Habari za Punde

Wasomesheni watoto wa kike kuondoa changamoto hospitali

 Na Haji Nassor, Pemba
WITO umetolewa kwa jamii, kubuni njia na mikakati mbali mbali ya kumsomesha mtoto wa kike, ili changamoto iliopo ya akinamama kupewa huduma za isiri hospitalini na akinababa iondoke.
Wito huo umetolewa na Naibu Mwenyekiti wa mahakama ya ardhi Chakechake Pemba, Salim Hassan Bakari alipokua akijibu hoja za wananchi wa shehia ya Mgagadu Jimbo la Chambani wilaya ya Mkoani, wakati Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba kikitoa masaada wa kisheria bila ya malipo.
Alisema kimsingi na kimaadili, akinamama wanaofika hospitali walipaswa kupewa huduma na wanawake wenzao, na sio wanaume kama ilivyo sasa, lakini hilo lipo kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa kutosha wa kike.
Alisema changamoto hiyo haipo Zanzibar pekee, bali kila nchi hujichomoza kutokana na watoto wa kike waliowengi kukatishiwa masomo kwa kuolewa mapema.
Naibu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, wakuliondoa hilo ni jamii kujipangia mikakati katika familia zao kuwasomesha watoto hasa wa kike, na kuacha tabia ya kuwaozesha waume kabla ya kuhitimisha malengo yao.
“Kidini na kiutamaduni haingii akili, kama mwanamke anaetaka kujifungua kisha mpokezi awe mwanamme, lakini mtafanyaje na suala la kuwasomesha watoto wa kike linakuwa zito kwa jamii’’,alifafanua.

Hata hivyo Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, aliishauri jamii wanapokuwa na mtoto anataka kuendelea na masomo ngazi ya shahada, kuwenda kwenye taasisi zinazotoa mikopo.
Alieleza kuwa pamoja na ukata wa fedha unaowakabili wananchi walio wengi, lakini serikali imeanzisha utaratibu wa utoaji mikopo ambao unaweza kuwasaidia wanawake kusoma.
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa ZLSC Khalfan Amour Mohamed, aliitaka jamii wa Mgagadu kukitumia kituo chao kwa ajili ya kupata ushauri wa mambo mbali mbali ya kisheria ikiwemo ya ubakaji.
Mwananchi wa shehia hiyo Khadija Omar Msellem, aliomba msaada wa kisheria kufuatia Shirika la Umeme Pemba kuwakatia vipando vyao pasi na malipo.
“Jamani kisheria inakuwaje tunapokatiwa migomba yetu na kisha hakuna malipo, maana ZECO ilipitisha nguzo na hadi leo hakuna chochote’’,alilalamika.

Nae naibu sheha wa shehia hiyo Kassim Makame Juma, alikipongeza kituo cha huduma za sheria kwa uamuzi wake wa kuwafikia wananchi wake katika shehia hiyo na kuwapa msaada wa kisheria bila ya malipo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.