Habari za Punde

Hotuba ya maoni ya kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo BLW



HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA FEDHA, BIASHARA NA KILIMO KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu , Mwingi wa Rehema, ambaye ametujaalia neema ya uzima na afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa ndani ya Baraza lako tukufu, tukitekeleza majukumu yetu mbali mbali ya kuwatumikia wananchi wetu. 

Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, napenda pia kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii ya kuwasilisha Maoni ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi   kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru na kuipongeza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kuweza kuwasilisha mbele ya Baraza lako tukufu Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ufanisi mkubwa katika mfumo mpya wa bajeti unaozingatia programu “Program Based Budget” (PBB).

Mheshimiwa Spika, aidha nitakuwa mkosefu wa fadhila kama sitatoa shukrani zangu za dhati kwa Wajumbe na Makatibu Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo kwa mashirikiano tuliyokuwa nayo kwa pamoja katika kutekeleza jukumu hilo kwa pamoja, pamoja na mashirikiano tuliyoyapata kwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi. Naomba niwatambue kwa kuwataja kwa majina Waheshimiwa Wajumbe hao  pamoja na Makatibu wake kama ifuatavyo:-

1.      Mhe. Yussuf Hassan Iddi                          -           Mwenyekiti
2.      Mhe. Hamida Abdalla Issa       -           Makamo Mwenyekiti
3.      Mhe. Ussi Yahya Haji                                    -           Mjumbe
4.      Mhe. Hamad Abdalla Rashid                          -           Mjumbe
5.      Mhe. Shadya Mohammed Suleiman              -           Mjumbe
6.      Mhe. Ali Salum Haji                                      -           Mjumbe
7.      Mhe. Bihindi Hamad Khamis                     
  -           Mjumbe
8.      Mhe. Moh’d Mgaza Jecha                               -           Mjumbe
9.      Ndg. Abuubakar Mahmoud Iddi                     -           Katibu
10. Ndg. Salum Khamis Rashid                             -           Katibu

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa, Wizara hii ndio uti wa mgongo kwa wananchi wa Zanzibar kwani imebeba sekta muhimu sana ambazo ni sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo wananchi wengi huzitegemea kwa ajili ya kuongeza kipato chao na kwa ajili ya mahitaji yao ya kila siku. Bado ipo haja kubwa sana kwa Serikali kupitia Wizara hii kuelekeza nguvu zake zaidi ili kuimarisha sekta hizi nchini. Hii inatokana na ukweli kwamba, tathmini inaonesha kuwa mchango wa sekta hizi katika pato la Taifa kwa mwaka 2015 umeshuka kutoka asilimia 27.9 ya mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 19.2 mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu mkubwa wa sekta hizi nchini, bado uingizwaji wa fedha katika sekta hizi ni wa wastani jambo ambalo linazorotesha utekelezaji wa mipango iliyojipangia Wizara. Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 iliyokuwa Wizara ya Kilimo na Maliasili imeidhinishiwa jumla ya Shilingi Bilioni Arobaini na Nane, Milioni Mia Moja Sabiini na Nne na Laki Tatu (48,174,300,000) hadi kufikia mwezi wa Aprili, 2016 Wizara imepata jumla ya Shilingi Bilioni Tisa, Milioni Mia Moja Themanini na Tano na Laki Tano Elfu Arubaini na Moja, Mia Saba na Hamsini (9,185,541,750) sawa na asilimia 69.6. na kwa upande wa fedha za maendeleo Wizara ilikadiriwa kutumia jumla ya TZS Bilioni Thelathini na Nne, Milioni Mia Tisa themanini na tatu na laki mbili (34,983,200,000/-) hadi kufikia aprili, 2016 fedha zilizopatikana ni TZS 11,641,070,476.

Mheshimiwa Spika, kwa iliyokuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeidhinishiwa jumla ya TZS Bilioni Nne,Milioni Mia Mbili na Elfu Kumi na Saba na Laki Nne (4,217,400,000) ambapo hadi kufikia mwezi wa aprili, 2016 Wizara imepata jumla ya TZS Bilioni Mbili, Milioni Mia Nne Tisiini na Nane, Laki Sita na Elfu Ishirini na tano, Mia Nne na thelathini na Sita (2,498,625,436) sawa na asilimia 59. Na kwa upande wa fedha za maendeleo Wizara ilikadiriwa kutumia jumla ya TZS 12,910,100,000 hadi kufikia Aprili fedha zilizopatikana ni TZS Bilioni Mbili, Milioni Mia Tatu Tisiini na Moja, Laki Mbili Arubaini Mbili Elfu, Mia Saba Sitini na Nne (2,391,242,764) sawa na asilimia 19.

Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya Serikali kuimarisha sekta hizi juhudu za ziada zinahitajika khasa kuipatia Wizara hii fedha kwa wakati, ili wazisimamie sekta hizi kwa lengo la kuziimarisha kwa maslahi ya wananchi na kupunguza malalamiko kwa wadau wa sekta hizi nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni moja kati ya Wizara ambazo zinategemewa kukusanya mapato kupitia sekta zake inazozisimamia, katika mwaka mwaka wa fedha 2015/2016 Wizara ilikadiriwa kukusanya mapato ya TZS Bilioni Moja, Milioni Mia Tisa na Ishirini na Mbili, Laki Saba na Hamsini na Tano (922,755,000)hadi kufikia Aprili,2016 Wizara kwa ujumla imekusanya mapato ya TZS Bilioni Moja,Milioni Mia Nane na Thamanini, Laki Saba na Tisini, Mia Nane Thelasini na Sita(1,680,790,836) sawa na asilimia 87.4 ya malengo ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Wizara katika ukusanyaji wa mapato, Kamati yangu haijaridhishwa na asilimia ya ukusanyaji iliyofikiwa na Wizara. Kwahivyo, Kamati inaitaka Wizara kuangalia upya vianzio vyake vya mapato na kufanya tathmini katika suala zima la uvujaji wa mapato ili kuhakikisha miyanya yote inayopelekea kuvuja kwa mapato ya Wizara hii inazibwa na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayehusika na eidha kukwepa kodi au kusababisha kuvuja kwa mapato ya Wizara.  

Mheshimiwa Spika, Wizara imetoa takwimu kadhaa katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kutoa mwelekeo wa sekta hizi kujifahamu wapi tulipotoka, wapi tulipo na wapi tunaelekea katika sekta hizi. Ni dhahiri kuwa takwimu za mifugo na uvuvi zinazotolewa na Wizara bado zinatolewa kienyeji sana kwani maeneo mengi yanayohusika na mifugo na uvuvi hayafikiwi na hivyo kupelekea takwimu zinatolewa ni za kubahatisha na sio sahihi. Kamati yangu inaitaka Wizara kuangalia upya vyanzo vya takwimu zinazotolewa na Wizara ili takwimu zinazotolewa zionekane kuwa vipo vianzio vya upatikanaji wa takwimu sahihi katika sehemu zinazohusika.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaipongeza sana Wizara kwa kuliangalia suala la bei ya mwani kwa jinsi wakulima wa zao hili wanavyopata tabu juu ya kilimo hiki ukilinganisha na bei ya zao lenyewe. Jitahada za Wizara kutaka kuandaa utaratibu maalum wa ununuzi wa zao la mwani kupitia Shirika la Biashara la taifa la Zanzibar (ZSTC) kwa lengo la kuwahakikishia soko la uhakika la zao hili linaungwa mkono na Kamati yangu kwani litaondoa kabisa tatizo la bei ya mwani kwa wakulima na kuwapatia soko la uhakika. Kamati inaiomba sana serikali iharakishe suala hili ili kupunguza kilio kwa wakulima wa zao la mwani.

