Na Mwandishi Wetu Pemba.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisiwani Pemba wameeleza kuwa
ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita umetokana na umoja na
ushirikiano kati yao na viongozi wa chama hicho sambamba na ukomavu wa kisiasa
alionao Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Maelezo hayo waliyatoa Viongozi wa chama
hicho walipokuwa wakisalimiana na Makamo
Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa nyakati tofauti kisiwani humo.
Viongozi hao walitumia fursa hiyo kutoa
pongezi kwa Dk. Shein kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu
uliopita na kusisitiza kuwa ushindi huo utaendelezwa mpaka katika uchaguzi ujao
wa mwaka 2020 kwani wanaamini kuwa hakuna tena uchaguzi katika kipindi hichi.
Katika maelezo yao viongozi hao walieleza
kuwa ukomavu wa kisiasa alianao Makamo Mwenyekiti wao Dk. Shein ndio chachu ya
mafanikio ndani ya chama chao pamoja na ushindi wake katika chaguzi zote.
Aidha, viongozi hao walimueleza Dk. Shein
kuwa yeye ndio Rais halali wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliechaguliwa
na wananchi kwa kura nyingi hivyo wataendelea kumuunga mkono katika kuhakikisha
Zanzibar inaendelea kupata maendeleo endelevu.
Pamoja na hayo, viongozi hao walitoa
pongezi kwa Dk. Shein kwa kuunda Serikali makini na kueleza imani zao kwa
viongozi aliowateua kushirikiana nao ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
huku wakieleza imani zao kuwa viongozi hao wanaweza kwenda na kasi ya Dk.
Shein.
Pia, viongozi hao walitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe
Magufuli kwa ushindi wake mkubwa pamoja na Makamu wake Mama Samia Suluhu
Hassan.
Viongozi hao walisisitiza kuwa ushindi wa
CCM na viongozi wake umewapa mwanga mkubwa wa mafanikio na utekelezaji katika
kukiimarisha chama chao kwa kuamini kuwa chama hicho ndicho kinachoweza
kusimamia maendeleo ya wananchi sambamba na amani na utulivu hapa nchini.
Viongozi hao walisisitiza kuwa Ibara ya 5
ya Katiba ya CCM, inasisitiza haja ya
chama hicho kushinda uchagazi mkuu kwa upande wa Zanzibar na Tanzania
Bara na kueleza kuwa hilo limefanyika kwa kuwepo umoja wao na mshikamano na ndio
unaowafanya waendelee kutembea kifua mbele hadi hivi leo.
Walieleza kuwa busara na hekima za Dk.
Shein ndio zinazoipelekea Zanzibar kuendelea kuwa ni nchi yenye amani, utulivu na
maendeleo huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono Dk. Shein pamoja na chama
chao cha CCM.
No comments:
Post a Comment