Habari za Punde

Hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais

HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA
 OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
 KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR
-------------------------------------------

1.0          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu lipokee na lijadili na hatimae likae kama Kamati ya Mapato na Matumizi ili liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya   Makamu wa Pili wa Rais kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

2.0          Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia afya njema na kuweza kutukutanisha hapa leo kwa ajili ya kuipokea hotuba hii, kuijadili na hatimae kuidhinisha Makadirio ya Mapato na matumizi ili tupate nyenzo za kutuwezesha kuwatumikia wananchi wetu.  

3.0          Mheshimiwa Spika, namshukuru na kumpongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake anazozichukua katika kuiongoza nchi yetu. Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa maelekezo na miongozo inayotekelezeka na yenye muelekeo wa kutuletea maendeleo na tija katika nchi yetu. Hotuba aliyoitoa wakati akilizindua Baraza la Tisa (9) la Wawakilishi imeonesha wazi azma yake ya kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo katika nyanja zote. Ni imani yangu kwamba wananchi wote tutaendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika juhudi zake hizi.

4.0          Mheshimiwa Spika, aidha, nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake chini ya kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.  Pia nawapongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais Magufuli katika kufanikisha majukumu yake.

5.0          Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na wasaidizi wako kwa kuliongoza vyema Baraza hili Tukufu. Aidha, nawapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Baraza kwa kuteuliwa na kuanza vyema kazi za kusimamia utendaji wa Taasisi za Serikali.  Vile vile, natoa shukrani maalum kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mheshimiwa Omar Seif Abeid, Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Konde, Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Panya Ali Abdalla, Mwakilishi wa Viti Maalum na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kuyapitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ya mwaka 2016/2017 na kutupatia ushauri na miongozo juu ya Makadirio hayo na kuikubali iwasilishwe katika kikao chako hichi kitukufu.

HALI YA SIASA:

6.0          Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliendesha Uchaguzi Mkuu wa marudio tarehe 20 Machi 2016.  Jumla ya Vyama 14 vilishiriki kugombea nafasi ya Urais ambapo Chama Cha Mapinduzi kiliibuka na ushindi wa kishindo.

7.0          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha uchaguzi kulijitokeza hali ya uvunjifu wa amani kwa baadhi ya wananchi kuchoma moto mali za Serikali na za wananchi wenzao vikiwemo vituo vya afya, mashamba ya mikarafuu na nyumba za makaazi. Aidha, kumejitokeza tabia kwa baadhi ya wananchi kususiana na kubaguana kutokana na tofauti za itikadi za kisiasa katika shughuli mbali mbali za kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha hali ya umoja, amani na utulivu inaendelea nchini. Nachukua fursa hii kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kusimamia amani ya nchi yetu.  Nawaomba wananchi waendelee kushirikiana katika shughuli zao za kijamii pamoja na kutoa ushirikiano kwa viongozi wa ngazi zote za Serikali katika kudumisha hali ya umoja, amani na utulivu.

       HALI YA UCHUMI WA ZANZIBAR:

8.0          Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Waziri wa Fedha na Mipango wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 katika Baraza lako Tukufu, uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 6.6 mwaka 2015 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 4.0 kwa nchi zinazoendelea na asilimia 3.4 kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hata hivyo, kasi hiyo inaashiria kupungua kidogo ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2014.

9.0          Mheshimiwa Spika, pato halisi la Taifa kwa mwaka 2015 limeongezeka na kufikia thamani ya Shilingi 2,308.0 Bilioni ikilinganishwa na thamani ya Shilingi 2,133.5 Bilioni mwaka 2014. Vile vile, wastani wa pato la mtu binafsi limeongezeka kufikia Shilingi 1,632,000 sawa na Dola za Kimarekani 817 mwaka 2015 kutoka Shilingi 1,552,000 sawa na Dola za Kimarekani 939 mwaka 2014 kwa bei za miaka husika. Kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani kwa wastani wa asilimia 20.8 mwaka 2015 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2014 imepelekea thamani ya pato la Mtu binafsi kwa Dola kupungua. Hata hivyo, kwa kutumia bei za kudumu za mwaka 2007 bado wastani wa pato la mtu binafsi limeongezeka kutoka Dola za Marekani 651 mwaka 2014 hadi Dola 674 mwaka 2015.

10.0        Mheshimiwa Spika, kasi ya mfumko wa bei imefikia wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2015 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2014. Kasi ya mfumko wa bei kwa bidhaa za chakula umeongezeka kufikia asilimia 7.4 mwaka 2015 kutoka asilimia 4.4 mwaka 2014. Aidha, mfumko wa bei kwa bidhaa, zisizo za chakula ulishuka hadi kufikia asilimia 4.0 mwaka 2015 kutoka asilimia 6.8 mwaka 2014. Hali hii inatokana na kushuka kwa bei za bidhaa za mafuta ikiwemo dizeli, petroli na mafuta ya taa.

11.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 maeneo muhimu yatakayoendelea kupewa kipaumbele na Serikali ni pamoja na kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu, kusimamia utunzaji na uendelezaji wa miundombinu na mawasiliano, kuendeleza utalii, kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, kuimarisha huduma za elimu, afya, pamoja na maslahi ya wazee nchini.
12.0        Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mafuta na Gesi, Serikali imekamilisha utayarishaji wa Rasimu ya Sera na Rasimu ya Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ambazo zinatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kukamilika kwa sera na sheria hizo kutaiwezesha Serikali kuwa na miongozo mizuri katika kusimamia masuala ya Mafuta na Gesi Asilia hapa nchini.
13.0        Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma za umeme, Serikali imejenga njia za kupitishia umeme mkubwa zipatazo kilomita 33.1 na  kilomita 83.9 za laini ndogo.  Aidha, Serikali imeweka transfoma 35 za kusambaza umeme katika vijiji 36 (Unguja vijiji 16 na Pemba 20).
14.0        Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda inaendelea kuimarika na tunategemea itachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi na kutoa ajira kwa wananchi. Kuanza kazi kwa Kiwanda cha Sukari cha Mahonda kunatoa matumaini ya kujitegemea kwa sukari hapo baadae. Pia Kiwanda cha Upigaji Chapa, Kiwanda cha Maziwa Fumba, viwanda vya maji na viwanda vyengine mbali mbali vikiwemo vya uchongaji na usindikaji vinatoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa uchumi wetu.

HUDUMA ZA JAMII:

15.0        Mheshimiwa Spika, huduma za jamii zitaendelea kupewa msukumo mkubwa katika kipindi hiki cha pili cha Awamu ya Saba. Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha huduma za elimu, afya, maji safi na salama pamoja na makaazi ili kuleta ustawi mzuri kwa jamii.
16.0        Mheshimiwa Spika, sekta ya elimu ni muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Sekta hii ina jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wa Zanzibar kwa mujibu wa malengo yaliyoainishwa katika Mipango na Sera ya Elimu, Dira ya Maendeleo 2020 na MKUZA. Katika kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuimarisha Skuli za Maandalizi, Msingi na Sekondari, Elimu Mbadala pamoja na Elimu ya Juu.

17.0        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza programu mbali mbali za elimu ikiwemo programu za vituo vya Tucheze Tujifunze (TuTu) na kufanya tathmini ya vituo hivyo pamoja na kusaidia watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia vifaa. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo viwili (2) vya mafunzo ya Amali Makunduchi kwa Unguja na Daya kwa Pemba; Upanuzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia; Upanuzi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii pamoja na Kukamilisha Kituo cha Elimu Mbadala – Wingwi Mtemani ili  kuwajenga vijana kitaaluma na kiujuzi ili waweze kuingia katika soko la ajira kwa uhakika.

18.0        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Afya, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa wananchi kwa kuifanya Hospitali ya Mnazimmoja kuwa ya Rufaa kwa kuiongezea huduma za matibabu ya saratani, kuimarisha huduma za uchunguzi (Magnetic Resonance Imaging - MRI). Hospitali za Abdalla Mzee na Wete Pemba pia zimeendelea kuimarishwa ili zifikie hadhi ya kuwa Hospitali za Mkoa.

