Habari za Punde

Hotuba ya Rais wa Zanzibar, Al Hajj Dk Shein Baraza la Idd el Hajj


HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHE. AL HAJJ DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA BARAZA LA IDD EL HAJJ, 12 SEPTEMBA, 2016
SAWA NA MWEZI 10 MFUNGUO TATU, 1437 HIJRIA

BISMILLAH RAHMAN RAHIM

Sifa njema na shukurani za viumbe wote ni zake Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu anaevimiliki vyote, vilivyomo katika Mbingu na Ardhi.  Ni Yeye peke yake mwenye uwezo wa kuwaongoa waja wake kuwa wacha Mungu na watiifu wa maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.  Tunamuomba Mola wetu Subhanahu Wataala kwa utukufu wa siku hii, atujaalie sote tuongoke kwa kuyatekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.  Tunamuomba atupe nguvu ya kufanya mambo ya kheri na Ucha Mungu hadi mwisho wa uhai wetu ili tupate mafanikio hapa duniani na kesho mbele ya haki.

Rehma na amani zimshukie Mtume  wetu, Sayyidna Muhammad (S.A.W), aliyeletwa kuwa ni Nuru na Rehema kwetu sisi Walimwengu.   Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaaliye kuwa wafuasi wake wema na wenye kuyazingatia na kuyafuata mafundisho yake.  Tunawaombea rehma na maghfira wazee, ndugu, jamaa na wenzetu wote waliokwishatangulia mbele ya haki. Tunamuomba Mola wetu awape shifaa wagonjwa wetu wote na awaondolee mtihani wa maradhi yanayowasibu, Amin!

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamo wa Pili wa Rais,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;
Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Mheshimiwa Omar Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Mheshimiwa Sheikh Khamis Haji Khamis;
Kadhi Mkuu wa Zanzibar,

Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri,

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya,

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi,

Viongozi mbali mbali wa Serikali,

Viongozi wa Vyama vya Siasa,

Wageni Waalikwa,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana,

Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh

IDDI MUBARAK!

Baada ya kumtakasa na kumtukuza Mola wetu, Subhanahu Wataala, na kumtakia rehma na amani, mbora wa viumbe aliyeletwa kwa Waja ili awe kigezo chema; Mtume Muhammad (S.A.W), tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu; Mtukufu kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima tukaweza kuifikia siku hii ya sikukuu ya Idd el Hajj.  Kwa hakika, hii ni neema kubwa aliyoturuzuku Mola wetu hivi leo, ambapo Waislamu tuliweza kusali Sala ya Idd kwa amani katika maeneo mbali mbali wakati wa asubuhi na hivi sasa baadhi yetu tumejumuika katika viwanja hivi vya Skuli mpya ya Mkanyageni kwa ajili ya Baraza la Idd.  Kwa furaha kubwa, natoa mkono wa Idd kwenu nyote mliohudhuria Baraza hili, kwa wenzetu wanaotufuatilia kupitia vyombo vya habari na kwa Waislamu na Wananchi wote.

Namuomba Mwenyezi Mungu aijalie siku hii iwe ya furaha na salama kwa kila mmoja wetu.  Atujaalie sote tuwe wenye kunufaika na baraka za sikukuu hii. Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuwa    ni    wenye    kudumu  katika   kumshukuru   kwa   neema

anazoturuzuku, ili atuzidishie neema hizo kama alivyotuahidi katika aya ya 7 ya Surat Ibrahim yenye tafsiri isemayo:
Na (kumbukeni) alipotangaza Mola wenu (kuwa) “Kama mkinishukuru, nitakuzidishieni, na kama mkinikufuru (jueni) kuwa adhabu Yangu ni kali sana”

Mwenyezi Mungu atulinde na adhabu zake na tuendelee kumshukuru ili  atupe kheri na neema zaidi. Atujaalie kuzitumia katika kuyatekeleza mambo anayoyaridhia ili tupate mafanikio hapa duniani na huko Akhera twendako.