Mheshimiwa Spika, Kamati pia imeridhika kwa jitihada za uanzishaji wa vikundi 144 vya wafugaji wa samaki, lakini Kamati inaishauri Wizara isiishie kwenye uanzishaji tu lakini pia iwe na ufuatiliaji juu ya maendeleo ya vikundi hivyo ili kujuwa mafanikio yao na changamoto zao. Kwani katika utendaji wetu jitihada zinaonekana sana kwenye uanzishaji wa mambo mbali mbali ya kimaendeleo katika jamii lakini hakuna ufuatiliaji, jambo ambalo hupelekea kutokuendelea kwa yale yanayoanzishwa. Na hivyo kurudisha nyuma jitihada za Serikali na jitihada za wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini, Kamati yangu pia inaipongeza sana Wizara kwa ununuzi wa mbolea na dawa za kuulia magugu, lakini bado Kamati inasikitishwa sana na utaratibu wa ugawaji wa mbolea na dawa pamoja na zinavyotumiwa. Aidha, Wizara ni vyema kufanya utafiti zaidi ili kuelewa mahitaji ya mbolea kwa wakulima wetu kwani ni dhahiri kuwa mbolea inayotolewa haitoshi na hivyo kusababisha malalamiko kwa wakulima wetu na kurudisha nyuma sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu ililijadili kwa kina suala la ununuzi wa matrekta na matumizi yake kwa wakulima, kwa mujibu wa tathmini ya Wizara ili kukidhi mahitaji ya wakulima yanahitajika matrekta 80, lakini sasa hivi yapo matrekta 48 (Unguja 29 na Pemba 19). Lakini kati ya matrekta hayo si chini ya matrekta 10 hayafanyi kazi na yanahitaji matengenezo. Kamati inaendelea kuishauri Wizara iwe makini sana na iwatumie wataalamu wake kabla ya ununuzi wa matrekta ili yatumike kwa muda mrefu na kuipunguzia gharama Serikali.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu pia ilijadili sana suala la uendelezwaji wa mashamba ya mipira, ni dhahiri kuwa mashamba haya yanaingizia mapato makubwa katika Serikali na kwa sasa hivi mashamba haya yamekodishwa kwa watu binafsi, lakini hayashughulikiwi ipasavyo jambo ambalo linapelekea miti mingi inakufa, mashamba yanavamiwa lakini pia hayaendelezwi kwa kupandwa miti mipya. Kamati inaitakwa Wizara kuliangalia vizuri suala hili na kama aliyekodishwa hayaendelezi basi mashamba haya yarudi kwenye mikono ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Kamati imefurahishwa kwa kupewa taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha usarifu wa mazao, lakini Kamati imesikitishwa sana na udanganyifu uliofanywa wa kutokukamilika kwa kufungwa kwa mashine na vifaa vya ujenzi huo na hatimae kushindwa kukamilika kama ilivyokusudiwa. Tunaomba sana hatua za kisheria zichukuliwe kwa yeyote aliyehusika na udanganyifu huo.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaipongeza sana Wizara kwa ujenzi wa Barabara za mashamba kilomita 148.5 kwa Unguja na Pemba chini ya mradi wa MIVARF kwa kiwango cha fusi, hata hivyo, Kamati inaishauri Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano kuzikamilisha barabara hizi kwa kiwango cha lami kwani kubakia kama zilivyo zitaharibika na hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuitia gharama kubwa Serikali ya kuzijenga tena upya barabara hizo au kuzifanyia ukarabati.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilifurahishwa sana baada ya kupata taarifa kuwa yapo mabonde mengi ya mpunga hapa Zanzibar ambapo kama yatalimwa mpunga yote basi yatakidhi mahitaji ya chakula kwa asilimia 80% kwa wananchi wa Zanzibar, Kamati yangu inaendelea kuitaka Serikali kuongeza juhudi katika kilimo ili tupunguze kununua vyakula kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaipongeza Wizara kwa kuotesha miche ya mikarafuu 347,650 kwa Unguja na Pemba kwa lengo la kuimarisha kilimo na zao la karafuu nchini. Lakini Kamati inaiomba sana Wizara baada ya kugawa miche kuwe na ufuatiliaji ili kufahamu ni miche mingapi ilipandwa na mingapi imeshika na mingapi imekufa ili isijekuwa tathmini yetu inakuwa kubwa katika kuotesha miche lakini karafuu zinazovunwa hazionekanwi kuongezeka, hapo itakuwa hatujafanya kitu.