19.0        Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Washirika mbali mbali wa Maendeleo katika utekelezaji wa Miradi/Programu za  Afya ikiwemo; Programu ya Kuimarisha Miundombinu ya Afya, Programu ya Kudhibiti Maradhi ya Malaria, Mradi Shirikishi wa UKIMWI na Kifua Kikuu, Programu Shirikishi ya Huduma za Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto na Mradi wa Taaluma za Afya. Ni matumaini yangu kuwa shughuli zote hizi zilizopangwa zitatekelezwa kwa ufanisi na kwa maslahi ya wananchi wote.

20.0        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Uwezeshaji, Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto za ajira kwa kuwajengea uwezo vijana ili waweze kujiajiri na kuajirika. Aidha, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Serikali inaendelea kusimamia jukumu la kutoa mitaji kwa wananchi wenye kipato kidogo ili watumie katika shughuli za uzalishaji mali kwa kujiajiri na kupunguza umasikini. Mfuko huo umefanikiwa kutoa jumla ya mikopo 307 yenye thamani ya Shilingi Milioni 467,278,000. Mikopo hiyo imeelekezwa katika shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, kazi za mikono, usindikaji matunda, viwanda vidogo vidogo vya mafuta ya nazi na mafuta ya mgando pamoja na viwanda vya sabuni za kufulia na kukogea.

21.0        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Ujenzi, Serikali inaendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara mbali mbali za Unguja na Pemba ili kuimarisha huduma za usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyengine. Katika kipindi cha 2015/2016 miongoni mwa Barabara zinazoendelea na ujenzi ni pamoja na Ole - Kengeja yenye urefu wa kilomita 35, Jendele – Cheju - Kaebona yenye urefu wa kilomita 11.6 na Koani - Jumbi yenye urefu wa kilomita 6.4. Aidha, matengenezo makubwa ya barabara yamefanyika kwa barabara kuu na za ndani.  

22.0        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uimarishaji wa usafiri wa anga, Serikali inaendelea na kazi ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume na kazi hiyo inategemewa kukamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018.

 

MASUALA MTAMBUKA:

Mazingira:

23.0        Mheshimiwa Spika, utunzaji wa mazingira ni suala la lazima na ni muhimu kulitekeleza ili kuleta maendeleo endelevu na kupunguza umasikini nchini kwetu. Nchi zote duniani na mashirika mbali mbali ya kimataifa yanatoa kipaumbele katika suala la kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ili kupunguza athari zinazotokana na hali hiyo. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekuwa ikihimiza wananchi kutunza maeneo ya misitu na kupanda miti kwa wingi maeneo ya wazi ikiwemo fukwe za bahari pamoja na kuachana na tabia ya kukata miti ovyo na uchimbaji wa rasilimali zisizorejesheka.
Athari za mvua za Masika:
24.0        Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 17 Aprili, 2016 ilinyesha mvua kubwa iliyofikia milimita 212.4 na kusababisha mafuriko katika maeneo mengi hasa ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Kufuatia mvua hiyo, jumla ya nyumba 3,330 zenye kaya 4,712 ziliathirika na kuilazimu Serikali kufungua kambi maalum katika Skuli ya Mwanakwerekwe C ili kuwahudumia wananchi hao.  Jumla ya watu 420 walihifadhiwa na kupatiwa huduma mbali mbali za kibinaadamu katika kambi hiyo. Athari nyengine zilizotokana na mvua hizo ni upotevu wa maisha ya mtu mmoja pamoja na kupotea kwa mali za wananchi. Nachukua fursa hii kuwapa pole wale wote waliopata athari ya mvua hizi. Naomba kuwanasihi wananchi wenzangu tuache kujenga katika maeneo ya mabondeni na katika njia za maji. Aidha, naziagiza Mamlaka zinazohusika na utoaji wa viwanja na vibali vya ujenzi wafuate taratibu zilizowekwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
   Kipindupindu:
25.0        Mheshimiwa Spika, mwanzoni mwa mwezi wa Septemba 2015, visiwa vyetu vya Zanzibar vilikabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa maradhi ya kuharisha na kutapika yaliyoripotiwa katika Vituo vya Afya vilivyopo Unguja na Pemba. Baada ya kupata matokeo ya uchunguzi wa kimaabara, ilithibitika kuwepo kwa mripuko wa maradhi ya kipindupindu. Kufuatia mripuko huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo, imeendelea kuchukua jitihada za dhati katika kukabiliana na maradhi haya.
26.0      Mheshimiwa Spika, Serikali ilifungua kambi maalum za matibabu ya kipindupindu Unguja na Pemba, ambapo hadi kufikia tarehe 11 Mei, 2016 jumla ya wagonjwa 3,897 walilazwa na kutibiwa. Kati ya hao, wagonjwa 2,450 walilazwa katika kambi za Unguja na wagonjwa 1,447 walilazwa katika kambi za Pemba. Jumla ya wagonjwa 59 wameripotiwa kufariki (46 Unguja na 13 Pemba).

27.0        Mheshimiwa Spika, mripuko wa maradhi haya katika kipindi hiki, umechukua muda mrefu zaidi kuliko miaka ya nyuma. Sababu kubwa zilizopelekea hali hiyo ni wananchi kutofuata kanuni za afya na usafi wa mazingira.  Hata hivyo, ni jambo linalotia matumaini kuona kwamba maradhi haya tumeanza kuyadhibiti baada ya kuchua hatua mbali mbali. Nawaomba wananchi tuongeze juhudi za kusafisha mazingira yetu pamoja na kufuata miongozo na kanuni za afya. Aidha, nachukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati watendaji wote ambao kwa namna moja ama nyengine wanashiriki katika hatua za kulitokomeza janga hili.

  Masuala ya Watu Wenye Ulemavu:

28.0           Mheshimiwa Spika, suala la udhalilishaji kwa Watu wenye Ulemavu  ikiwemo ubakaji, kupigwa, kutelekezwa, kuitwa majina mabaya na kunajisiwa ni kubwa katika jamii yetu. Serikali inaendelea na juhudi za kudhibiti vitendo hivi vya udhalilishaji na itaendelea kuchukua hatua kwa wale wote watakaojihusisha na vitendo hivyo. Kwa mantiki hiyo, naviagiza vyombo vya kusimamia haki na sheria kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuzishughulikia kesi za namna hii kwa haraka na kuwapatia haki watu wenye ulemavu ili kulinda utu wao. Pia, naiasa jamii kuacha vitendo vya udhalilishaji kwa Watu Wenye Ulemavu kwani wao pia ni binaadamu na wanastahiki kuheshimiwa na kutendewa haki na kupatiwa fursa sawa katika jamii.

Uwajibikaji, Utawala Bora na Mapambano dhidi ya Rushwa:

29.0        Mheshimiwa Spika, wakati wa kulizindua Baraza lako hili Tukufu tarehe 05 Aprili, 2016 Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alilikemea kwa nguvu zake zote suala la rushwa na kusisitiza masuala ya uwajibikaji na utawala bora. Katika kufikia azma hiyo Serikali inaendelea kutekeleza Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar Namba 1 ya mwaka 2012 pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 4 ya mwaka 2015. Hatua za utekelezaji wa Sheria hizi unaendelea ambapo hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amemteuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Maadili ya Viongozi ili Tume hiyo iweze kuanza kazi rasmi.

