Kupata sh/=35.5 milion, ilisaidiwa
shilingi 9 milion na TASAF
Na Haji Nassor, Pemba
‘’TULILICHAGUA eneo hili, maana
likukua kama kichwa cha mtu alieokosa nywele, lilikuwa jeupe kama uwanja wa mpira
tu, leo unaona kiza kimetanda’’,.
Niliguna huu..!!!!..
na kushangaa kweli, hapa palikuwa na uwanja, kutokana na nini…. nikamuuliza
aliekuwa karibu yangu, kisha kajibu mbio, ndio palikatwa miti.
‘’Aaaa !!!! acha
tu wewe huwezi kuamini, kwamba miti hii iliopo tuliipanda hata kabla ya kupata
mradi huu kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania TASAF, leo
pazuri’’,alisema Mwenyekiti wa kikundi hicho Khamis Ali Juma.
Wakati
tukiutembelea mradi huo, huku tukipigwa na vitawi vya Mivinjem Misaji, Mikungu
na Mitondoo, ule upepo wa asili unaotokana na miti, ndipo hasa unapojitokeza
kwa mbali.
Hatukujali
jua lililokuwa kiliwaka wakati huo, maana hapo ni mithili ya ofisi ya kiongozi,
iliopambwa kwa viyoyozi zisivyokatiwa umeme daima, na huwezi kutamani kuondoka.
Kumbe miti
ndio asili ya upep bora, tena usiolipiwa kodi, na wala usio na madhara, ni
mazungumzo ya chini chini yaliokuwa yakisikika kutoka kwa baadhi ya watu
tuliokua katika msafara.
Mwenyekiti
huyo, baada ya ‘kukiet’ chini kati ya mti mmoja ndani ya shamba lao hilo
lililoko bonde la Dobi Wawi Chake chake Pemba, ndipo hapo alipopata fursa ya
kunipa utandu na ukoko.
Kwenye
shamba hili la ‘MEO’ wenyewe bila ya kuona uvivu na kwa lengo lilelile la
kuhifadhi mazingira, wameotesha miti zaidi ya aina tisa, huku wakiendelea
kuitunza ile ya asili kama Mzambarau.
Sikuwa na hamu ya kutaka kuondaoka ndani ya
shamba hilo, maana kila kona ya jicho langu linavyokwenda, hukumbana na
Mivinje, Mitondoo, Mikungu, Mikeshia na hata zao la Mkorosho.
Kwani
kiujumla hii aina ya miti ninayoiona imo mingapi, niliuliza na mwanachama wa ‘MEO’
Ali Khamis Omar ndie aliepewa jukumu na Mwenyekiti kunipa idadi halisi.
Bila ya
kuchachawa…. mwanachama huyo aliekuwa amevalia mavazi rasmi ya shambani,
alisema wanayo Mivinje 9,000, Mitondoo 300, Mikungu 700, Misaji 100, Miembe
250, Mikeshia 100, Mikorosho 200, bila ya kusahau zao la nanasi 4,000.
Lakini pia
MEO kwa vile lengo kuu ni kulirejeshea hadhi yake eneo hilo lenye urefu za
zaidi ya ekari tisa, (9) wameamua kuitunza miti ya asili kama Mizambarau,
Mitope tope na Mifuu.
Mwanachama
huyo wakati akizungumza na ukurasa wa makala, hakuacha kusema kumbe upandaji wa
miti unaweza kumvua mtu na umaskini alionao, kama atalijua hilo mapema.
Kihistori ya
Kikundi hicho cha shehia ya Wawi Wilaya ya Chake chake, Mkoa wa kusini Pemba, kilianza
mwaka 2011, ambapo hapo chini ya wanachama wao 19.
“Unajua
ndani ya MEO yaani ‘Mchekeni Environmental Organization’ wapo pia na wanawake,
lakini wanawake waliomo ni majasiri maana kila kazi wanafanya’’,alisema
Mwenyekiti
Wanachama wa
MEO walikuwa wakichacharika kwa nguvu, na hasa walikuwa wakipata hamasa, baada
ya wananchi wa Wawi wakiwacheka kutokana na kupannda miti isio na chakula cha
haraka.
“Hapa sisi
tulichekwa na jamii ya Wawi na vitongoji vyake, na wengine walitoka, lakini
tulishikamana na kutoa fedha zetu mfukoni, ili eneo hili tulipande
miti’’,alisema Katibu wa MEO Kombo Yahaya Juma.
MEO pamoja
na fedha taslimu na nguvu kazi, walijikuta wameshatumia zaidi ya shilingi 10
milioni, ambapo kama ukizichanganya za zile za TASAF, utakuta shilingi 19
milioni zimewekezwa msituni.
‘’Tulifika
hata kijiji cha Vitongoji, Wete kusaka mbegu za Mivinje, Mitondoo na Mikungu, wananchi
wengine walitushangaa’’,alinifafanulia.
Mvua za
masika kuanzia mwaka 2011 na mwanzoni mwa mwaka 2012, walizitumia vyema kwa
upandaji miti, na leo hii wakizisubiri kwa hamu fedha za mavuno ya miti, pale
watakapoanza kuvuna.
Ingawa Mwenyekiti
huyo, aliswenenaka sana kwamba walipata kazi kubwa sana wakati ilipokuwa
michanga miti hiyo, kutokana na wafugaji kutumia kama sehemu ya malisho ya
wanyama wao.