Mheshimiwa Spika, tuna tatizo la bandari bubu ambazo kwa kiasi kikubwa sana linaathiri kupungua kwa mapato ya nchi lakini pia linaathiri katika sekta mbali mbali zikiwemo kilimo na mifugo kwasabubu wanyama na mbegu za mimea huingizwa kiholela na hatimae kupelekea kutokea kwa maradhi ya mimea na mifugo. Kamati yangu inaitaka Serikali kwa kushirikiana na vikosi vyake vya SMZ kukomesha moja kwa moja tatizo hili ili kuokoa mapato ya nchi na madhara yote yanayotokana na tatizo hili. Lakini pia mashirikiano baina ya wananchi na Serikali yanahitajika ili kukomesha tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, tatizo la matumizi ya msumeno wa moto bado lipo Zanzibar na linaendelea kuathiri sana miti katika maeneo tofauti ya Zanzibar, pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Wizara kukomesha matumizi ya msumeno wa moto lakini bado jitihada za ziada zinahitajika kwa wananchi kutoa mashirikiano kwa vyombo na taasisi husika ili kuinusuru miti yetu na hatimaye nchi yetu isijekuwa jangwa.

Mheshimiwa Spika, uvuvi haramu ni tatizo jengine lipo katika visiwa vyetu ambalo kwanza hupoteza mapato ya nchi na kuharibu mazalia ya samaki na hivyo kusababisha madhara makubwa katika sekta ya uvuvi nchini. Tunaiomba Serikali na tunaamini kuwa inaweza kukomesha moja kwa moja jambo hili ili tuokoe mapato yetu na kuweka matumizi mazuri ya rasilimali yetu ya bahari.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaipongeza sana Serikali pamoja na Wizara hii kwa kufikia pahala pazuri katika ujenzi wa soko la Malindi ambapo mwanzo lilishindwa kuanza kujengwa kwasababu michoro ya awali kutoendana na majengo ya Mji Mkongwe ambao upo kwenye urithi wa dunia.Tunaimani kuwa kwakuwa hatua zote zimeshakamilika ujenzi huu utaanza muda wowote kuanzia sahivi ili kuimarisha sekta ya uvuvi nchini.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imezungumzia mambo mengi sana na hayo ni machache tu kati ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati yangu naamini yapo mengi Waheshimiwa Wajumbe watayazungumza, kwahivyo sasa baada ya mchango huo wa jumla naomba kwa ruhusa yako niende kwenye Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa Wazara hii ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Kamati yangu ilipitishia Bajeti ya Wizara hii pamoja na marekebisho ambapo marekebisho haya yalipendekezwa na Wizara kwa kuongeza fedha katika baadhi ya vifungu ambavyo vilisahaulika.
Marekebisho haya yamebadilisha jumla ya fedha katika matumizi ambapo kabla ya marekebisho ilikuwa ni TZS Bilioni Arobani Nane, Milioni Mia Tisa Arobani na Mbili, Laki Tatu (48,942,300,000) na baada ya marekebisho ni TZS Bilioni Arobani Nane, Milioni Mia Tisa Sabini na Saba, Laki Tatu (48,977,300,000). Vifungu ambavyo vimefanyiwa marekebisho ni hivi vifuatavyo:-
Kifungu L0105
Kabla ya Marekebisho
Baada ya Marekebisho
Program Kuu ya Mipango na usimamizi wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
19,481,687,000
19,516,647,000

Kifungu L010502


Program Kuu ya Mipango, Sera na Utafiti wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
14,765,449,000
14,800,449,000

Kifungu L01050205

Mradi wa Kuimarisha         1,873,964,000
Miundombinu ya masoko
ya mazao ya Kilimo                                         
1,908,964,000

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 Wizara inakadiria kukusanya TZS 2,817,599,000/. Ni imani yetu kuwa makusanyo haya yatakusanywa zaidi endapo kutakuwa na mikakati mizuri katika kukusanya wa  mapato na udhibiti wa uvujaji wa mapato. Tunaiomba sana Wizara katika kuhakikisha kuwa tufanikisha malengo tuliyojipangia kwanza tusiwe na muhali katika suala la ukusanyaji wa mapato nahatua kali zichukuliwe kwa yeyote atakaye kwepa kulipa kodi au atakae sababisha kuvuja kwa mapato, na hilo tunaomba sana lizingatiwe katika maeneo yote ya ukusanyaji kodi. Lakini pia Kamati inaendelea kuishauri Wizara isiridhike na vianzio tulivyonavyo itumie wataalamu wake kubuni vyanzo vipya vya mapato na jambo hili tunaamini linawezekana.

