Habari za Punde

Viwanja vilivyotumika kuombea kura, sasa vitumike kwa shukurani


Na Haji Nassor, Pemba

SEPTEMBA 2, mwaka huu rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: John Pombe Magufuli, alifika kisiwani Pemba na kuzungumza na wananchi wa mikoa miwili ya kisiwani humo.

Lengo hasa la mkutano huo uliofurika mamia ya wananchi, ilikuwa ni kuwashukuru kwa kumuingiza Ikulu ya Tanzania, baada kinyang’anyiro kizito mbele ya wagombea wenzake kutoka vyama vyengine.

Magufuli anakumbuka vyema Oktoba 15 alipofika kwenye uwanja huo wa Gombani ya kale, kuwaomba kura wananchi wa kisiwa cha Pemba, ingawa pia aliahidi kurudi kuja kuwashukuru.

Naam, ahadi yake hiyo ya kuja kuwapa neno la ahasante, shukuran, ‘thanks’ au kama wanavyosema wachina ‘xie xie’ ilitimia Septemba 2, akijua kuwa muungwana ni vitendo na sio maneno.

Kama hivyo ndivyo, lazima kwa viongozi wengine wakumbuke kuwa vile viwanja walivyovitumia usiku na mchana kuomba kura, sasa vigeuke kuwa viwanja vya kuwapa neno la shukuran wananachi.

Viongozi wetu wa majimbo, hatukumbuki pale tulipokuwa tukivivamia viwanja kwa saa na dakika kadhaa, kwa kuwaomba kura wananchi, sasa kama twakumbuka tuje tena kuwashukuru kwa kutimiza ahadi zao.

Mbona ilikuwa tunakutana Polisi kila mmoja akimueleza mgombea mwenzake kuwa yeye aliomba mwanzo uwanja fulani kwa ajili ya mkutano wa kuombea kura, sasa vipi tumesahau kwamba hatujawapa shukuran.

Wakati huo wa kusaka Jimbo, ilikua hata waandishi wa habari nao hawakunywa maji, kulikoni kuna mgombea anataka kuzungumza na wananchi tena wakati mwengine, hata kiwanja kisicho na hadhi, mgombea huyoo wamkuta, sasa je wako wapi?

Jawabu wapo majimboni, niwaulize? Je mmesahu sasa kuwaska tena waandishi wa habari na vipaza sauti vyao, kufanya mikutano kama ile, kwa ajili ya kuwashukuru wananchi?.

Waandishi wala hawana haja ya kuwakusanywa kwa kuwapa neno la ahasante, lakini hawa wapiga kura wetu, mbona sasa hatuoni shamra shamra za mikutano ya shukuran?

Wapo wagombea ukiwauliza walifanya mikutano ya hadhara pengine nane, sita au zaidi kwa ajili ya kusaka kura, sembuse ile mikutano ya ndani katika nyumba na vijiwe, leo wamesahau kupita humo humo kutoa shukuran, he maajabu haya.

Naamini hawajasahau kuwapa neneo la shukuran wapiga kura na wananchi wengine, pengine wametingwa na kazi za kiinchi, si unajua wengine mawaziri na wengine manaibu, lakini msijejisahau.

Maana kuna baraka kubwa na zenye thawabu ndani yake, iwapo mtu atampa shukuran mwenzake kwa kumfanyia wema, lakini sijui kinyume chake nini kwa kukosa kutoa shukuran.

Yeye rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: John Pombe Magufuli, na hata mwenzake wa Zanzibar, walishatimiza ahadi hiyo, maana septemba 2 alikuwa Pemba na kisha siku ya pili mapema Unguja kwa kutoa shukuran.

Sisi madiwani, wawakilishi na wabunge tumeshatoa shukuran kwa waliotuvisha suti, makoti na mitandio ya bei, kama bado wakati ndio huu.

Nanyi wananchi msisite kuwakumbusha viongozi wetu wote, kwamba walau kama walituwekea mikutanio kumi ya kuomba kura, sasa watuwekee japo mitano ya kutushukuru, maana hakuna kuna leo na kesho.

Lakini nayi makatibu na wenyeviti wa vyama, lazima muwakumbushe viongozi wetu hawa, kwamba wapite kurejesha fadhila kwa wananchi, maana miaka mitano mengine haiko mbali hata kidogo.


Mimi naamini kila jambo linawezekana, iwapo kila mmoja atafanya kazi zake kwa kufuata sheria na kanuni, na rushwa kwake ikiwa ni mwiko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.