Ndugu Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujalia kuwa leo ni siku ya sikukuu, ambapo wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla, tunaungana na Waislamu wenzetu wa nchi mbali mbali katika kuisherekea siku hii tukufu.  Mwenyezi Mungu ametujaalia neema ya sikukuu hii ya Idd-el-Adha; yaani sikukuu ya kuchinja baada ya Waislamu wenzetu kwa maelfu kuikamilisha ibada ya Hijja katika mji Mtukufu wa Makka na kuishi japo kwa siku chache katika maeneo mashuhuri ya Saudi Arabia alikozaliwa Mtume wetu Muhammad (S.A.W).
 

Tunamuomba Mola wetu, Subhanahu Wataala, awajaalie Mahujaji wetu, Hijja njema na azikubali ibada zao zote walizozifanya, wakiwa wageni wa Mwenyezi Mungu katika maeneo matukufu.  Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Anas bin Malik (RA), kwamba Mtume Muhammad (S.A.W) amesema, mwenye kufanya Hijja na mwenye kufanya Umra ni mgeni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.  Mtu huyo hupewa anachoomba na hurudishiwa alivyovitowa kwa ajili ya kufanya ibada na huzidishiwa.  Mwenyezi Mungu awajaalie Mahujaji wetu wote wawe ni wenye kunufaika na ukarimu huo wa Mola wetu na awajaalie wadumu katika kuyatekeleza mafunzo waliyoyapata katika kipindi chote cha ibada ya Hijja na waendelee kuyatumia katika maisha yao ya kila siku.

Ndugu Wananchi,
Hatua ya Waislamu wenzetu kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu kwenda kuizuru nyumba ya Mwenyezi Mungu (Al-Kaaba) kwa kufanya ibada, ni kuitimiza nguzo ya tano ya Uislamu.  Vile vile, hatua ya kushiriki katika mkusanyiko  mkubwa wa Waislamu wa kila mwaka huko Saudi Arabia, ni kielelezo cha umoja wa waislamu duniani, kwa lengo moja tu, la kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja na kujiepusha kufanya vitendo vinavyomchukiza,

ili kuepuka adhabu Zake kama anavyotubainishia katika aya ya 52 ya Suratul Muumin katika tafsiri inayosema;
Na kwa yakini huu umma wenu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu, basi niogopeni.”

Kadhalika, katika kutudhihirishia udugu tulionao waja wa Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mtukufu ametwambia katika Qurani kwenye aya ya 10 ya Surat Al-Hujurat yenye tafsiri isemayo:
Kwa hakika Waumini wote ni ndugu (imani imeunganisha nyoyo zao); basi wapatanisheni ndugu zenu na mumche Mwenyezi Mungu ili akupeni rehema”.

Ndugu Wananchi,
Mwenyezi Mungu ni mwenye uwezo wa kutambua udhaifu wa Wanadamu katika kukabiliana na mitihani inayoweza kusababisha mgawanyiko miongoni mwetu kwa sababu mbali mbali.  Katika aya mbali mbali za Qurani, Mwenyezi Mungu ametuasa kuacha kuendekeza tofauti zetu kwa kuwa sote ni ndugu na katu tusifarikiane na kuacha kuifuata njia Yake ya kheri na salama ili tuweze kufanikiwa hapa Duniani na Akhera twendako.



Kwa hivyo, miongoni mwa mafunzo muhimu ya kuzingatia katika sikukuu hii ya Idd-el-Hajj ni kuibaini hali ya umoja na udugu wa Waislamu wote duniani katika mkusanyiko mkubwa kwenye uwanja wa Arafa.  Kwa upande wetu tulioko katika maeneo mengine duniani, na sisi nyoyo zetu zinaungana na wenzetu hao katika kuuadhimisha mkusanyiko huo mkubwa wa kila mwaka.

Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu wa kumuomba Mwenyezi Mungu, aujaalie mkusanyiko huo wa Waislamu katika mji Mtukufu wa Makka, wanaotoka kwenye Mataifa mbali mbali na watu wenye rangi, hadhi mbali mbali, wanaofuata madhehebu tofauti na wanaozungumza lugha mbalimbali, iwe ni sababu ya kuleta umoja na amani duniani.  Msingi mkubwa wa dini yetu ni umoja na amani, lakini hivi sasa tunaendelea kushuhudia mifarakano miongoni mwa Waislamu hali ambayo inaweza kusababisha kuvunjika kwa amani na kupelekea uharibifu mkubwa wa mali za watu, za Serikali na hata watu wanaweza kupoteza maisha yao. 

