Na Haji Nassor, Pemba
WATU watatu wa familia moja, akiwemo
mtoto mchanga wa mwaka mmoja na miezi miwili, wamenusurika kupoteza maisha,
baada ya nyumba wanayoishi, kuwaka moto katika kijiji cha Nanguji shehia ya
Kendwa wilaya ya Mkoani Pemba.
Moto
huo uliotokea majira ya saa 7:00 usiku, wakati familia hiyo ikiwa imelala,
ndipo ghafla mama wa familia hiyo Bimkubwa Salim Rashid (23), alipoona mwangaza
na kisha kumuamsha mume wake.
Alisema
hatua ya kumuamsha mume wake, na kisha kupiga kelele, ndio iliosababisha ndugu,
jamaa, marafiki na majirani wa kijiji hicho, kuamka na kuanza kuuzima moto kwa
kutumia maji.
Alieleza
kuwa, ingawa hakukuwa na mtu aliejeruhiwa kwenye tukio hilo, lakini vipo baadhi
ya vitu vyao vya ndani viliunga ikiwa ni pamoja godoro na kitanda walichokuwa
wamelalia.
“Moto
haukuwa mdogo, si unajua nyumba za makuti ikishika moto, lakini majirani
wamekuja usiku huo huo, na kutusaidia kuzima, na twawashukuru sana’’,alifafanua.
Nae
baba wa familia hiyo Issa Shehe Othaman, alieleza kuwa hajui asababu ya moto
huo, kwa vile taa ya kibatali ambayo ilikuwa inawaka, haikuripuka wala kupinduka
kama ishara ya chanzo.
Issa
alieleza kuwa, wapo baadhi ya majirani na watu wengine wa karibu, waliidai kusiki
harufu ya mafuta ya petrol, nusu saa kabla ya kutokea tukio hilo.
“Majirani
waliokuwa wakitusaidia kuzima moto, walisema walisikia harufu kali ya mafuta,
na kisha ndio wakaona mwangaza mkali wa moto, uliounguza nyumba
yangu’’,alifafanua.
Mapema
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, alifika kwenye eneo hilo, na
kuitaka familia hiyo kuwa na moyo wa subra, na serikali itakikisha kama kuna
yeyote aliehusika atasakwa.
Hemed
alifafanua kuwa, sasa serikali imeshachoshwa na vitendo vya kihalifu vinavyoendelea
kutokea, na iko tayari kufanya kila njia, ili kuhakikisha wahusika wanafikishwa
mbele ya vyombo vya sheria.
“Sisi
kama serikali tunaalani vikali matendo haya, na kwa kweli lazima tutumie nguvu
kubwa, ili kuhakikisha kama kuna yeyote, basi apatikane, ingawa hatoonewa mtu
katika hili’’,alifafanua.
Nae
shuhuda aliesaidia kuzima moto huo, Salim Mbarouk Salim alisema baada ya
kusikia kelele alitoka nje, na kuona moshi na kusikia moto…moto na kufika
kusaidia kuzima.
“Mimi
usingizini nilisikia kelele zikinadi juu ya moto, kutoka nje..naam moto
unawaka, nikachukua maji na ngazi kupanda juu kuzima’’,alifafanua.
Sheha
wa shehia Kendwa Sabiha Mohamed Ali, alisema na yeye alifika usiku huo huo, na
kushirikiana na wananchi wake, kuzima moto huo, huku akiitaka familia hiyo kuwa
na moyo wa subra.
Tukio
la kuungua moto nyumba hiyo, ambayo ni miongoni mwa nyumba 78 zilizowahi kutiwa
alama ya X na watu wasiofahamika mwezi Febuari mwaka huu, inalifanya kuwa tukio
la tatu, baada ya juzi migomba 129 na mikarafuu tisa kukatwa katwa.
No comments:
Post a Comment