Mheshimiwa Spika, katika Kifungu L0105 jumla ya TZS 28,641,000 zimetengwa kwa ajili ya Kusimamia mapato na matumizi ya Wizara. Kwakuwa zipo fedha maalumu ambazo zimetengwa kwa ajili ya kusimamia mapato, tunaamini kuwa suala la uvujaji wa mapato katika Wizara hii halitakuwepo.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaitaka Wizara kuyasimamia mapato ya Wizara hii kwa nguvu zake zote lakini maeneo yafuatayo yanahitaji usimamizi zaidi kwani ni maeneo ambayo yanafanyiwa udanganyifu sana na kusababisha kuvuja kwa mapato, maeneo yenyewe ni haya yafuatayo:
Ø  Ada za uuzaji wa mawe,mchanga na kokoto
Ø  Leseni za uvuvi
Ø  Mapato ya mashamba
Ø  Ada ya uingizaji wa wageni
Ø  Mapato ya mifugo
Ø  Mapato ya uvuvi wa bahari kuu

Mheshimiwa Spika, kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Waziri kuwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ambayo Fungu lake ni L01 inazo Programu Kuu 5 na Programu ndogo 13. Katika utekelezaji wa Programu hizo tano Wizara imepanga kutumia jumla ya TZS  48,977,300,000 kwa mwaka 2016/2017 kati ya fedha hizo TZS 15,743,300,000/ kwa ajili ya kazi za kawaida na 33,234,000,000/ kwa ajili ya kazi za Maendeleo ambapo katika fedha hizi za maendeleo TZS 1,068,000,000/ kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na 32,168,000,000/ kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Programu Kuu ya Maendeleo ya Kilimo

Mheshimiwa Spika, katika kifungu L0101 Programu Kuu ya Maendeleo ya Kilimo ambayo imetengewa jumla ya TZS 6,615,744,000, ndani yake zimetengwa TZS 3,382,472 kwa ajili ya Maendeleo ya Huduma za Kilimo na Karakana ya Matrekta. Naomba sana fedha hizi ziingizwe kwa wakati ili kuboresha na kuimarisha kilimo na kuindeleza karakana yetu ya matrekta na kuacha kutengeza vyombo vya Seriklai kwa watu binafsi. Suala hili la kutengeneza vyombo vya Serikali kwa watu binafsi siku hizi limekuwa ni la kawaida sana wakati Serikali inayo maeneo yake maalum ya kutengeneza vyombo vyake, tunaomba sana karakana ya Serikali iwezeshwe kwa kupewa vifaa vya kutosha ili tuzilinde fedha zinazotumika kwa ajili ya kutengeneza vyombo nje ya karakani zetu.

Mheshimiwa Spika, aidha katika Programu hii jumla ya TZS 1,068,660,000 zimetengwa kwa ajili ya umwagiliaji maji. Wakati Kamati ikijadili suali hili ilielezwa kuwa, Wizara inadaiwa takriban TZS 600,000,000/- na Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) kwa gharama za umeme, na umeme mwingi unatumika kwa ajili ya umwagiliaji maji. Kamati yangu inaishauri Wizara iangalie njia mbadala ya matumizi ya umeme wa jua (solar power) ili kupunguza gharama za matumizi ya umeme katika shughuli hii ya umwagiliaji maji na kuwapunguzia gharama wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika Programu hii jumla ya TZS 344,454,000 zimetengwa kwa ajili ya Uhakika wa Chakula na Lishe. Kamati yangu inaiomba sana Serikali kuhakikisha fedha hizo zinapatika kwa wakati ili ghala yetu tuliyonayo iweze kutumika kwa kuhifadhia chakula hicho na kupunguza usumbufu kwa wananchi ikitokea kuadimika kwa chakula nchini.