Hali ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI:

30.0        Mheshimiwa Spika, kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI hapa Zanzibar ni asilimia 1 na kuwa ni miongoni mwa nchi chache kusini mwa Jangwa la Sahara yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya UKIMWI. Maambukizi haya yanawaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume kwa uwiano wa 3 kwa 1. Hata hivyo, kuna makundi maalum ambayo kiwango cha maambukizi ni kikubwa ukilinganisha na kile kilichomo katika jamii. Makundi hayo ni wanawake wanaojiuza (19.3), wanaojidunga dawa za kulevya (11.3) na wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao (2.9). Serikali itaendelea na jitihada za kupambana na ongezeko la maambukizi kwa makundi yote haya na jamii kwa jumla. Natoa wito kwa wananchi kuendelea kubadili tabia na kudhibiti mazingira hatarishi kwa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kuacha kuwanyanyapaa watu wenye maambukizo ya Virusi vya UKIMWI.

Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya:

31.0        Mheshimiwa Spika, Dawa za Kulevya bado ni tatizo sugu duniani kote na hapa Zanzibar linaendelea kutuathiri siku hadi siku. Hali halisi inaonesha kwamba vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa ndio wanaoathirika zaidi na matumizi ya dawa hizo.  Katika kupambana na changamoto hii Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuchukua hatua za kuondoa kabisa usafirishaji na usambazaji, matumizi na athari zinazotokana na matumizi ya dawa hizo. Hivyo, nachukua fursa hii, kuvitaka vyombo vyote vinavyosimamia udhibiti wa dawa za kulevya kufanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya udhibiti wa dawa hizo.

MALENGO NA UTEKELEZAJI WA KAZI ZA KAWAIDA NA MIRADI YA MAENDELEO KWA KIPINDI CHA MIEZI TISA (JULAI-MACHI) 2015/2016:

32.0        Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi tisa (Julai - Machi) cha mwaka wa fedha 2015/2016, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake imechukua juhudi kubwa katika kutekeleza malengo iliyojipangia katika Programu zake kama ifuatavyo:-

1.  Programu ya Uratibu wa Shughuli za Makamu wa Pili wa Rais (C011):

33.0        Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Programu hii imetekeleza kazi zifuatazo:-
i)             Ofisi imeratibu ziara 16 za ndani ya nchi pamoja na kutekeleza ahadi 10 za masuala mbali mbali zilizoahidiwa na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais;
ii)            Ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi na Taasisi mbali mbali za ndani na nje ya nchi, Kikanda na Kimataifa, Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais alikutana na Wageni Mashuhuri na Mabalozi wa nchi 14.
iii)           Ofisi imefanya matengenezo makubwa katika nyumba ya makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais Mazizini na Dar es Salaam;
iv)           Ofisi imempatia mafunzo ya muda mrefu mfanyakazi mmoja nje ya nchi.  Aidha imewalipa stahiki za likizo wafanyakazi watano (5).
2. Programu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali (CO12):

34.0        Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Programu hii imetekeleza kazi zifuatazo: -
i.              Ofisi imetayarisha Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu  Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 - 2015 kwa kipindi cha miaka mitano (Novemba, 2010 hadi Julai, 2015).
ii.             Ofisi imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, ikiwa ni pamoja na kufuatilia marejesho ya matumizi ya fedha za mwaka 2014/2015 pamoja na kufuatilia miradi iliyotekelezwa kwa ufadhili wa Mfuko huo. Pia, Ofisi imeandaa Rasimu ya Kanuni ya Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ambayo inatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
iii.            Ofisi imeratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) unaotekelezwa katika Shehia 204 (Unguja 126 na Pemba 78).  Katika kipindi cha miezi tisa, Ofisi imefanya malipo kwa Kaya Masikini 33,632 (Unguja 18,944 na Pemba 14,688) ambapo jumla ya Shilingi 6,188,276,000 zimelipwa. Aidha, mafunzo ya wataalamu 20 wa kisekta kuhusu uibuaji na usanifu wa miradi 94 ya kutoa ajira za muda (Unguja 43 na Pemba 51) yamefanyika. Mafunzo juu ya kujaza fomu za masharti ya elimu na afya yametolewa kwa watumishi wa vituo vya afya na walimu 338 (Unguja 135 na Pemba 203) wa skuli zinazohusika na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kwa Unguja na Pemba.
iv.           Ofisi imeandaa muundo mpya na kutayarisha mapendekezo ya uendeshaji wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam.
v.            Ofisi  imetoa mafunzo ya kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa wanafunzi wa skuli za Msingi na Sekondari kwa Wilaya za Kusini, Kati na Kaskazini ‘B’ kwa Unguja, Mkoani na Chake Chake kwa Pemba ambapo jumla ya wanafunzi 500 wa Skuli za Msingi na 490 wa Sekondari wamepatiwa mafunzo hayo.
vi.           Ofisi imeratibu na kutoa huduma katika majanga na maafa yaliyotokea ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba yakiwemo maafa ya mafuriko, ajali za moto na maradhi ya kipindupindu.
vii.          Ofisi imeendesha mafunzo kwa wafanyakazi 22 wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, watano (5) kutoka Wilaya tano za Unguja na Pemba na mmoja kutoka ZBC radio walishiriki katika ziara ya kimafunzo ya wiki moja juu ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika Wilaya za Kinondoni, Kilosa na Chamwino Tanzania Bara. Aidha, makongamano matatu ya kujiandaa na kukabiliana na maafa yameendeshwa kwa wanafunzi kutoka Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (ZIFA) kwa upande wa Unguja pamoja na Chuo cha Ualimu Benjamin Mkapa kwa upande wa Pemba.
viii.         Ofisi imeratibu Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kusimamia kilele cha Sherehe hizo zilizofanyika tarehe 12 Januari, 2016 Uwanja wa Amaan.
ix.           Ofisi imeratibu Hitima na Dua ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui tarehe 7 Aprili, 2016.
x.            Ofisi imejenga kaburi la Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Nne, Marehemu Sheikh Idris Abdulwakil huko Makunduchi na kuendelea kusimamia mazingira ya eneo lilipo kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, Kisiwandui.

3. Programu ya Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa (C013):
35.0        Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Programu hii imetekeleza yafuatayo: -
i.              Ofisi imetayarisha Rasimu ya Sheria inayoipa mamlaka Kiwanda cha Upigaji chapa iwe Taasisi inayojitegemea.
ii.             Ofisi imechapisha nyaraka na machapisho mbali mbali ya Serikali kama vile Gazeti Rasmi la Serikali, Miswaada ya Sheria, Sheria na machapisho mengine yaliyowasilishwa kiwandani kwa mujibu wa mahitaji ya Taasisi husika.
iii.            Ofisi imenunua mitambo mipya kwa awamu ya pili ambayo tayari imeshaanza kufungwa kiwandani.

4. Programu ya Mipango na Utawala (C014):

36.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Programu hii imetekeleza kazi zifuatazo:-
i.              Ofisi imefanikiwa kununua vifaa mbali mbali vya kuendeshea kazi ikiwa ni pamoja na kompyuta tatu (3); Aidha, Ofisi imelipia huduma za maji, umeme, mawasiliano pamoja na kufanya matengenezo madogo madogo ya Ofisi.
ii.             Ofisi imewapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi 28, wafanyakazi 27 wapya wamepatiwa mafunzo ya  awali (Induction Course) pamoja na kulipia stahiki za likizo kwa wafanyakazi 72.
iii.            Ofisi imefanya  kikao kimoja cha Kamati ya Uongozi, vikao vitatu vya Kamati ya Ukaguzi na kikao kimoja cha kujadili makisio ya mishahara na maposho ya wafanyakazi. Aidha, Ofisi  imeratibu na kusimamia vikao vitatu vya Bodi ya Zabuni na kuendelea kulifanyia mapitio daftari la mali za Serikali.
iv.           Ofisi inaendelea na utayarishaji wa ripoti ya tathmini ya mahitaji ya mafunzo ili kuandaa mpango mkuu wa mafunzo.
v.            Ofisi imeandaa Taarifa za Utekelezaji kwa kipindi cha mwaka mzima 2015/2016, miezi sita (6) Julai - Disemba na taarifa ya Utekelezaji miezi mitatu (Oktoba – Disemba) 2015/216. Aidha, Ofisi imetayarisha Mpango wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
vi.           Ofisi kwa kupitia kitengo cha Kusimamia miradi ya Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na maradhi hayo (ZGFCCM) imeendesha  vikao viwili vya robo  mwaka vya kawaida na Kikao kimoja cha dharura pamoja na vikao vyengine vya Kamati vikiwemo Kamati ya “Oversight ommittee”, Kamati Tendaji na Kamati ya Fedha. Aidha, Kitengo kimefanya uchaguzi wa kuwapata wajumbe wake katika majimbo saba ya ZGFCCM ambayo yanaundwa na Sekta tofauti.

