Habari za Punde

Serikali kuwazuilia leseni watakaopandisha bei za bidhaa

TAKDIR  ALI NA MIZA OTHMAN     HABARI MAELEZO.              
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itawazuilia leseni wafanyabiashara watakaobainika kuwanyima huduma  ama kuwapandishia bei baadhi ya wananchi kutokana na  misingi ya kisiasa.

Akijibu suali la  Mwakilishi wa viti maalum Viwe Khamisi Abdallah, katika Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar alietaka kujua  iwapo Serikali inafahamu suala la hilo, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali alisema Serikali inalifahamu suala hilo na tayari linafanyiwa kazi na wakuu wa wilaya.

Balozi Amina alisema katika kisiwa cha Pemba kumekuwa na uchafuzi wa kisiasa na baadhi ya wanasiasa wanatumia nafasi hiyo kuwapandishia bei wananchi hususan wanachama wa CCM.

Alisema wamekuwa  wakichukua hatua ya  kuwafungia kwa muda mfupi wafanyabiashara  wenye tabia hiyo  lakini hivi sasa watawazuilia leseni kwa muda wa mwaka mmoja kama  adhabu na onyo.

Mapema akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Fuoni Yussuf Hassan Iddi, Balozi Amina alisema Seriksali inafanya juhudi kubwa za kusimamia  bei za bidhaa muhimu  ikiwemo,mchele,Unga wa ngano,na sukari ili kuhakikisha hakuna upandaji wa bei kiholela.


Alikiri  kuwa baadhi ya bidhaa hizo zimepanda  bei kidogo kutokana na kupanda mara kwa mara kwa thamani ya Dola na kuongezeka kwa gharama nyengine za biashara zikiwemo  kuchelewa kushusha mizigo bandarini.

Alisema Serikali imefanya juhudi kubwa  kupunguza tatizo la upandaji wa bidhaa,  ikiwemo  kufanya mazungumzo na Shirika la Bandari pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (ZNCCIA) ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Aliongeza  kuwa Wizara yake inaendelea na juhudi  ya kuhahikisha bidhaa muhimu za chakula kwa ajili ya mwezi mtukufu Ramadhani ikiwemo unga wa ngano,Tende na Sukari  vinapatikana kwa bei nafuu ili kuwapunguiza mzigo wananchi ndani ya mwezi huu.         

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.