Mheshimiwa Spika, katika Programu hii vile vile jumla ya TZS 1,425,000,000 zimetengwa kwa ajili ya Kuimarisha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo. Kamati yangu inaiomba sana Serikali kuingiza fedha hizi mara tu baada ya kupitisha bajeti hii, kwani kuna wakulima ambao wanaidai fedha kwa Wizara  hii ambazo walikopeshwa mbegu na wakulima. Deni hili ni la muda mrefu na kutokuwalipa wakulima fedha zao tutakuwa tuna wavunja moyo sana wakulima wetu na hivyo kurudisha nyuma sekta ya Kilimo. Kamati yangu haitaridhia endapo madeni haya itafika bajeti ya mwakani hayajalipwa kwa wakulima wanaoidai Wizara. Wanaodai fedha hizo wameshalalamika mpaka kwenye vyombo vya habari kuonesha hisia zao.

Programu Kuu ya Maendeleo ya Rasilimali za misitu na Maliasili zisizorejesheka

Mheshimiwa Spika, katika kifungu L0102 Programu Kuu ya Maendeleo ya Rasilimali za Misitu na Maliasili Zisizorejesheka jumla ya TZS 1,667,436,000 zimetengwa. Dhumuni la Programu ni kuhifadhi na kuendeleza misitu, kupitia Programu hii tunaiomba sana Wizara ihakikishe kuwa misitu inahifadhiwa na kuendelezwa ili iwe ni kivutio kikubwa cha watalii wanaotembelea katika misitu hiyo, na iweze kuingiza mapato zaidi katika nchi. Lakini pia pamoja nakuihafadhi na kuilinda misitu yetu, Kamati inaitaka Wizara pia iitangaze misitu yetu ndani na nje ya nchi ili tupate wageni wengi wanaotembelea katika misitu yetu. Kwa maana kwamba isiishie kwenye kuhifadhi na kuendeleza lakini iitangaze pia ili ijulikane ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, katika programu hii kiasi cha TZS 1,570,725,000 zimetengwa kwa ajili ya Uhifadhi na Kusimamia  Misitu na Mashamba ya Serikali. Kamati yangu wakati inajadili Programu hii  ilitaka kujua kuhusu uwepo wa hati miliki kwa mashamba ya Seriklai kama ni njia moja ya kuhifadhi na kusimamia mashamba hayo, Kamati ilielezwa kuwa Serikali inayo jumla ya mashamba 52, kati ya hayo mashamba 12 yameshapatiwa hati miliki na mashamba 40 bado hayajapatiwa. Kamati inaitaka Serikali kwa kushirikiana na Wizara ilifuatilie suala hili la upatikanaji wa hati miliki ya mashamba ya Serikali yaliyobaki kwani uvamizi wa mashamba haya unaendelea siku hadi siku.

Programu Kuu ya Maendeleo ya Mifugo

Mheshimiwa Spika, katika kifungu L0103 Programu Kuu ya Maendeleo ya Mifugo jumla ya TZS 1,760,746,000 zimetengwa. Fedha hizi zimetengwa kwa ajili uzalisahji wa mifugo na huduma za utabibu wa mifugo.

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze kuwa Wizara hii kupitia Idara ya Mifugo ina mifugo 95 kati ya hiyo 75 ni ng’ombe ambao kati ya hao shamba la Pangeni lina ng’ombe 44 na Chamanangwe 31 na Kitumba mbuzi 20. Kwakuwa, Wizara kupitia Idara hii ambayo ndio tegemeo kwa wafugaji tulitarajia tuone idadi kubwa ya mifugo ili iweze kuwasaidia wafugaji wengine, lakini Kamati yangu inasikitishwa sana kuona kuwa katika mashamba haya wapo wafanyakazi wa Serikali ambao wanalipwa mishahara na Serikali kushughulikia mashamba hayo lakini idadi ya mifugo iliyopo hairidhishi. Tunaomba Serikali kupitia Wizara ya fedha iipatie idara hii fedha ili idadi ya mifugo iongezeke na  izalishe mifugo kwa wingi na hatimae kuweza kuwasaidia wafugaji.

 Mheshimiwa Spika, Katika Programu hii jumla ya TZS 106,540,000 zimetengwa kwa ajili ya Kudhibiti Maradhi ya Mifugo. Maradhi ya mifugo yapo na yanaathiri sana sekta hii ya mifugo kwa wafugaji wote walioko Unguja na Pemba. Tunaamini fedha hizi zitapatikana ili kudhibiti moja kwa moja maradhi ya mifugo. Lakini Kamati yangu imesikitishwa sana baada ya kuona kuwa katika Idara hii ya mifugo kwa upande wa Unguja wapo madaktari 10 na kwa Pemba yupo (1) mmoja tu. Tunaomba sana Wizara iliangalie sana suala hili kwani wataalamu wanahitajika kwa wingi kwa pande zote mbili ili kuinusuru mifugo yetu na maradhi.

