Habari za Punde

Rais Dk Sheni ahimiza na kusisitiza wakulima kuuza karafuu zao shirika la biashara la Taifa - ZSTC

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                            11 Septemba, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahimiza tena wakulima wa karafuu kuendelea kuuza karafuu zao kwa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar-ZSTC kwa kuwa kufanya hivyo kuna manufaa makubwa kwao 
binafsi na Taifa kwa jumla.

Dk. Shein ametoa wito huo leo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa ZSTC pamoja na baadhi ya wakulima wa zao hilo huko katika kituo kikuu cha karafuu wilaya ya Mkoani.

Dk. Shein ambaye alifika kituoni hapo kuangalia maendeleo ya ununuzi wa karafuu pamoja na usafirishaji wake alisema hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Saba zimerejesha tena hadhi ya zao la karafuu hivyo wakulima hawana budi kuuza karafuu zao ZSTC ili kuzidi kuendelea kulipa hadhi zao hilo.

“tuliwatazama wakulima kwanza kwa kuwapata bei nzuri na tukahakikisha kuwa biashara ya karafuu haibinafsishwi na ndio maana tukapitisha sheria kuwa Serikali ndie mnunuzi pekee wa zao hilo” Dk. Shein alifafanua.

Aliwaeleza watumishi hao na baadhi ya wakulima waliokuwepo kituoni hapo kuwa uamuzi wa serikali wa kuwapatia wakulima asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la nje ulikuwa uamuzi unaothibitisha dhamira ya serikali ya kuliendeleza na kulienzi zao hilo ambalo ni utambulisho wa Zanzibar.

“tumechukua hatua muhimu za kulifanyia mabadiliko shirika (ZSTC) kutoka kuwa lisilotengeneza faida hadi kuwa shirika lenye kutengeneza faida na kujiendesha lenyewe” alieleza Dk. Shein.

Dk. Shein aliwapongeza wakulima wote wanaoshirikiana na serikali katika kuliendeleza zao la karafuu ikiwemo kuuza karafuu zao ZSTC pamoja na kuwafichua wananchi wanaoshiriki uhalifu wa kufanya magendo ya zao hilo.

“kutokana na ushirikiano wa wananchi vitendo vya magendo ya karafuu mwaka jana vilishuka hadi chini ya asilimia tano” Dk. Shein alibainisha na kutahadharisha kuwa uuzaji wa karafuu kwa magendo kunaweza kuharibu sifa za karafuu za Zanzibar kwa kuwa biashara hiyo ya magendo haizingati taratibu za kulinda ubora wa karafuu.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wajumbe wa kikosi kazi pamoja na viongzoi wengine kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa masuala ya karafuu ikiwemo kuangalia usalama wake wakati wote.

Awali Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa msimu wa uchumaji na ununuzi wa karafuu unaendelea vyema hadi sasa na kubainisha kuwa walengwa wote wamewezeshwa kutekeleza majukumu yao.     

Akitoa taarifa kwa Mheshimiwa Rais, Afisa Mdhamini wa ZSTC Pemba Bwana Abdallah Ali Ussi alieleza kuwa hadi kufikia tarehe 9 Septemba, 2016 shirika hilo limenunua jumla ya tani 1371.6 kisiwani Pemba ambazo ni sawa na asilimia 51 ya makisio ya manunuzi ya tani 2,650.

Kati ya hizo alisema tani 1157.6 ambazo zina thamani ya shilingi bilioni 16.2 tayari zimeshasafirishwa Unguja na tani 183 zenye thamani ya shilingi bilioni 2.6 ziko katika kituo hicho cha Mkoani zikisubiri usafiri kupelekwa Unguja.

Kwa upande wa wilaya ya Mkoani, hadi tarehe hiyo ilikuwa tayari tani 780 zilikuwa zimeshanunuliwa ambazo ni sawa na asilimia 52 ya tani 1500 ambazo shirika hilo linatarajia kununua wilaya humo.

Akitoa maelezo zaidi kuhusu zoezi la ununuzi na usafirishaji wa karafuu katika wilaya hiyo mdhamini wa Shirika la ZSTC wilayani humo Bwana Seif Suleiman Kassim alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa hadi sasa hajapata malalamiko yeyote kutoka kwa wakulima wa karafuu tangu msimu wa ununuzi ulipoanza.

Hata hivyo changamoto kubwa inayolikabili shirika alieleza kuwa ni usafirishaji wa karafuu kwenda Unguja kutokana na meli kuchelewa kushusha mizigo inapofunga gati bandari ya Mkoani hivyo kuchelewesha kazi ya upakiaji.

Katika ziara hiyo Dk. Shein alifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum Said Soud.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anaendelea na ziara yake kisiwani Pemba na kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idd El Hajj litakalofanyika huko katika skuli mpya ya Mkanyageni.   

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.