Habari za Punde

Uadilifu na Kazi Nzuri Ndiyo Iliyoleta Matunda na Mafanikio ya Skuli ya Msingi Kinduni Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Na Othman Khamis OMPR.
Uadilifu na kazi nzito inayoendelea kufanywa kwa pamoja kati ya Kamati ya Skuli pamoja na Walimu wa Skuli ya Msingi ya Kinduni iliyomo ndani ya Jimbo la Mahonda ndio iliyoleta mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka Minane tokea ilipoanzishwa.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Walimu na Wanafunzi wa Skuli hiyo akiiongoza Timu ya viongozi wenzake waliopewa jukumu la kuliongoza Jimbo hilo kuangalia changamoto na kupanga mikakati ya kutanzua kero zinazowakabili wanataaluma hao.

Balozi Seif alisema Kada ya Ualimu ni dhamana nzito inayohitaji uvumilivu mkubwa na kujitolea mambo ambayo yanaonekana kutekelezwa vyema na walimu na Kamati ya skuli hiyo na kuifanya skuli hiyo kufanya vizuri katika mitihani yake ya Taifa.

Alisema Walimu ndio tegemeo kubwa la Taifa kutokana na dhamana yao waliyopewa katika kuwafinyanga watoto kuwa katika maadili yanayohitajika na hatimae wawe warithi wazuri wa kuliendeleza Taifa hili katika muelekeo wa Maendeleo na Ustawi wa Wananchi wake.


Hata hivyo Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Walimu  Nchini kujiepusha na tabia ya kuwaingiza wanafuzi wao katika masuala ya Kisiasa.

Balozi Seif alisema wanafunzi  wanahitaji kujengewa msingi imara wa maisha yao ya baadaye na suala la siasa linapaswa waachiliwe wenyewe kwa vile wakati wa masomo halitawasaidia chochote zaidi ya kuanzisha fitina, majungu na kupoteza muelekeo wao wa kimasomo.

Alisema vipo vikundi vya baadhi watu vikiendelea na tabia ya kudanganya wananchi wakiwemo wanafunzi katika kuwapotosha kwa kuwambia kwamba Zanzibar bado imekumbwa na mgogoro wa Kisiasa.

Balozi Seif alisema Taifa la Tanzania kwa sasa limeshamaliza uchaguzi Mkuu wake ambapo kwa upande wa Zanzibar ina Rais Mmoja tu ambae ni Dr. Ali Mohammed Shein anayeiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Alionya kwamba vikundi vinavyopita mitaani na kudanganya Wananchi kwa kutumia vipaza sauti vielewe kwamba vinavunja sheria na kuhatarisha amani ya Taifa jambo ambalo vyombo vya dola vinapaswa na wajibu wa kuchukuwa hatua zinazofaa kisheria.

Mapema Mwalimu Mkuu wa Skuli ya msingi Kinduni Bibi Miza Omar Mohammed  amempongeza Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda wakati akiwa Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa jitihada zake zilizowezesha  Wanafunzi wote wa Skuli hiyo kusoma kwenye madeski.

Mwalimu Miza alisema skuli ya Kinduni imekuwa mfano wa kuondokana na tatizo sugu la vikalio linalozikumba skuli nyingi nchini hali iliyowapa ari wanafunzi wake kusoma kwa bidii na hatimae kupata mafanikio makubwa katika mitihani yao ya taifa ngazi ya michepuo.

Hata hivyo mwalimu mkuu huyo wa Skuli ya msingi Kinduni alisema walimu na wanafunzi wa skuli hiyo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kuwawezesha kujiandaa na mitihani yao ya taifa akivitaka kuwa ni pamoja na Kompyuta, Printa pamoja na Mashine ya Foto kopi.

Katika kuunga mkono  jitihada za walimu na wanafunzi hao Balozi Seif alikabidhi vifaa vya usafi vitakavyowasaidia wanafunzi hao katika mpango wao wa utunzaji wa mazingira ya skuli.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda na Timu yake pia alipata fursa ya kukagua maendeleo ya matengenezo makubwa ya Jengo moja la Skuli ya Msingi Mahonda lilioko katika mazingira mabovu ya kutoa huduma kwa wanafunzi.

Hivi karibuni Balozi Seif alikabidhi mifuko mia Moja ya Saruji na Fedha Taslim Shilingi Milioni 5,000,000/- za mafundi kwa ajili ya matengenezo makubwa ya jengo hilo akijitolea kushirikiana na washirika wa Maendeleo katika kutatua changamoto zinazozikabili Skuli za msingi na Sekondari za Mahonda.

Balozi Seif aliwahi kukaririwa akisema kwamba hali ya mazingira ya baadhi ya Maskuli ikiwemo majengo, vikalio na hata vifaa vya maabara na Maktaba sambamba na Walimu bora lazima iimarishwe ili kumuwezesha Mwanafunzi apate Taaluma kwa utulivu zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.