Programu Kuu ya Maendeleo ya Uvuvi

Mheshimiwa Spika, katika L0104 Programu Kuu ya Maendeleo ya Uvuvi jumla ya TZS 19,416,727,000 zimetengwa. Fedha hizi zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha ufugaji wa mazao ya baharini na Maendeleo ya uvuvi na hifadhi za baharini, katika fedha hizo jumla ya TZS 15,045,000 kwa ajili ya Kuimarisha Kilimo cha Mwani lakini pia TZS 2,297,000 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha Usarifu na Uongezaji Thamani wa Zao la Mwani. Tunaimani kuwa fedha hizi zitaingizwa kwa wakati ili kupunguza kilio kwa wakulima wa mwani na ni matarajio yetu kuwa uzalisaji wa mwani utaongezeka zaidi endapo fedha hizi zitapatikana.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika Program hii jumla ya TZS 9,000,000 zimetengwa kwa ajili ya Kusimamia Mali za Wizara na Manunuzi kwa Mujibu wa Sheria. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Wizara hii ni Wizara pekee ambayo inazo mali nyingi sana za Serikali hasa vyombo vya moto kama vile magari, pikipiki, matrekta nakadhalika ambavyo vinahitaji kusimamiwa vizuri ili vitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa na Serikali. Kamati yangu inapata mashaka sana juu ya fedha hizi zilizotengwa kwa ajili ya usimamizi wa mali za Wizara ukilinganisha na idadi ya vyombo vilivyomo ndani ya Wizara hii. Pamoja na ufinyu wa fedha hizo Kamati yangu inaitaka Wizara kuhakikisha kuwa mali za Wizara zinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio vyenginevyo.

Mheshimiwa Spika, Aidha, katika Programu hii jumla ya TZS 14,970,993,000 zimetengwa kwa ajili ya Kuimarisha Uvuvi wa Bahari Kuu. Mheshimiwa Spika suala hili la uvuvi wa bahari kuu limekuwa likizungumzwa sana katika Baraza lako tukufu, tunaomba sana Serikali iharakishe kuanzishwa kwa uvuvi wa bahari kuu kwani rasilimali yetu kubwa visiwani ni bahari. Kamati yangu pamoja na Wajumbe wa Baraza lako tukufu tunaamini kuwa kuanzishwa uvuvi huu kutaimarisha uchumi wa Zanzibar kwani kutaingiza mapato mengi katika nchi na kutaongeza ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya rasilimali ya bahari katika kisiwa chetu bado ni madogo sana hususan katika suala la uvuvi, kwani bado tunatumia uvuvi wa kienyeji, jambo hili limepelekea sasa hivi katika visiwa vyetu tunaagiza samaki kutoka nje jambo ambalo ni la kusikitisha sana, takwimu za upatikanaji wa samaki kwa Zanzibar kwa mwaka 2015 ni tani 34,104 wakati nchi kama China inavua samaki tani 49,467,463; Peru inavua samaki tani 9,416,285 na India 6,318,639 na zipo nchi nyigi ambazo zinavua samaki wengi sana na zimeendelea kupitia sekta hii ya uvuvi.

Tunaiomba sana Serikali suala hili sasa sio la kuzungumzwa tena bali ni la kuanza kufanyiwa kazi kwani tumeshuhudia kuwa zipo nchi nyingi ambazo zimeendelea kwa matumizi mazuri ya rasilimali ya bahari na sisi tuwe ni miongoni mwa nchi hizo.

Tunaishauri Serikali itafute wawekezaji wa ndani au nje katika suala hili la uvuvi wa bahari kuu ili rasilimali yetu ya bahari itumike kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar na kuinua uchumi wetu. Tunaomba sana katika Wizara hii kipaombele cha Wizara katika bajeti ya mwaka huu iwe ni kuanzishwa kwa uvuvi wa bahari kuu.

