Habari za Punde

ESRF Yakutanisha Wanavyuoni Kuandaa Ripoti ya Maendeleo ya Binaadamu Tanzania.

MAANDALIZI ya Ripoti ya pili ya Maendeleo ya Binadamu (THDR) inayotarajiwa kuzinduliwa Juni 2017 yamefikia katika ngazi ya mwisho ya ukusanyaji wa maoni ya kitaalamu katika mada mbalimbali zinazojadiliwa katika ripoti hiyo.

Maandalizi hayo yanayowezeshwa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na wadau wengine yanafanyika kwa mfumo wa warsha ya siku mbili jijini Dar es salaam, jana Jumatatu na

Katika warsha hiyo ya rasimu ya pili na ya mwisho kabla ya uhariri, inajadiliwa na wanazuoni kupitia mada 11 ambazo zitakuwapo katika taarifa hiyo ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2017.

Warsha hiyo ya siku mbili itatoa msingi wa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu nchini kwa kuangalia Sera ya hifadhi ya jamii katika muktadha wa mabadiliko ya kiuchumi nchini Tanzania.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa jana baada ya ufunguzi wa kongamano hilo uliofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida ni usambazaji wa maji kwa kuangalia sera, fedha na upatikanaji wake; elimu; sera ya jamii na mabadiliko ya kiuchumi; na hifadhi ya jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akifungua warsha ya siku mbili iliyowakutanisha wanazuoni kuandaa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania ya mwaka 2017 jijini Dar es Salaam. (Picha na Modewjiblog)

Akifungua kongamano hilo Dkt. Kida aliwataka wadau wote kutambua kwamba kazi wanayoifanya ni ya muhimu sana kwa taifa kwani imekuwa chanzo cha upangaji wa mipango ya maendeleo na namna inavyostahili kuwa.

Alisema mpango wa pili wa maendeleo nchini kuelekea uchumi wa kati umechukua fikra na falsafa nyingi kutoka katika taarifa ya Maendeleo ya Binadamu iliyofanyiwa mwaka 2014 na kuzinduliwa mwaka 2015.

Mpango wa maendeleo wa pili wa miaka mitano uliozinduliwa wiki iliyopita umetumia vionjo vingi kutoka katika ripoti iliyopita na hivyo ni vyema wadau wakachangia mada hizo na kuzipa uhai mkubwa zaidi kwa manufaa ya Ripoti ijayo alisema Dkt. Kida.

Aidha aliwataka wahusika wote kuwa karibu na ESRF wakati wa uandishi wa mwisho ya ripoti hiyo baada ya kumalizika kwa kongamano hilo.
Mtafiti mwandamizi mshiriki na Mshauri wa kiufundi wa mradi wa THDR, Marc Wuyts akizungumzia mada ya uhusiano wa sera ya jamii na mabadiliko ya kiuchumi katika warsha hiyo ya siku mbili inayoendelea jijini Dar esSalaam.

Akizungumza uhusiano wa sera ya jamii na mabadiliko ya kiuchumi (Situating Social Policy in social economic transformation: A conceptual Framework) Mtafiti mwandamizi mshiriki na Mshauri wa kiufundi wa mradi wa THDR, Marc Wuyts alisema iko haja ya kutambua kwamba mabadiliko ya kiuchumi yatafanikiwa kwa kuongeza ufanisi na tija ya kiuchumi kabla ya kugawa manufaa yake kuimarisha huduma za kijamii.


Alisema kukosekana kwa maunganisho na kuanza kutekeleza sera za jamii na kusahau misingi ya kuinua uchumi, ndio uliokwamisha siasa za Ujamaa na kujitegemea za Rais Julius Nyerere.

Alisema ipo haja kubwa ya kutambua muunganiko na kipi kinafaa kuanza kwanza ili kufanikisha maendeleo na ustawi wa binadamu na kutahadharisha kwamba tafiti yoyote ambayo haitazingatia ukuaji wa uchumi kwanza hayatapeleka taifa hili katika uchumi wa kati.

Alisema utekelezaji wa mpango wa Mkukuta utafanikiwa ikiwa kutaangaliwa namna ya kuunganisha mpango huo na sera ya maendeleo ya kupeleka taifa katika uchumi wa kati.

Kumekuwa na dhana kwamba utekelezaji wa sera zinazonyanyua hifadhi ya jamii kunaimarisha uchumi lakini huwezi kutumia ambacho hujakizalisha.
Profesa Flora Kessy kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es salaam akizungumzia upatikanaji wa maji, usambazaji, gharama na sera zake wakati wa kujali vipengele muhimu katika taarifa ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2017 katika warsha ya siku mbili inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Mtaalamu huyo alisema kwa kufanya kitendo hicho unakuwa unakwamisha maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa umetumia ambacho hujakizalisha.

Imani kuwa elementi zilizomo katika hifadhi ya jamii zinachochea ukuaji wa uchumi, ndio kisa kilichuokwamisha siasa ya ujamaa.

Mtaalamu huyo anaamini katika mada yake kwamba ujamaa ulijali zaidi kuwaweka watu katika hali bora na kusahau kushughulika na masuala ya kiuchumi na hivyo kuikwamisha siasa hiyo.

Alisema ustawi wa jamii kama usipoangaliwa hukwamisha ukuaji wa kiuchumi.

Mtaalamu mwingine Profesa Flora Kessy kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es salaam alizungumzia upatikanaji wa maji, usambazaji, gharama na sera zake (Water Provision in Tanzania- Access Financing and Policy Trends).
Profesa wa Elimu na Menejimenti yake, kutoka Shule Kuu ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Herme Mosha akichambua kipengele cha elimu katika kuendeleza maarifa nchini wakati wa warsha hiyo ya siku mbili iliyowakutanisha wanazuoni kuandaa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania ya mwaka 2017 jijini Dar es Salaam.

Katika mada yake alisema kwamba bado kuna tatizo kubwa la utumiaji wa maji katika usafi na pia matumizi ya vyoo. Alisema japokuwa kumekuwepo na maendeleo katika matumizi ya vyoo, asilimia 11.5 hawana vyoo kabisa.

Aidha alitaja mikoa ya Mara, Arusha na Manyara kuongoza kwa kutokuwa na vyoo huku akisema wastani asilimia 7.5 hawana vyoo na Mara ikiongoza katika kundi hilo.

Mikoa yote hiyo ni ya wafugaji labda tabia zao za kuhamahama na mifugo yao zinachangia. Pia profesa huyo alisema kwamba matumizi ya maji unaweza kuona kama yapo ya kutosha kwa kuangalia suala la uoshaji mikono.

Alisema watu hawaoshi mikono kwa maji na sabuni na mkoa wa Dare s salaam unaongoza sana katika hilokwa wastani wa asilimia 21 huku maeneo mengine yakiwa katika wastani wa 7 hadi 9. Alisema upatikanaji wa maji ni muhimu katika kuonesha maendeleo ya binadamu.
Pichani juu na chini ni sehemu ya washiriki wakiwasilisha maoni yao katika warsha ya rasimu ya pili na ya mwisho kabla ya uhariri, inayojadiliwa na wanazuoni hao kupitia mada 11 ambazo zitakuwapo katika taarifa ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2017.

Naye Profesa wa Elimu na Menejimenti yake, kutoka Shule Kuu ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es salaam Herme Mosha, akichambua elimu katika kuendeleza maarifa alizungumzia tatizo la hesabu nchini na kutaka juhudi za makusudi kuchukuliwa kukabiliana nalo kwani maendeleo ya rasilimali watu katika stadi ni muhimu sana kufikia uchumi wa kati.

Alipongeza serikali kwa kuweka uwiano mzuri wa jinsia katika shule na pia ongezeko la fedha kwa ajili ya maabara na uboreshaji wa elimu nchini.

Aidha amesema kwamba maamuzi ya makusudi ya serikali kurejesha vyuo vya kufunza stadi badala ya kuwa vyuo vikuu utasaidia kuwepo kwa wataalamu wanaostahili katika kufanikisha mapinduzi ya viwanda.

Mwenyekiti wa warsha hiyo ya siku mbili Prof. Amon Mbelle akitoa mwongozo wakati wa kupitia na kufanyia maboresho rasimu ya pili na ya mwisho kabla ya uhariri wa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania ya mwaka 2017 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wanazuoni wanaoshiriki kwenye warsha ya siku mbili ya kupitia na kufanya maboresho katika Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania ya mwaka 2017 inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanazuoni wanaoshiriki kwenye warsha ya siku mbili ya kupitia na kufanya maboresho kwenye Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania ya mwaka 2017 jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.