BARAZA LA WAWAKILISHI:

Programu ya 1: Kutunga Sheria, kupitisha Bajeti na kusimamia Taasisi za Serikali (CO21):

 Programu ya 2: Uongozi na Utawala wa Baraza la Wawakilishi (CO22):
37.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza la Wawakilishi limetekeleza yafuatayo:-
i.              Ofisi kupitia Baraza la Wawakilishi limekamilisha mkutano wa ishirini ambao ulikuwa ni wa mwisho kwa Baraza la Nane (2010 – 2015).
ii.             Ofisi kupitia Baraza la Wawakilishi ilisimamia uzinduzi wa Baraza jipya la Tisa.
iii.            Mafunzo elekezi juu ya majukumu ya Mjumbe wa Baraza la tisa (9) yalitolewa.
iv.           Ofisi imewapatia mafunzo watumishi 17 katika ngazi na fani mbali mbali, kama vile Sheria, Utawala.  Utawala wa Fedha, Utawala wa rasilimali Watu.  Ukatibu Muktasi, Ukutubi, na Ukarani masjala kwenye ngazi ya Digrii ya Kwanza.  Digirii ya Juu na Digrii ya Uzamivu.

TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR:

Programu ya 1:  Uendeshaji wa Shughuli za Uchaguzi:

Programu ya 2: Usimamizi wa Kazi za Utawala na Uendeshaji wa Shughuli za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar:

38.0        Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Tume ya Uchaguzi imetekeleza yafuatayo:-
i.          Ofisi kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeendesha na kusimamia Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Madiwani.
ii.         Ofisi imesomesha wafanyakazi wawili kwa kiwango cha Shahada ya Pili na Shahada ya Kwanza kwa lengo la kuongeza taaluma na kuleta ufanisi zaidi katika utendaji wa kazi.  Aidha, wafanyakazi watatu walipatiwa mafunzo ya muda mfupi nchini Afrika ya Kusini yanayohusiana na mambo ya Uchaguzi.
iii.        Ofisi iliandaa Semina kwa Majaji na Mahakimu kwa lengo la kutatua migogoro na kesi za uchaguzi.
iv.       Ofisi imeendesha makongamano kwa vijana ili wapate uelewa zaidi kuhusiana na Uchaguzi, kwa lengo la kuwaepusha kujiingiza katika vurugu.
v.        Ofisi kupitia Tume ya Uchaguzi kwa kushirikikiana na UNDP iliandaa Semina kwa Vyama vya Siasa, vilivyoshiriki katika Uchaguzi.
vi.       Ofisi kupitia Tume ya Uchaguzi kwa kushirikiana na UNDP imetoa elimu ya Mpiga Kura katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kwa lengo la kuwawezesha wapiga kura kupata uelewa mzuri wa Uchaguzi.
vii.      Ofisi imenunua vifaa vya kuweka kumbukumbu za wapiga kura zikiwemo sava, kompyuta na printa za kuchapisha kadi pamoja na kulipia huduma za mitandao.

UTEKELEZAJI KIFEDHA KWA PROGRAMU:

39.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 625,568,698 kwa ajili ya Programu ya Uratibu wa Shughuli za Makamu wa Pili wa Rais.  Hadi kufikia mwezi Machi, 2016 jumla ya Shilingi 357,646,714 zilipatikana na kutumika kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 57.2 Kiambatisho Nam. 1
40.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016 Programu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ilipangiwa kutumia jumla ya Shilingi 2,239,727,000 kwa kazi za kawaida. Hadi kufikia mwezi wa Machi 2016, Programu hii imeingiziwa jumla ya Shilingi 1,397,031,987 ikiwa ni sawa na asilimia 62.  Kiambatisho Nam. 1.
41.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 714,050,000 kwa Programu ya Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa.  Hadi kufikia Machi 2016 jumla ya Shilingi 479,710,617 zimetumika kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 67. Kiambatisho Nam. 1.

42.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 1,587,354,000 kwa Programu  ya Mipango na Utawala. Hadi kufikia Machi 2016 jumla ya Shilingi 949,727,773 zimetumika kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 60. Kiambatisho Nam. 1.

43.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 16,762,600,000 kwa programu za Baraza la Wawakilishi. Hadi kufikia Machi 2015 jumla ya shilingi jumla ya Shilingi. 4,546,691,512 zimetumika kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 27. Kiambatisho Nam. 1.

44.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 1,404,000,000 kwa  programu za Tume ya Uchaguzi. Hadi kufikia Machi, 2015 jumla ya  Shilingi 885,251,255 zimetumika kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 63. Kiambatisho Nam. 1.

UKUSANYAJI WA MAPATO:

45.0        Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais   inakusanya mapato kutoka Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa. Katika kipindi cha Miezi Tisa (Julai - Machi 2015/2016), Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi 600,000,000. Hadi kufikia Mwezi Machi, 2016 Ofisi imekusanya jumla ya Shilingi 279,145,120 sawa na asilimia 47 ya lengo. Aidha, Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi 12,360,000. Hadi kufikia mwezi wa Machi 2016, Ofisi imekusanya Shilingi 10,180,000  sawa na asilimia 82 Kiambatisho Nam. 2.

UTEKELEZAJI KWA TAASISI ZILIZOHAMISHIWA OFISI YA

MAKAMU WA PILI WA RAIS:


46.0        Mheshimiwa Spika, kufuatia mabadiliko ya Muundo wa Serikali yaliyofanyika katika Serikali ya Awamu ya Saba kipindi cha Pili, Idara moja (1) na taasisi mbili (2) zilizokuwa chini ya iliyokuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Taasisi hizo ni:-
i.      Idara ya Watu Wenye Ulemavu
ii.     Tume ya Kitaifa ya Kudhibiti na Uratibu wa Dawa za Kulevya
iii.    Tume ya UKIMWI

IDARA YA WATU WENYE ULEMAVU:

     Programu ya Usimamizi wa Masuala ya Watu
      Wenye Ulemavu:


47.0        Mheshimiwa Spika, kazi za Programu hii zimetekelezwa na Idara ya Watu Wenye Ulemavu kama ifuatavyo:-
              i.        Ofisi imehudhuria Mikutano ya kupitia na kuandaa mpango kazi na Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya Afrika Mashariki iliofanyika Dar es Salaam na Kampala, Uganda.
             ii.        Ofisi imetoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya upatikanaji wa haki na fursa kwa Watu Wenye Ulemavu kupitia vipindi vya redio na televisheni, midahalo ya wanafunzi pamoja na mikutano iliyofanywa kwa taasisi za umma na binafsi, vikundi vya watu wenye ulemavu pamoja na kuzitembelea familia zenye watu wenye ulemavu Unguja na Pemba.
            iii.        Ofisi kwa kushirikiana na watu binafsi imewapatia visaidizi Watu Wenye Ulemavu 48 (21 wanawake na 27 wanaume) Unguja na Pemba. Visaidizi hivyo ni pamoja na Viti vya magurudumu mawili, viti vya chooni, magongo ya kutembelea na kusimamia.

 TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA:

            Programu ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya:
            Programu ya Mipango na Utawala wa Tume ya  Kitaifa ya Kuratibu
             na Udhibiti wa Dawa za Kulevya:  

48.0         Mheshimiwa Spika, kazi za Programu hizi zimetekelezwa na Tume ya Kitaifa ya Kudhibiti na Uratibu wa Dawa za Kulevya kama ifuatavyo:-
i.      Ofisi imerusha hewani vipindi vinne (4) vya redio  kwa lengo la kuelimisha jamii  juu ya athari za Dawa za Kulevya, kufanya ziara za utoaji taaluma  kwenye Skuli 38  ambapo jumla ya wanafunzi 1620 (Wanawake 913,  Wanaume 707) walipatiwa taaluma hiyo. Pia ziara kama hizo zimefanyika kwenye Shehia  16 za Unguja na Pemba.
ii.     Ofisi imezipatia ruzuku nyumba 13 za Makaazi ya Vijana walioacha matumizi ya Dawa za Kulevya (Sober Houses).
iii.    Ofisi kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya  pamoja na wadau wengine imeandaa muongozo wa kuwazawadia watoa taarifa kuhusu uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya ambapo muongozo huo unasubiri vikao vya Tume kwa ajili ya kupatiwa mapendekezo.

                 TUME YA UKIMWI:


Programu ya Kuratibu Muitiko wa Taifa wa Ukimwi:

                       Programu ya Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Ukimwi:
                  
49.0         Mheshimiwa Spika, kazi za Programu hizi zimetekelezwa na Tume ya UKIMWI kama ifuatavyo:-
i.      Ofisi kupitia Tume ya UKIMWI imetoa mafunzo ya Sheria ya Kukinga na Kusimamia Masuala ya UKIMWI Zanzibar (Nam.18 ya mwaka 2013) kwa wadau mbali mbali. Aidha, Ofisi imetoa mafunzo kwa Viongozi 50 wa Taasisi za Kidini za Kiislamu na Kikiristo Unguja na Pemba juu ya muongozo wa Taasisi za Kidini wa masuala ya UKIMWI na afya ya uzazi kwa lengo la kuutambua muongozo huo na kuufanyia kazi.
ii.     Ofisi imeandaa Mkakati wa Tatu wa Taifa wa UKIMWI kwa mwaka 2016/2020 kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali ambao walitoa maoni ya vipaumbele, shabaha  na dira ya mkakati huo.
iii.    Ofisi imeandaa Jarida la JIHADHARI kwa kuchapisha nakala 5000 na kusambazwa.
iv.   Ofisi imefanya ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za UKIMWI ambapo ilifanya ziara kwa wadau 16 na Shehia 49 Unguja na Pemba zinazotekeleza shughuli mbali mbali za UKIMWI.
v.    Ofisi imetoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya UKIMWI kupitia vipindi vya redio, filamu, maonyesho ya sanaa pamoja na kuwapatia mafunzo ya stadi za maisha vijana wenye ulemavu wa uziwi 60 na mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana  28 kutoka makundi maalum juu ya mbinu za kujiongezea kipato ili kuepukana na tabia hatarishi.

UTEKELEZAJI KIFEDHA:


Mheshimiwa Spika, Utekelezaji kifedha kwa Idara na Taasisi hizi mbili ulikuwa kama ifuatavyo:-

50.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 289,782,000 kwa Idara ya Watu Wenye Ulemavu. Hadi kufikia Machi, 2016 jumla ya Shilingi 25,680,000 zimetumika kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 8.8.

51.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya shilingi 544,383,451 kwa Tume ya UKIMWI. Hadi kufikia Machi, 2016 jumla ya Shilingi 343,711,200 zimetumika ambazo ni sawa na asilimia 60.

52.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shilingi 351,218,753 kwa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Hadi kufikia Machi, 2016 jumla ya Shilingi 237,449,000 zimetumika ambazo ni sawa na asilimia 70.

BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017:

53.0        Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya Muundo wa Serikali yaliyofanyika, Programu zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais pamoja na Taasisi zake zimeongezeka kutoka programu kuu nane (8) na programu ndogo 14 hadi kufikia programu kuu kumi na mbili (12) na programu ndogo ishirini na nne (24).  Zifuatazo ni Programu Kuu:
i.                    Uratibu wa Shughuli za Makamu wa Pili wa Rais
ii.                   Uratibu wa shughuli za Serikali
iii.                  Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa
iv.                 Mipango na Utawala
v.            Kutunga Sheria, kupitisha Bajeti na kusimamia Taasisi za Serikali
vi.                 Uongozi na Utawala wa Baraza la Wawakilishi
vii.                Uendeshaji wa Shughuli za Uchaguzi
viii.         Usimamizi wa Kazi za Utawala na Uendeshaji wa Shughuli za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
ix.                 Udhibiti wa Dawa za Kulevya
x.            Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
xi.                 Kuratibu Muitiko wa Taifa wa UKIMWI
xii.                Utawala na Uendeshaji wa Tume ya UKIMWI

54.0        Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake inatarajia kutumia jumla ya Shilingi 35,992,076,000 kwa ajili ya kutekeleza program hizo kumi na mbili (12).

Programu ya kwanza: Uratibu wa Shughuli za Makamu wa Pili wa Rais (C011):

55.0        Mheshimiwa Spika, lengo la Program hii ni kuimarisha utendaji wa kazi kwa Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Pili wa Rais.  Matarajio ya muda mrefu ni kuimarika kwa Ofisi hii na kutoa huduma bora kwa Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.   Huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kuratibu kazi za Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais ikiwemo ziara za ndani na nje ya nchi, mikutano na Mabalozi wa nchi mbali mbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa na mikutano na wananchi ya kusikiliza kero na malalamiko yao.

56.0       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Idara ya Faragha kupitia Programu ya (C011) ya Uratibu wa Shughuli za  Makamu wa Pili wa Rais imepanga kufanya yafuatayo:-
a)    Kuimarisha Ofisi ya Faragha kwa kuendelea kuratibu ziara mbali mbali za ndani na nje ya nchi.
b)   Kuimarisha uhusiano mwema na nchi rafiki kwa kuongeza mashirikiano kwa kukaribisha wageni na Mabalozi wa nchi mbali mbali wa Kitaifa na Kimataifa.
c)    Kuratibu na kutekeleza ahadi zinazolenga kuleta maendeleo katika jamii.
d)    Kuyafanyia matengenezo makubwa Makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais yaliyoko Dar es Salaam na Dodoma pamoja na kuimarisha huduma za usafiri.
e)    Kuendelea kuwapatia mafunzo wafanyakazi watatu (3) wa Ofisi ya Faragha katika kiwango cha Diploma pamoja na kuwapatia stahiki za likizo wafanyakazi tisa (9).

Programu ya Pili: Uratibu wa shughuli za Serikali (C012):


57.0        Mheshimiwa Spika, programu hii lengo lake kubwa ni kuweka mfumo imara na endelevu kwa Uratibu wa Shughuli za Serikali, ambapo matarajio ya muda mrefu ni kutoa huduma bora za Serikali kwa jamii.  

Programu hii ina programu ndogo tano ambazo ni: -
i.      Kukabiliana na Maafa
ii.     Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa.
iii.    Shughuli za SMZ, SMT, Utafiti na Masuala ya Muungano.
iv.   Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dar es Salaam
v.    Usimamizi wa masuala ya watu wenye mahitaji maalum.

Programu ndogo C0121 Kukabiliana na Maafa:

58.0         Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya Kukabiliana na Maafa  ina lengo la kujenga uhimili wa jamii katika kukabiliana na maafa kabla na baada ya kutokea. Huduma ambazo zinazotarajiwa kutolewa ni Uratibu wa shughuli za Kukabiliana na Maafa ikiwemo kutoa mafunzo kwa jamii, kuwahudumia waathirika wa majanga na maafa pamoja na kuandaa na kutoa miongozo inayosimamia utekelezaji wa kazi za maafa.