Programu Kuu ya Mipango na Usimamizi wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi

Mheshimiwa Spika, katika kifungu L0105 Programu Kuu ya Mipango na Usimamizi wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi jumla ya TZS 19,481,647,000 zimetengwa, ambapo ndani yake zipo programu ndogo za utawala na uendeshaji wa kazi za kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi. Katika Programu hii jumla ya TZS 352,830,000 zimetengwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kitaaluma wafanyakazi. Mheshimiwa Spika, katika kifungu hiki Kamati yangu ilichukuwa muda mrefu kujadiliana na Wizara ili kupatiwa maelezo ya fedha hizo kuzielekeza kwenye kusomesha wafanyakazi badala ya kuimarisha kwenye kilimo chenyewe. Tatizo lilipo ni kuwa, Zanzibar tunayo Bodi yetu ya Mikopo kwanini wafanyakazi hawa wasisomeshwe na Bodi ya Mikopo ili kuokoa fedha hizo kwenda kwenye kilimo, na kwakuwa wanaosomeshwa ni wafanyakazi ingekuwa rahisi fedha hizo kurudishwa ili wasomeshwe watu wengine.

Mheshimiwa Spika, Kamati imeelezwa kuwa wafanyakazi wengi ambao wanasomeshwa na Wizara wana umri zaidi ya miaka 35 ambapo moja ya vigezo vya kupata mkopo mtu awe na umri usiopungua miaka 35. Kwa msingi huo, Kamati yangu inashauri kuwa Wizara ya Elimu kupitia Bodi ya Mikopo sasa iangalie uwezekano wa kusomesha  wafanyakazi ambapo faida mbili zitapatikana; kwanza fedha zitakazotumika kwa ajili kuwafundisha zitakuwa na uhakika wa kuwarudishwa na la pili tutaokoa fedha nyingi katika mawizara ambazo zinatumika kuwasomesha wafanyakazi, jambo ambalo baadhi yao wakishakusomeshwa huwa wanahama kwenye zile taasisi na hivyo malengo yaliyokusudiwa kutokufikiwa.

Mheshimiwa Spika, katika Programu hii jumla ya TZS 8,044,968,000 zimetengwa kwa ajili ya Kuimarisha uzalishaji wa mpunga. Kamati yangu inaipongeza sana Wizara kwa kutenga fedha maalum kwa ajili ya kuzalishaji mpunga, na kama tunavyofahamu kuwa chakula kikuu kwa wananchi wa Zanzibar ni wali ambao unatokana na mpunga. Kamati yangu inaiomba sana Serikali iipatie Wizara fedha hizo huku ikizingatia kuwa mabonde yetu tuliyonayo yatumike ipasavyo na kwa utaalamu ili tuzalishe mpunga kwa wingi na tupunguze kuagiza mchele kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe angalizo kwa Serikali kuwa katika miradi ya maendeleo iliyomo ndani ya Wizara hii ambapo jumla ya TZS 33,234,000,000/ zimetengwa kwa ajili ya kazi za Maendeleo, katika fedha hizi za maendeleo TZS 1,068,000,000/ kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na 32,168,000,000/ kutoka kwa washirika wa maendeleo. Katika sekta hii muhimu fedha nyingi tumeziweka kwa washirika wa maendeleo ambazo upatikanaji wake sio wa uhakika, kwa maana kuwa zikikosekana hizo fedha miradi hii haitafanyika na kutokufanyika kwa miradi hii tutakuwa tunazirudisha nyuma sana sekta hizi. Kwahiyo, kuna haja kwa Serikali kuingalia miradi hii kwa jicho jengine ili tuhakikishe kuwa miradi inatekelezwa hata kama fedha hizi hazikupatikana kutoka kwa washirika wa maendeleo.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo imeyakubali  mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo,Maliasili, Mifugo na Uvuvi  kwa mwaka wa fedha 2016/2017, na inawaomba Waheshimiwa Wajumbe wako wote waijadili, watoe  mapendekezo yao na hatimae kuipitisha Bajeti hii muhimu. Pia Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu kwa kunisikiliza kwa makini na utulivu wa hali ya juu wakati wote nilipokuwa nikiwasilisha hotuba hii.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
………………………….
Mhe. Yussuf Hassan Iddi,
Mwenyekiti,
Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo,
Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.