‘’Wengine
sisi wanakamati tulikaribia kuachana na mradi huu, maana wanaotufungia Ng’ombe
ni ndugu na jamaa zetu, na kila siku hua tunawambia, sasa ukienda jioni mifugo
imo’’,alisikitika.
Ingawa
alieleza kuwa wapo baadhi ya wananchi walikuwa mstari wa mbele kuwapa nguvu, hasa
kutokana na kuelewa kuwa mradi huo ni kwa ajali zaidi ya kuhifahdhi mazingira.
Lakini kazi
nzito zaidi ya mradi huo, ni pale walipofika wakati wa kuipalilia kwa maana ya
kuisafishia hapo ilibidi wanachama wahamie bondeni na wakafanikiwa.
“Ama kweli
kila mazigo ukikaribia kufika, ndio machofu houngezeka, maana na sisi wakati wa
kuilimia ugumu ulijitokeza, lakini tulifanya hivyo hadi leo imekuwa safi’’,alisema
wakati akiwa ameegemea Mvinje Mwenyekiti huyo.
Wakati huu
kwa mujibu wa wanaushirika hao, ni kwamba baadhi ya miti kulingana na aina ya
matumizi inaweza kuvunwa, lakini hilo hawajalifikiria kwa sasa.
‘’Unajua
ukitaka Mvinje hasa uunvune na kupata fedha nzuri, uusubiri alau miaka mitano,
nadio hapo ukitaka guzo la umeme, ukitaka ya kujengea na kazi nyengine’’, alielezea
kitaalamu Mwenyekiti.
Mradi huu
ualionza baina ya mwaka 2010 na 2011, kwenye mradi huo TASAF awamu ya pili
iliwapa ‘MEO’ jumla ya shilingi 9 milioni kwa ajili ya kujiendeleza.
Kwa mujibu
wa aliekuwa Mratbu wa ‘TASAF’ Pemba, Issa Juma Ali, miradi ya aina hiyo, walengwa
huwa hawapaswi kuchangia, fedha taslim bali ni nguvu kazi pekee.
‘’Miradi ya
aina hii wananchi hupata mteremko, kama wanaosukuma mlevi tu, wao mchango wao
ni jasho lao, na sio fedha kama ilivyo miradi mengine ya kimaendeleo’’, aliweka
bayana.
Kama Jumuia
hiyo ya ‘MEO’ itavuna kwa pamoja miti yote wanaweza kujipatia zaidi ya shilingi
35.5 milion, kwenye idadi yote ya miti ifikayo 25,000.
Ingawa
uongozi wa MEO ulisema lengo hasa, sio kuotesha miti hiyo na kisha kuvuna, bali
uvunaji wake utaenda samba mba na uhifadhi wa mazingira.
“Unajua
hatutaki kuotesha miti hii na kurejesha hali yake ya zamani, kisha akija mtu
aone pana jangawa, bali uvunaji wake tutaomba wataalamu watuelekeze’’,alisema
Katibu.
Juma Mohamed
ambae ni mwananchi wa Wawi, alisema mradi huo awali hawakuona kwamba, unaweza
kuleta maslahi, lakini kwa sasa hali ya eneo hili limeimarika.
Lakini Amini
Haji Ali na Asha Kombo Hilali wanasema suala la upandaji miti pamoja na
kuhifadhi mazingira, ni chanzo kikuu cha kujipatia fedha na mvua ikiwa mradi
huo utatunzwa.
Wakati suala la ukataji miti ovyo na
uchafuzi mwengine wa kimazingira ukifanyika sheria ya usimamizi wa mazingira ya
Zanzibar ya mwaka 2015 haikukaa kimnya.
Maana katika kifungu cha 51 (1) kimeweka
marufuku kwa mtu yeyote kuchafua au kumruhusu mtu mwingine kufanya kitendo hicho
kitakachosababisha uchafuzi wa mazingira kwa kukiuka viwango vyovyote vya
kimazingira vilivyoweka na sheria yoyote inayotumika.
Na ndio maana kifungu cha
(2) kimeweka adhabu kwa kwa yeyote atakayekwenda kinyume na masharti ya kifungu
hiki atahesabiwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatozwa faini
isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni kumi au
kifungo kwa muda kisichopungua miaka miwili na usiozidi miaka mitano au adhabu
zote mbili kwa pamoja.
Kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii, misitu kadhaa ya
Tanzania inabailiwa na changamoto kubwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu,
uvunaji holela wa mbao, miti ya majenzi na utipagaji mkaa.
Tanzania inakisiwa kuwa na hekari milioni 33 za misitu na miti
ya mbao, ambapo taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa na Kilimo kwenye utafiti
wale wa mwaka 2010 (Forest Resources Assessment) ulieleza kuwa imekuwa
ikipoteza wastan wa hekari 400,000 ya misitu kwa kwa miongo miwili mfululizo
sasa.
Ingawa juhudi za serikali ya Tanzania baada ya kujitokeza hilo
mwaka huo huo, ilianzisha shirika huru lenye dhamana ya kusimamia ustawi wa
misitu (Tanzania Forest Services Agency) ingawa taarifa zainaeleza shirikia
hilo lilishindwa kusimamia vyema, alisema Felician Kilahama.
Yeye ni Afisa Misitu Mwandamizi aliekuwa akifanya kazi katika
Idara ya misitu na nyuki Wizara ya Maliasili, Misitu na Utalii.
Asasi za kirai kama zikisimamiwa vyema na serikali kuu kwa
kushirikiana na Idara za mazingira na misitu, zinaweza kuimarisha misitu na
uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment