Na Miza Kona – Maelezo.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Moudline Castico ameitaka jamii kutoa mashirikiano kwa vijana wanatoka katika nyumba za kurekebisha tabia (Sober House) ili Vijana hao wasirudie kutumiaji dawa za kulevya.
Amesema sio jambo zuri kuwabagua na kuwanyanyapaa vijana hao kwa kuwatenga na kuwanyooshea vidole kwa kisingizio kuwa ni wateja kwa vile wanahitaji msaada mkubwa ili waenelee kubadilika na waweze kutoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa.
Waziri Castico ameyasema hayo huko Chukwani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati vijana hao walipotembelea Barazani hapo katika shamrashamra za kuadhimisha Siku ya kupambana na Dawa za Kulevya Duniani.
Amesema jamii isipokuwa tayari kuwapa ushirikiano vijana hao wanaweza kupata madhara makubwa na kurejea tena katika kutumia dawa hizo.
Amewapongeza vijana hao pamoja na Tume ya Taifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya kwa juhudi kubwa wanazochukuwa katika kuwasaidia kuwajenga katika maadili mema.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Welezo Hassan Khamis Hafidh amesema dawa za kulevya ni janga la taifa hivyo jamii inapaswa kuwafichua wafanyabiashara wanaoingiza na kusambaza dawa hizo bila ya woga na kuhakikisha kuwa wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kuratibu na Kudhibiti dawa za kulevya Bi. Kheriyangu Khamis ameomba kupatiwa eneo la kufanyia kazi vijana hao kwa vile hivi sasa ni wajasiriamali wenye vipaji tofauti na wanaweza kufanya shughuli za kujikimu kimaisha.
Nao vijana hao wameiomba jamii iwakubali na kuwapa mashirikiano na kuacha tabia ya kuwanyanyapaa kutokana hali waliyokuwa nayo awali kwani tayari wameshabadilika na wapo tayari kuisadia jamii kupiga vita janga hilo lisiendelee kuathiri vijana.
No comments:
Post a Comment