tarehe 25 Aprili hadi 31 Mei, mwaka huu.


Ameyataja maeneo yatakayokosa umeme kwa laini ya Kusini mpya, kuwa ni Tunguu, Kibele, Unguja Ukuu, Muyuni, Kizimkazi, Makunduchi, Paje, Jambiani na Bwejuu.
h
Kwa upande wa laini ya Kusini Kongwe, maeneo yatakayozimiwa umeme wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo, ni  Garagara, Miembe saba, Mwera, Fuoni, Dunga kiembeni, Ndijani, Chwaka, Uroa na Pongwe.

Zeco imewataka wananchi watakaoathirika na kazi hiyo wawe wastahmilivu wakijua kwamba shirika linakusudia kuwaondoshea tatizo la kukatika umeme mara kwa mara kutokana na uchakavu wa miundombinu.

Mradi wa kubadilisha nguzo mbovu za laini za umeme mkubwa, umefadhiliwa na serikali ya Norway pamoja na serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR 22/04/2016

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.