Kadhalika, hali ya kuwepo kwa mizozo na mivutano kwa baadhi ya Masheikh na Waumini inayotokana na misimamo yao, nayo inaweza kusababisha mifarakano katika jamii yetu.  Kwa nyakati

tofauti tumeweza  kuyashuhudia mambo haya hapa nchini kwa baadhi ya Masheikh na Maimamu wa misikiti wakisusiwa kufanya ibada kwa visingizio mbali mbali.   Mambo haya yanatokea miongoni mwa watu ambao kabla ya hapo tulikuwa wamoja katika ibada zetu na shughuli za kijamii, lakini imefika hadi leo tunahasimiana, tunanuniana, tunaharibiana mazao na mifugo yetu na tunadiriki hata kuchomeana moto makaazi yetu. Sote tunafahamu kwamba haya yametokea hivi karibuni katika kisiwa hiki cha Pemba katika Mikoa yote miwili. Sina haja ya kuzitaja sehemu yalikofanywa mambo hayo ya aibu na yenye kufedhehesha katika jamii yetu.  Mambo hayo yamemtia simanzi na kumuhuzunisha kila mmoja wetu.  Mwenyezi Mungu atuepushe na kufanyiana mambo maovu ya namna hiyo.

Ndugu Wananchi,
Mambo hayo ni kinyume na mafundisho ya Mwenyezi Mungu katika Qurani ambao ndio muongozo wetu pamoja na Hadithi za Bwana Mtume (S.A.W). Uislamu unatuhimiza umoja, mapenzi na ucha Mungu na kuacha kufarikiana kwani hivyo ni vitendo vya kishetani ambae amelaaniwa na Mwenyezi Mungu.  Sote tuvilaani vitendo vya aina hiyo na tukumbuke kuwa sisi ni wamoja na hatupaswi kuhasimiana kwa kufikia kiwango hicho.   Tunapaswa

tujitahidi kufanyiana mambo mema yenye kheri, kwani tukifanya hivyo,  ni ibada na ina malipo mema mbele ya Mwenyezi Mungu.

Katika hadithi iliyopokelewa na Twabraaniy, Mtume (S.A.W) amesema:
Amali ipendezayo zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu baada ya zile za faradhi, ni kumfurahisha Muislamu.”

Kwa hivyo, wajibu wetu ni kukimbilia kuyafanya mambo ya kheri yanayoiendeleza jamii, kuwafanyia watu mambo ya kuwafurahisha na kuyazingatia mafundisho ya dini, maadili mema, utamaduni na malezi tuliyoachiwa na wazee wetu.  Hayo ndiyo mambo ambayo tunayopaswa kuwarithisha watoto wetu na wale watakaokuja baada yetu.  Mafunzo ya dini yanatukataza kufanya mambo maovu lakini mafunzo hayo kwa upande mwengine yanatufundisha tushirikiane katika kheri na ucha Mungu.   Aya ya 2 ya Surat Al-Maidah inabainisha amri hiyo ya Mola wetu kwa kusema:

“Na saidianeni katika wema na ucha Mungu.  Wala msisaidiane katika dhambi na uadui.  Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu”.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuongoze katika kuyatekeleza mambo ya kheri na atuepushe mbali na adhabu zake.

Ndugu Wananchi,
Mafunzo mengine tunayoyapata kutokana na ibada ya Hijja waliyoitekeleza Waislamu wenzetu katika mji Mtukufu wa Makka, ni utii wa maamrisho ya Mola wetu kwa kuzitumia vyema neema alizoturuzuku zikiwemo uhai, afya na mali kwa kutafuta radhi zake.  Hili ni jambo la msingi la kulizingatia na kumuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe, kwani kutokana na udhaifu wa kibinadamu,  baadhi yetu huwa tunaghafilika.  Uhai, uzima wa afya na kuwa na mali huweza kuwajengea watu kiburi na mtu akajikuta anasahau lengo la kuumbwa kwetu na kuletwa duniani na la kumuabudu Mwenyezi Mungu, kama Anavyotukumbusha katika aya ya 56 ya Suratu -Dhaariyat isemayo:
“ Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu”.

Tunapaswa kila wakati tujitathmini katika vitendo vyetu tunavyovifanya kama vinakubaliana na lengo la kuumbwa na kuletwa kwetu duniani.  Haifai kufanya na kushabikia mambo mabaya kwani hayana hatima njema.  Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha kwamba vitendo viovu havitokei.   Mtume

(S.A.W) ametubainishia wazi wajibu wetu huo katika Hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim kwa kusema:

“Nyote ni wasimamizi, na kila mmoja wenu atasailiwa kuhusu namna alivyotekeleza usimamizi wake”

Tumuombe Mwenyezi Mungu atuwafikishe katika utekelezaji mzuri wa majukumu yetu katika njia anayoiridhia.  Atupe nguvu za kuzimudu nafsi zetu katika kuvishinda vitendo viovu.

Ndugu Wananchi,
Mbali na utii waliouonesha ndugu zetu katika kuitikia wito wa Mola wetu na kuitekeleza amri ya kwenda kuhiji, mafunzo mengine ya utii kwa Mwenyezi Mungu, yanapatikana kwenye kisa cha Nabii Ibrahim (A.S.) aliporidhia amri ya Mola wake ya kumchinja mwanawe wa pekee; Nabii Ismail.

Kisa hiki kinatufunza utii wa dhati waliokuwa nao wawili hao kwa kuridhia  amri ya Mola wao bila ya kusita kwa mategemeo ya kupata fadhila za Mwenyezi Mungu.  Kutokana na kufuzu kwao, Mwenyezi Mungu ndipo kwa kudura yake akawateremshia kondoo ili Sayyidna Ibrahim amchinje badala ya mwanawe Sayyidna Ismail. Kwa hivyo,  ikasuniwa kumchinja mnyama katika siku hii.  Kuchinja mnyama na kugawa nyama yake kwa marafiki na wahitaji wengine ni suna muhimu tunayopaswa kuitekeleza katika sikukuu hii ya Idd el Hajj kama alivyokuwa akifanya Mtume Muhammad (S.A.W) na Sahaba zake.

Ndugu Wananchi,
Utii ni kigezo muhimu cha ukamilifu wa imani.  Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuwe na utii Kwake na kwa Mtume wake pamoja na kwa wenye mamlaka juu yetu.  Hayo yameelezwa katika aya ya 59 ya Surat An-nisa yenye tafsiri inayosema:
Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu.  Na mkihitilafiana katika jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.  Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema”.

Kwa upande wa kijamii, utii ni kielelezo cha ustaraabu na msingi muhimu wa kuyaendeleza maadili mema katika jamii.  Aidha, utii wa sheria ni muhimu sana katika kudumisha amani, kuimarisha mshikamano na kuchangia katika kuleta maendeleo ya nchi.  Kutokutii sheria kunasababisha kuongezeka kwa vitendo viovu na makosa  mbali mbali ya  uhalifu ambayo yanaweza  kuwa chanzo

cha kuvunjika kwa amani na kuzikwamisha jitihada zetu za kujiletea maendeleo.  Kwa hivyo, kila mmoja wetu ana wajibu wa kuuona umuhimu wa kutii sheria bila ya shuruti, kwani nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya sheria na hakuna hata mtu mmoja au kikundi cha watu kilicho juu ya sheria.

Ndugu Wananchi,
Kwa nyakati mbali mbali nimekuwa nikisema kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha usalama na hali nzuri kwa wananchi.  Nililisema hilo katika Baraza la Idd el Fitri la mwaka huu kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni na kukinukuu kifungu cha 9 (2) (b) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.  Kutokana na kuendelea kujitokeza kwa vitendo vinavyoashiria kutaka kukwamisha jitihada za Serikali za kusimamia usalama na hali nzuri ya wananchi wetu, leo napenda nisisitize kwamba Serikali imesimama imara na haina mzaha katika suala la kusimamia amani na usalama wa wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea nchi yetu.

Napenda nimpongeze kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kusisitiza umuhimu wa kutunza amani nchini katika hotuba zake,

wakati wa ziara yake aliyoifanya Pemba na Unguja hapo tarehe 2 na 3 Septemba 2016. Naungana naye katika kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo.

Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kwamba watu wote wanaishi kwa amani na utulivu na wanapata fursa ya kufanya kazi na kwenda kutafuta riziki bila ya hofu.  Kadhalika, kuwepo kwa amani kutatuwezesha kupata wasaa mzuri wa kufanya vyema ibada zetu mbalimbali na kupata utulivu wa nafsi.  Nawaomba viongozi wa dini waendelee kutukumbusha na kutuhimiza kila mara kwani ukumbusho huwafaa walioamini.  Mwenyezi Mungu atujaalie sote tuwe miongoni mwao.

Vile vile, kuwepo kwa amani na utulivu nchini, kunaiwezesha Serikali kupata fursa nzuri ya kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi mipango mbali mbali ya maendeleo tuliyojipangia kwa lengo la kukuza uchumi na kuongeza Pato la Serikali.



Hivi sasa tayari Wizara zote kumi na tatu (13) nilizoziunda mara hii,  zimeshaandaa programu  ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020. Napenda nikuhakikishieni kuwa tumeanza vizuri katika kipindi hiki cha pili na tunategemea kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.  Wajibu wa wananchi wote ni kuziunga mkono jitihada za Serikali katika kuyafikia malengo yetu.  Mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya Serikali yanategemea sana namna wananchi wanavyoshirikiana na Serikali yao, kwa kujituma katika kufanya kazi zao na kusimamia kwa nguvu zote amani na utulivu.

Ndugu Wananchi,
Ushirikiano baina yetu una mchango mkubwa katika kuufanikisha utekelezaji mzuri wa mipango tuliyojiwekea katika kuinua uchumi wa nchi yetu, kuimarisha miundombinu ya uchumi na kuongoza upatikanaji wa huduma bora za jamii.  Kila mmoja wetu anaziona hatua kubwa za maendeleo tulizozifikia nchini katika Mikoa yote.  Haya ni matunda ya ushirikiano kati ya Wananchi na Serikali yenu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo tunayojiwekea. Wahenga wanasema “Mwenye macho haambiwi tazama”.  Napenda nikupongezeni sana wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba kwa hatua mliyofikia ya mafanikio katika sekta zote.  Hongereni sana.

Hivi sasa hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama katika Mkoa huu imefikia asilimia 80.  Makisio ya mahitaji ya maji kwa watu 228,350 wa miji ya Chake Chake na Mkoani na vijiji vya Mkoa huu ni lita 24,150,285 kwa siku.  Uzalishaji halisi kwa sasa ni lita 22,525,944 kwa siku sawa na upungufu wa lita 3,923,466.  Tuna matarajio makubwa ya kuongeza kiwango cha sasa kutokana na maendeleo ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji tunayoendelea kuitekeleza mijini na vijijini.

Lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kutoka asilimia 70 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 mwaka 2020 katika vijiji na katika miji kutoka asilimia 87 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 97 ifikapo mwaka 2020.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kulifikia lengo hilo.

Ndugu Wananchi,
Ni jambo la faraja na tumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na mafanikio tunayoendelea kuyapata katika huduma za afya ndani ya  Mkoa  wa  Kusini  Pemba  wenye  jumla  ya  vituo vya afya 27,

hospitali kubwa mbili ya Abdalla Mzee na Chake Chake na hospitali ndogo moja ya Vitongoji.  Kwa lengo la kuzidi kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya, Serikali inakamilisha kazi za ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Vikunguni na Ndagoni kwa Wilaya ya Chake Chake na Michenzani na Tasini, Mkanyageni kwa Wilaya ya Mkoani.  Aidha, tunakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani ambayo inatarajiwa kufunguliwa baada ya muda si mrefu panapo majaaliwa.  Azma ya Serikali ni kuzidi kuziimarisha huduma za afya zinazotolewa katika hospitali na vituo vyote vya afya kwa kuongeza madaktari, wataalamu mbali mbali na wahudumu wengine wa sekta ya afya, kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu na kuziimarisha huduma za maradhi mbali mbali, ili kuondokana na usumbufu wa kuzifuata huduma hizo katika maeneo ya mbali au nje ya kisiwa cha Pemba.

Ndugu Wananchi,
Mkoa wa Kusini Pemba umepiga hatua nzuri ya miundombinu ya barabara ambapo vijiji vingi vya Mkoa huu vinaweza kufikika kwa kipindi chote cha mwaka kutokana na kuwa na barabara za lami na zile zilizojengwa kwa kiwango cha kifusi.  Kazi ya matengenezo ya barabara katika Mkoa huu inaendelea ambapo hivi sasa  Serikali inaifanyia  matengenezo  barabara ya Mgagadu

hadi Kiwani (km 7.6) na barabara ya Ole hadi Kengeja (km 35). Vile vile, ujenzi wa barabara ya Mkanyageni-Jundamiti, kupitia Tasini hadi Kangani umekamilika; kwa kiwango cha kifusi pamoja na ujenzi wa daraja.

Wito wangu kwenu wananchi, muendelee kuwa na subira, wakati ujenzi wa barabara hizi ambazo zina mchango muhimu kwa maendeleo ya wananchi na upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ukiendelea.  Serikali itajitahidi kuhakikisha kwamba inatoa msukumo ili kuona kuwa ujenzi wake unakamilika kwa haraka kama ilivyokusudiwa.  Kadhalika, wananchi hasa wale wanaoishi katika maeneo zilimopita barabara hizo washirikiane na wakandarasi wetu kuvilinda vifaa na kuzuwia uharibifu wowote dhidi ya miundombinu hii ambayo imegharimu fedha nyingi.

Ndugu Wananchi,
Sherehe za Idd el Hajj tunazifanya katika msimu wa mavuno ya karafuu, msimu ambao ulianza mwezi Julai na utamalizika mwezi Oktoba, 2016.  Makisio ya mavuno ya mwaka 2015/2016 yalikua ni tani 3,685 kwa mapitio ya awali.  Hata hivyo, baada ya kupitia mara ya pili hali ya mazao imebainika kupungua ambapo sasa tuna matarajio  ya  kupatikana  tani 2,810  za karafuu.  Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia neema hii ambapo hapa katika kisiwa cha Pemba hadi kufikia tarehe 8 Septemba, 2016 vituo vyetu vya ZSTC vimeweza kununua tani 1,345.5 zenye thamani ya TZS Bilioni 18.8  Hii ni sawa na asilimia 47.9 ya makisio.

Napenda kuwapongeza sana wakulima wa karafuu kwa kuendelea kuuza karafuu zao katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa na kuzitumia vyema fursa zinazotolewa na Serikali kupitia Shirika hilo.  Serikali itaendelea kuwapatia wakulima bei nzuri, mikopo, vifaa na miche ya mikarafuu pamoja na kuziimarisha huduma katika vituo vya kununulia karafuu ili lengo la kulikuza na kuliendeleza zao hili muhimu kwa uchumi liweze kufanikiwa.  Kadhalika, nawasihi wananchi wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na magendo ya karafuu ili faida ya zao hili iweze kutunufaisha sote. Jitihada mnazozifanya za kuisaidia Serikali katika kupambana na wafanya magendo ziendelezeni, kwani zinatusaidia sote.

Ndugu Wananchi,
Leo ni siku ya furaha kwa hivyo sitopenda nikuchosheni kwa hotuba ndefu.  Hata hivyo, nasaha zangu ni kuwa tunaendelea kuyatumia mafunzo  ya ibada ya Hijja  katika maisha  yetu ya kila

siku. Tusherehekee Sikukuu hii kwa amani, kutembeleana, tuombeane dua, tuwaombee wazee wetu, ndugu na jamaa zetu waliotangulia mbele haki na vile vile, tuwaombee dua  waislamu wenzetu walioko katika mji mtukufu wa Makka ambao tunaungana nao katika sherehe hizi.  Mwenyezi Mungu awajaalie na wao sikukuu njema na awarudishe nyumbani salama.

Mafunzo ya Hadithi za Bwana Mtume (S.A.W) yanatufundisha juu ya kheri kubwa ya kuidiriki siku ya leo ambayo Mtume (S.A.W) ameeleza kwamba;
“Habakii yoyote siku ya Arafa mwenye imani (ndogo kama) ya mdudu chungu katika moyo wake ila Mwenyezi Mungu Anamsamehe. Akauliza mtu,  Hii ni kwa walio Arafa tu ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), au kwa wote? Mtume (S.A.W) akajibu, bali ni kwa watu wote” (Bin Humeyd).

Kwa hivyo, neema za Siku ya Arafa zinaenezwa kwetu sote ingawa kwa Mahujaji wetu huwa ni zaidi.  Kwa hivyo, tunapowasiliana nao tusiache kuwakumbusha watuombee dua na waiombee nchi yetu kheri ili tuzidi kuishi kwa amani, umoja na mshikamano.


Ndugu Wananchi,
Kabla sijamaliza hotuba yangu hii, napenda nitoe shukurani maalum kwa taasisi zote zinazowahudumia mahujaji wetu, waliopata uwezo wa kwenda kuitekeleza Ibada ya Hijja kama sote tunavyotarajia.  Ni vyema taasisi hizi zikaendelea kutoa huduma zao kwa kuzingatia imani zaidi na kuwaondelea wananchi usumbufu usio wa lazima.  Kadhalika, taasisi zinazoshughulikia Hijja ziendelee kushirikiana na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana kwa niaba ya Serikali kwani tunawajibu wa kuhakikisha usalama wa wananchi wetu.

Napenda nikuhakikishieni kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wahusika wote wanaoshughulikia masuala ya Hijja ikiwa ni pamoja na kuhakikisha azma yetu ya kuanzisha Mfuko wa Hijja.  Kadhalika, kwa kutambua kuwa watu wengi hutumia fedha zao za kiinua mgongo kwa ajili kwenda Hijja, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wastaafu wanapata fedha zao kwa wakati.  Kwa mfano, katika kipindi cha Januari hadi Agosti, kwa mwaka huu, Serikali imelipa jumla ya TZS Bilioni 16.2 kwa wastaafu 1,193 kwa ajili ya kiinua mgongo ambapo wastaaafu 90 waliomba fursa maalum kwa ajili ya kutaka kwenda Hijja na wakapewa kipaumbele.   Mwenyezi Mungu atuwezeshe kufanya vizuri zaidi ya hayo.

Ndugu Wananchi,
Kama tunavyoelewa, leo tunasherehekea Sikukuu ya Idd el Hajj katika Mkoa huu wa Kusini Pemba, ikiwa ni katika kuendeleza utaratibu tuliojiwekea ambapo Waislamu na wananchi walioko katika Mikoa yetu mbali mbali hupata fursa ya kujumuika pamoja katika kuisherehekea Sikukuu hii kila mwaka.  Mtakumbuka kuwa sherehe kama hizi mwaka jana tulizifanya katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Kamati ya Maandalizi kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kusini Pemba pamoja na Wilaya zake kwa kuzifanikisha sherehe hizi.  Nakupongezeni kwa dhati na natoa shukurani kwa Wananchi wote wa Mkoa huu pamoja na Wananchi kutoka maeneo mengine ya Pemba mliojitokeza kwa wingi katika Baraza hili la Idd na wale tulioshirikiana katika Sala ya Idd wakati wa asubuhi.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu azidi kuziunganisha nyoyo zetu, atupe mapenzi baina yetu na atuwezeshe kuendelea kushirikiana katika mambo yote ya kheri na maendeleo katika nchi yetu.


Ndugu Wananchi,
Namalizia nasaha zangu kwa kuzidi kuiombea nchi yetu amani na maendeleo zaidi.  Mwenyezi Mungu atupe mapenzi na uwezo wa kudumu katika kufanya mambo ya kheri.  Awajaalie watoto wetu wawe wema, wenye bidii katika masomo yao na wanaozingatia maadili na malezi mema tuliyoachiwa na wazee wetu.  Awaepushe kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuyaharibu maisha yao, jamii yetu na wawe Wazalendo na raia wema wa nchi hii.  Wale wanaojiandaa na mitihani, Mwenyezi Mungu awajaalie wafaulu katika mitihani yao yote.

Natoa shukurani zangu tena kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini, Pemba, kwa waandalizi wa shughuli hii pamoja na nyote mliohudhuria katika Baraza hili.  Kadhalika, natoa shukurani kwa vyombo vya habari na wale wote wanaotufuatilia wakiwa majumbani.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu aturudishe sote majumbani kwetu kwa salama na amani.
 
IDD MUBARAK
WAKULLU AAM WA ANTUM BIKHEIR


Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.