TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Ndugu, Waandishi wa Habari.
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mtukufu kwa kutujaalia uzima, afya njema na utulivu na pia kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu ya kila siku.
Pili, nikushukuruni sana ndugu waandishi
wa habari kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwapasha habari wananchi juu ya
masuala mbali mbali katika jamii yetu
ikiwemo kazi na majukumu ya Baraza la Wawakilishi.
Pia napenda kuwashukuru sana kwa mashirikiano
mazuri mliyonayo kwetu. Baraza la
Wawawakilishi linakupongezeni sana na kuwaomba muendelea kuwa karibu na Ofisi
yetu ili kuwafahamisha wananchi habari mbali mbali zinazohusiana na Baraza lao
tukufu.
Ndugu Waandishi wa Habari, Baraza la Wawakilishi linachukua hatua mbali mbali katika kuhakikisha kunakuwa na ushiriki mkubwa zaidi wa wananchi hasa katika mchakato wa utungaji wa Sheria za nchi yetu. Miongoni mwa hatua hizo ni kurekebishwa kwa kanuni zetu na hatimae kuelekeza miswada kusomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano mmoja na baadae kujadiliwa na kupitishwa katika Mkutano wa Baraza unaofuatia ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi kushiriki katika kutoa maoni yao. Kufuatia mabadiliko hayo, Kanuni inaelekeza baada ya miswada hiyo kusomwa mara ya kwanza itangazwe kwa wananchi ili waifahamu miswada hiyo na waweze kushiriki kutoa maoni yao mbali mbali.
Ni matarajio yetu kuwa maoni yatakayotolewa na wananchi, kwa kiasi kikubwa yatazisaidia Kamati zitakazoichambua miswada hiyo ili kuifanya miswada hiyo kuwa bora zaidi na hatimaye kupata sheria zitakazozingatia kwa upana zaidi maslahi ya wananchi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Katika Mkutano wa Tatu wa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi unaotarajiwa kuanzia mwishoni mwa mwezi ujao miswada minne ambayo tayari ilisomwa kwa mara ya Kwanza katika Mkutano uliopita itajadiliwa, miswada yenyewe ni kama ifuatayo;-
1.
MSWADA
WA SHERIA YA (UTAFUTAJI NA UCHIMBAJI) MAFUTA NA GESI ASILIA, 2016. Mswada huu
pamoja na mambo mengine utakuwa na lengo la kuanzisha Kampuni ya Maendeleo ya
Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) ambayo itashiriki katika shughuli za
utafutaji na uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa niaba ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
2.
MSWADA
WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA SUZA
NA MAMBO MENGINE YANAYOHUSIANA NA HAYO. Mswada huu una lengo la
kuunganisha Taasisi ya Uongozi wa Fedha (ZIFA), Taasisi ya Maendeleo ya Utalii
(ZIToD) na Chuo cha Sayansi ya Afya (CHS) kuwa chini ya Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar (SUZA).
3.
MSWADA
WA SHERIA YA KUANZISHA TAASISI YA ELIMU YA ZANZIBAR NA MAMBO MENGINE
YANAYOHUSIANA NA HAYO. Mswada huu unalenga kupendekeza kuanzishwa kwa Taasisi
ya Elimu Zanzibar, ambayo itakuwa ni wakala wa Serikali na itakuwa na jukumu la
kuandaa mitaala, vifaa vya kufundishia, kufanya tafiti za elimu zinazohusiana
na maendeleo ya mitaala na kuimarisha vifaa vya kujifunzia ili kuhakikisha
utoaji wa elimu kwa wananchi.
4.
MSWADA
WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALI MBALI NA MAMBO MENGINE YANAYOHUSIANA
NA HAYO. Mswada huu unarekebisha baadhi ya vifungu vya Sheria; zikiwemo Sheria
ya Mahusiano Kazini, Sheria ya Mahkama za Mahakimu, Sheria ya Mahkama ya
Biashara, Sheria ya Madawa na Usambazaji Haramu wa Madawa ya Kulevya, Sheria ya
Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, Sheria ya Biashara, Sheria ya Chuo Kikuu cha Kilimo Kizimbani
na Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo. Marekebisho hayo yanayopendekezwa
katika Sheria hizo ni kwa ajili ya kufanya marekebisho ya makosa yaliyomo
katika Sheria hizo na vile vile kuweka masharti bora ili kwenda sambamba na malengo
ya kuwepo kwa Sheria husika.
Ndugu waandishi wa Habari, katika
kuhakikisha kwamba wananchi wanapata
fursa na kushiriki katika Shughuli hii ya utungaji wa Sheria,
Afisi ya baraza la wawakilishi inawaomba
watume maoni yao kwa kwa Katibu
wa Baraza la Wawakilishi kwa njia ya maandishi kabla ya tarehe 9/9/2016.
Aidha, nakala za miswada hiyo zinapatikana katika Afisi ya
Katibu wa Baraza la Wawakilishi na hivyo kila mwananchi atakayependa, anaweza
kuomba kupatiwa nakala hizo.
Maoni yatumwe kupitia anauni
zifuatazo:-
1. Sanduku
la Posta (S.L.P. 902, Zanzibar)
2. Barua
pepe (zahore@zanlink.co au
3. Yaletwe
Afisi ya Baraza iliyopo Chukwani
1. Afisi
ndogo ya Baraza la Wawakilishi – Wete Pemba .
Mwisho kabisa napenda kuwashukuruni tena Ndugu
Waandishi wa Habari wa mashirikiano yenu mnayoendelea kutupa katika kuwapasha
habari wananchi.
Ahsanteni sana kwa kuniskiliza.
……………………
Amour M Amour,
Amour M Amour,
Kny: KATIBU,
BARAZA LA WAWAKILISHI,
ZANZIBAR.
Tarehe 17/8/2016
BARAZA LA WAWAKILISHI,
ZANZIBAR.
Tarehe 17/8/2016
No comments:
Post a Comment