59.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kupitia Programu ndogo (C0121) imepanga kufanya yafuatayo:-
a)        Kufanya tathmini na kutoa mafunzo ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa kwa Shehia 50 za Unguja na Pemba.
b)       Kuijengea uwezo Kamisheni katika kujikinga, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa.
c)        Kuandaa Kanuni ya Sheria ya Kukabiliana na Maafa Namba 1 ya mwaka 2015.
d)        Kuendelea kuandaa na kutoa miongozo inayosimamia utekelezaji wa kazi za maafa.

Programu ndogo C0122: Uratibu wa Shughuli za Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa:


60.0        Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa ina lengo la kuwa na Sherehe zenye hadhi na kudumisha historia na kumbukumbu za Viongozi Wakuu wa Kitaifa.  Huduma ambazo zinatarajiwa kutolewa ni Uratibu wa shughuli za Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa.

61.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kupitia Programu ndogo (C0122) ya Uratibu wa Shughuli za Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa imepanga kufanya yafuatayo:-
a)          Kuandaa mazingira mazuri ya Ofisi na utendaji kazi kwa kununua vitendea kazi na kuendelea kulipia gharama za masomo kwa wafanyakazi wawili (2).
b)         Kuratibu Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
c)          Kuratibu Hitma na Dua ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Viongozi wengine waliotangulia mbele ya haki.
d)          Kuratibu ushiriki wa Viongozi na wananchi wa Zanzibar katika maadhimisho na sherehe za Kitaifa zitakazofanyika nje ya Zanzibar.
e)          Kukamilisha mapitio ya Sheria Namba 10 ya mwaka 2002 ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa.

Programu ndogo (C0123): Shughuli za SMZ, SMT, Utafiti na Masuala ya Muungano:


62.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Programu ndogo ya Uratibu wa Shughuli za SMZ, SMT, Utafiti na Masuala ya Muungano (C0123) imepanga kufanya yafuatayo:-
a)            Kuimarisha mfumo wa uratibu wa shughuli za Serikali
b)           Kuratibu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala (CCM) ya 2015 hadi 2020.
c)            Kuratibu shughuli za Muungano na Miradi ya Muungano ndani ya Zanzibar, ikiwa ni pamoja na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III).
d)            Kuratibu shughuli za utafiti nchini.

Programu Ndogo C0124:   Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dar es Salaam:

63.0        Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dar es Salaam ina lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa Taasisi za SMZ kwa upande wa Tanzania Bara. Huduma inayotolewa ni Uratibu wa shughuli za Serikali (SMZ) Dar es Salaam.

64.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Dar es Salaam kupitia Programu ndogo (C0122) imepanga kufanya yafuatayo:-
a)            Kuimarisha mashirikiano baina ya Ofisi ya uratibu shughuli za Serikali Dar es Salaam na Taasisi za SMZ na SMT, Ofisi za Kibalozi na Taasisi za Kimataifa.
b)           Kukamilisha muundo mpya wa kitaasisi na kiutumishi wa Ofisi.
c)            Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Ofisi kwa ununuzi wa vifaa vya Ofisi na samani.
d)            Kuwapatia mafunzo wafanyakazi wawili (2) ili kuwaongezea utaalamu.
e)            Kufanya maandalizi ya awali ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Dar es Salaam.

Programu Ndogo C0125:  Usimamizi wa Masuala ya Watu Wenye Ulemavu:

65.0        Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya Usimamizi wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu ambapo lengo lake ni kupatikana kwa haki na fursa sawa kwa Watu wenye Ulemavu. Huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kuimarishwa ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu, uwezeshwaji wa watu wenye ulemavu na kukuza uelewa wa jamii juu ya watu wenye ulemavu.

66.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Idara ya Watu  Wenye Ulemavu kupitia Programu ndogo (C0125) ya Usimamizi wa Masuala ya Watu Wenye Ulemavu imepanga kutekeleza yafuatayo:
a)            Kupitia upya Sheria Nam. 9 2006 (HAKI NA FURSA) ya Watu wenye Ulemavu.
b)           Kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za Watu wenye Ulemavu.
c)            Kusimamia upatikaji wa Haki na Fursa sawa za Watu wenye Ulemavu.
d)            Kufanya ukondoeshwaji, kuwajengea uwezo Watu wenye Ulemavu na taasisi zao na kufanya uhamasishaji wa jamii juu ya masuala ya Watu wenye Ulemavu.
e)            Kuimarisha mazingira ya kazi na kuwajengea uwezo wafanyakazi.

Programu ya Tatu: Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa (C013):

67.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii lengo lake ni kukiimarisha Kiwanda cha Upigaji Chapa ili kutoa huduma bora za machapisho na kwa ufanisi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 programu hii imepanga kutekeleza yafuatayo:
a)          Kutoa huduma bora za uchapishaji wa nyaraka na Sheria za Serikali.
b)         Kutangaza na kushajiisha uelewa wa utoaji huduma za Uwakala na Kiwanda kwa lengo la kuongeza idadi ya wateja na mapato.
c)          Kufanya maandalizi ya uanzishaji wa Bohari Kuu ya vifaa vya Ofisi.
d)          Kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa lengo la kutoa machapisho bora yanayoendana na teknolojia ya kisasa ya uchapishaji.

Programu ya Nne: Mipango na Utawala (C014):


68.0        Mheshimiwa Spika, lengo la Programu hii ni kuimarisha mazingira bora ya wafanyakazi, usimamizi wa mipango na shughuli za Ofisi. Matokeo yanayotarajiwa ni kuimarika mipango na utendaji kazi na kutoa huduma bora kwa wafanyakazi na wadau mbali mbali wa Ofisi hii. Programu hii ina programu ndogo tatu (3) ambazo ni:-
i.      Uongozi na Utawala
ii.     Mipango, Sera na Utafiti
iii.    Ofisi Kuu Pemba  

Programu ndogo (C0141): Uongozi na Utawala:


69.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ndogo ina lengo la kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi na usimamizi wa shughuli za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Matokeo yanayotarajiwa ni matumizi bora ya rasilimali, wafanyakazi wenye ujuzi na uzoefu na ufanisi katika utendaji kazi.  Huduma zinazotolewa ni kusimamia maslahi ya wafanyakazi na matumizi bora ya rasilimali za Ofisi.

70.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Ofisi kupitia programu ndogo ya Uendeshaji na Utumishi imepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-
a)              Kusimamia shughuli za uendeshaji wa Ofisi za kila siku ikiwemo malipo ya umeme, maji, mawasiliano, mafuta, vifaa vya usafi pamoja na vifaa vya kufanyia kazi.
b)             Kufanya ukarabati mdogo katika jengo kongwe la Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga.
c)              Kuimarisha huduma za usafiri.
d)              Kuimarisha Kitengo cha kumbukumbu kwa kukifanyia ukarabati pamoja na kuwekwa samani za kisasa na vifaa vya kufanyia kazi.
e)              Idara inaendelea kufanya mapitio ya mahitaji ya mafunzo (Training Need Assessment -TNA).
f)               Kuendelea kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi.
g)              Kufanya semina moja juu ya Sheria Nam. 2 ya mwaka 2011 na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2014 na Semina moja ya kujikinga na maambukizi na madhara ya UKIMWI pamoja na maradhi yasioambukiza kwa wafanyakazi 100.
h)              Kuandaa vikao vinne (4) vya Kamati ya Uongozi, Vikao vinne (4) vya Kamati ya Ukaguzi, Vikao vinne vya Bodi ya Zabuni pamoja na kuendelea kufanyia mapitio daftari la mali za Serikali kwa mujibu wa Sheria za Udhibiti wa mali za Serikali

Programu ndogo (C0142): Mipango, Sera na Utafiti:


71.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ndogo ina lengo la kuandaa na kusimamia Mipango na Bajeti na kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Matokeo yanayotarajiwa ni kuwa na mipango endelevu na yenye kuleta maendeleo. Huduma inayotolewa ni kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera, Mipango na Bajeti.

72.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Ofisi kupitia Programu ndogo (C0142) imepanga kufanya yafuatayo:-
    1. Kuandaa Bajeti na kutayarisha Miradi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na kufanya ziara nne (4) za ufuatiliaji wa utekelezaji wa Programu/ Miradi ya Maendeleo inayotekeleza chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
    2. Kusimamia tafiti zinazotekelezwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
    3. Kuratibu Sera na Sheria zinazotayarishwa kwa ajili ya shughuli zinazotekelezwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
    4. Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi yanayohusu ufuatiliaji na tathmini kwa kazi za kawaida na maendeleo na wafanyakazi watatu (3) mafunzo ya muda mrefu.
    5. Kuratibu utekelezaji wa Miradi ya Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kupitia Mfuko wa Dunia (Global Fund).

Programu ndogo (C0143): Ofisi Kuu Pemba:

73.0        Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Program hii ndogo ni Kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi na usimamizi wa shughuli za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Pemba. Matokeo yanayotarajiwa ni utendaji na utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba kwa ufanisi. Huduma inayotolewa ni Uratibu wa kazi za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba.

74.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha  2016/2017 Ofisi Kuu Pemba itatekeleza Lengo la Kuratibu shughuli  za Idara na Taasisi zilizo chini ya  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba kama ifuatavyo:- 
a)            Kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi na kusimamia shughuli za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
b)           Kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi wanne (4).
c)            Kuandaa mipango ya Ofisi na Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2017/2018.
d)            Kuimarisha kazi za usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa Programu na Miradi ya Maendeleo iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
e)            Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Serikali Pemba.
f)             Kutangaza huduma za Kiwanda kwa ajili ya kuongeza idadi ya wateja na mapato.

75.0        Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais pia inaratibu shughuli za Baraza la Wawakilishi,  Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na Tume ya UKIMWI, ambazo nazo zina Programu Kuu na Programu Ndogo kama ifuatavyo:-

BARAZA LA WAWAKILISHI:

76.0        Mheshimiwa Spika, Baraza la Wawakilishi linatekeleza Program kuu mbili (2) ambazo ni:-

Programu ya tano: Kutunga Sheria, kupitisha Bajeti na kusimamia Taasisi za Serikali:


77.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ina jukumu la kuhakikisha haki na utawala wa sheria unatekelezwa Zanzibar, ambapo matarajio yake ya muda mrefu ni kukua kwa demokrasia na uwakilishi wa wananchi. Huduma zinazotolewa ni kujadili, kurekebisha na kupitisha miswada ya Sheria, kusimamia utendaji wa Taasisi za Serikali na kupitisha bajeti ya Serikali.

Programu ya sita: Uongozi na Utawala wa Baraza la Wawakilishi:


78.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ina jukumu la kuweka mazingira mazuri ya kazi, kuwajengea uwezo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wafanya kazi wa Ofisi ya Baraza, ambapo matarajio yake ya muda mrefu ni kuongezeka kwa ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Ofisi. Huduma zinazotolewa ni kuwapatia Wajumbe na wafanyakazi wa Baraza huduma na stahiki zao, kuimarisha uwezo wa Wajumbe na watendaji na kuimarisha mazingira ya kazi ya Ofisi ya Baraza.

79.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 Baraza la Wawakilishi limepanga kutekeleza mambo yafuatayo:-
a)            Kufanya mikutano minne ya Baraza.
b)           Kuziwezesha Kamati zake za kudumu kufanya kazi
c)            Kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wake.
d)            Kuendeleza mahusiano na vyombo vyengine vya Mabunge, Kanda ya Afrika na ngazi ya Kimataifa.
e)            Kuendelea kutoa mafunzo kwa Wajumbe ili waweze kutekeleza majukumu yao.
f)             Kuendelea kutoa elimu kwa  Umma inayohusu majukumu ya Baraza kupitia Redio na Televisheni
g)            Kuendelea kuweka mazingira mazuri ya majengo na kumbi za mikutano.

TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR:

80.0        Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi inasimamia Programu kuu mbili kama zifuatazo:-

Programu ya saba: Uendeshaji wa Shughuli za Uchaguzi:

81.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ina jukumu la kukuza Demokrasia na Umoja wa Kitaifa ambayo matarajio yake ya muda mrefu ni kuwa na Uchaguzi Huru na wa haki na wenye kufuata misingi ya kisheria. Huduma zinazotolewa ni kufanya Uchaguzi Mkuu, Chaguzi ndogo na Kura ya maoni, Kufanya Uchambuzi wa Idadi, Majina na Mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi, Kuratibu na kutoa elimu ya Wapiga Kura pamoja na Uandikishaji wa Wapiga Kura na Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

82.0        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia programu hii imepanga kuendesha Chaguzi Ndogo.

Programu ya nane: Usimamizi wa Kazi za Utawala na Uendeshaji wa Shughuli za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar:


83.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ya pili ina jukumu la kuimarisha usimamizi wa mwenendo wa Shughuli za Uchaguzi, ambayo matarajio yake ya muda mrefu ni uendeshaji bora wa kazi za Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Programu hii inasimamia  programu ndogo mbili nazo ni:-
i.      Usimamizi wa kazi za Utawala na Uendeshaji wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
ii.     Usimamizi wa kazi za Utawala na Uendeshaji wa Ofisi Ndogo ya Tume ya Uchaguzi Pemba.

84.0        Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya Usimamizi wa kazi za Utawala na Uendeshaji wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ina lengo la kuimarisha Usimamizi wa mwenendo wa Shughuli za Uchaguzi. Matokeo yanayotarajiwa ni uendeshaji bora wa kazi za Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Huduma zinazotolewa na program hii ndogo ni kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi, kuimarisha maslahi ya wafanya kazi na kuwajengea uwezo wafanya kazi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

85.0        Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya Usimamizi wa kazi za Utawala na Uendeshaji wa Ofisi Ndogo ya Tume ya Uchaguzi Pemba ina lengo la kuimarisha Usimamizi wa mwenendo wa Shughuli za Uchaguzi Pemba. Matokeo yanayotarajiwa ni uendeshaji bora wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Huduma zinazotolewa na program hii ndogo ni kuimarisha mazingira mazuri ya kufanyia kazi ya Tume ya Uchaguzi Pemba.

86.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 Tume ya Uchaguzi kupitia programu hii imepanga kutekeleza mambo yafuatayo:-
a)            Kuweka na kusimamia mazingira mazuri ya utendaji kazi.
b)           Kuwapatia mafunzo wafanya kazi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA:

87.0        Mheshimiwa Spika, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya ina jukumu kuu la kuratibu mapambano dhidi ya matumizi, biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, kutoa taaluma kwa jamii juu ya athari za dawa za kulevya pamoja na tiba na ushauri nasaha kwa waathirika wa dawa hizo. Taasisi hii imepangiwa kusimamia Program Kuu mbili kama ifuatavyo:-

Program ya tisa: Udhibiti wa Dawa za Kulevya:

88.0        Mheshimiwa Spika, shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika programu hii ni:-
a)            Kuzijengea uwezo nyumba za upataji nafuu (sober houses).
b)           Kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya katika bandari zilizo na zisizo rasmi.
c)            Kuratibu na kuendeleza mapambano juu ya uingizaji, usambazaji na usafirishaji wa dawa za kulevya
d)            Kupunguza matatizo ya athari za utegemezi wa dawa za kulevya.

Programu ya kumi: Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya:


89.0        Mheshimiwa Spika, lengo kuu la programu hii ni kuweka mazingira mazuri ya kazi za ofisi. Huduma zinazotarajiwa ni upatikanaji wa huduma na vitendea kazi, kujenga uwezo wa wafanya kazi na usimamizi wa matumizi ya fedha pamoja na kukuza uwajibikaji.

90.0        Mheshimiwa Spika, Kazi za programu hii zinatekelezwa na Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na ina program ndogo mbili ambazo ni:
i.      Utawala wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya,
ii.     Uratibu wa Masuala ya Dawa za Kulevya Pemba.

Mheshimiwa Spika, shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika programu hii ni:-

a)    Kuweka mazingira mazuri ya kazi na kusimamia utekelezaji wake.
b)   Kujenga uwezo wa wafanyakazi katika mapambano ya dawa za kulevya.
c)    Kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi wafanya kazi.

TUME YA UKIMWI:

91.0        Mheshimiwa Spika, Tume ya Ukimwi ina jukumu la kuratibu masuala ya UKIMWI hapa Zanzibar,  ambapo imepangiwa kusimamia Programu Kuu mbili kama ifuatavyo:-

Programu ya kumi na moja:  Uratibu wa Muitiko wa Taifa wa UKIMWI:


92.0        Mheshimiwa Spika, Programu hii ina programu ndogo mbili   ambazo ni:
i) Uratibu wa muitiko wa Taifa wa UKIMWI.
ii) Mawasiliano na Utetezi wa Masuala ya UKIMWI

93.0        Mheshimiwa Spika, shughuli zilizopangwa kutekelezwa na programu hii ni:
a)            Kuongeza uelewa wa masuala ya UKIMWI na afya ya uzazi na matumizi ya huduma kwa makundi ya vijana na rika baleghe (10 – 24).
b)           Kujenga uwezo wa wadau na jamii  kutekeleza Mkakati wa Tatu utakaochangia kudhibiti kuenea UKIMWI, udhalilishaji wa kijinsia na kuimarisha masuala ya afya ya uzazi.
c)            Kutekeleza programu za ushawishi na mawasiliano kwa ubunifu zaidi na kukabiliana na changamoto mpya.
d)            Kusimamia mfumo wa ufuatiliaji na tathmini uendelee kufanya kazi.
e)            Kujenga uelewa wa jamii wa Sheria ya Kukinga na Kusimamia Masuala ya UKIMWI Nam. 18 ya mwaka 2013.
f)             Kuendeleza maandalizi ya uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa UKIMWI.

Program ya kumi na mbili: Utawala na Uendeshaji wa Tume ya UKIMWI:


94.0        Mheshimiwa Spika, lengo kuu la programu hii ni kuweka mazingira mazuri ya kazi za ofisi. Huduma zinazotarajiwa ni upatikanaji wa huduma na vitendea kazi, kujenga uwezo wa wafanyakazi na usimamizi wa matumizi ya fedha, uwazi na uwajibikaji. Programu hii imepangiwa kusimamia programu ndogo mbili ambazo ni: -
i.      Uratibu wa masuala ya UKIMWI Pemba
ii.     Utawala na uendeshaji Unguja.

95.0        Mheshimiwa Spika, shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika programu hii ni:-
a)             Kununua vifaa, huduma na kufanya matengenezo ya majengo, vifaa na gari.
b)           Kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili kuongeza ufanisi wa kazi.
c)            Kufanya mapitio ya Muongozo wa Fedha na Uhasibu wa Tume na kutoa mafunzo ya mfumo wa kiuhasibu kwa wahusika.
d)            Kutekeleza programu ya afya kwa wafanya kazi na familia zao.

96.0        Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari wa Programu na Programu ndogo za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake Angalia Kiambatisho Nam 3.

MGAO WA FEDHA KWA PROGRAMU:

97.0        Mheshimiwa Spika, mgao wa fedha kwa Programu kumi na mbili (12) za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake ni kama ifuatavyo: -

Programu ya kwanza: Uratibu wa Shughuli za Makamu wa Pili wa Rais. Programu hii imepangiwa kutumia jumla ya Shilingi 756,466,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya pili: Uratibu wa shughuli za Serikali. Programu hii imepangiwa kutumia jumla ya Shilingi 3,028,975,000 kwa kazi za kawaida na Shilingi 8,330,450,000 kwa kazi za maendeleo (Shilingi 210,000,000 za SMZ na Shilingi 8,120,450,000 ni mchango wa Wahisani).

Programu ya tatu:  Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa. Programu hii imepangiwa kutumia jumla ya Shilingi 873,940, 000 kwa matumizi ya kawaida.

Programu ya nne: Mipango na Utawala. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 1,857,468,000 kwa kazi za kawaida na Shilingi 1,000,000,000 kwa kazi za maendeleo.

Programu ya tano: Kutunga Sheria, Kupitisha Bajeti na Kusimamia Taasisi za Serikali. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 6,542,950,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya sita: Uongozi na Utawala wa Baraza la Wawakilishi. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 10,595,550,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya saba: Uendeshaji na Usimamizi wa Shughuli za Uchaguzi. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 1,174,812,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya nane: Usimamizi wa Kazi za Utawala na Uendeshaji wa Shughuli za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 185,388,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya tisa: Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 88,813,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya kumi:  Utawala wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 351,087,000 kwa kazi za kawaida.

Programu ya kumi na moja:  Kuratibu Muitiko wa Taifa wa UKIMWI. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 222,589,000 kwa kazi za kawaida na Shilingi 519,076,000 kwa kazi na maendeleo (Shilingi 20,000,000 fedha za SMZ na 499,076,000 mchango wa Wahisani).

Programu ya kumi na mbili: Utawala na Uendeshaji wa Tume ya UKIMWI. Programu hii imepangiwa kutumia Shilingi 464,511,000 kwa kazi za kawaida.

98.0        Mheshimiwa Spika, jumla ya makisio kwa Programu zote 12 za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni Shilingi 35,992,076,000. Kiambatisho Nam. 3.

UKUSANYAJI WA MAPATO:

99.0        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imepanga kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 806,126,000 kwa mchanganuo ufuatao:-

Wakala wa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali: TShs. 793,766,000
Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa:         TShs.   12,360,000
  

HITIMISHO:

100.0      Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hayo, sasa naomba kuchukua fursa hii kumshukuru kwa dhati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, kwa kunisaidia kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa. Aidha, nawashukuru pia watendaji na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zilizo chini ya Ofisi hii wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ndugu Joseph Abdallah Meza na Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Ahmad Kassim Haji kwa juhudi zao katika kutekeleza majukumu yaliyo mbele yetu.

101.0       Mheshimiwa Spika, natoa shukurani zangu za dhati kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na shukurani maalumu kwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa mashirikiano, ushauri na maelekezo waliyotupa  katika kukamilisha bajeti. Aidha, napenda kuwashukuru sana Washirika wa Maendeleo, (Development Patners) na nchi marafiki ambazo zinaendelea kuchangia katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Ofisi yangu na ya nchi kwa jumla katika mwaka wa fedha 2015/2016. Miongoni mwao ni: Benki ya Dunia, Clinton Foundation, China, FAO, Finland, Norway, India, Japan, Marekani, Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Kifua Kikuu Malaria na UKIMWI (Global Fund), Oman, UNAIDS, USAID, UNDP, UNICEF, UNFPA, WHO, WFP na WIPO. Vile vile naishukuru sana Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Waziri MKuu kwa ushirikiano wao mkubwa na Ofisi yangu.  Pia nazishukuru Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima kwa kuendelea kuisaidia Serikali katika kutoa huduma za jamii na kuleta maendeleo katika nchi yetu. Pia nawashukuru sana wananchi wote ambao wamefuatilia na kusikiliza hotuba yangu hii.

102.0 Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa    naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 35,992,076,000 kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza Programu nilizozielezea hapo juu. Mchanganuo halisi wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:

          i.    Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais               TShs:  15,847,300,000
         ii.    Ofisi ya Baraza la Wawakilishi                  TShs:  17,138,500,000
        iii.    Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar                 TShs:    1,360,200,000
       iv.    Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na
Udhibiti wa Dawa za Kulevya                             TShs:       439,900,000
        v.    Tume ya UKIMWI Zanzibar                      TShs:    1,206,176,000
Jumla:                                                   TShs:   35,992,076,000


Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.