Habari za Punde

Mama Mwanamwema asisitiza kudumisha amani na utulivu nchini

          
MKE wa Rais wa  Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amesisitiza haja ya kuiendeleza na kudumisha amani na utulivu kwani ndio msingi muhimu wa maendeleo na mustakbali mwema wa nchi. 
Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Nyumba za Wazee, Sebleni mjini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Mikoa ya Unguja wa Majimbo na Viti Maalum ikiwa ni pamoja na kuwapongeza kwa ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika maelezo yake, Mama Shein ambaye pia ni mlezi wa Umoja wa Wake wa Viongozi, aliwataka viongozi hao kuendelea kuielimisha jamii wakiwemo watoto na vijana juu ya umuhimu wa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjaji wa sheria sambamba na kuienzi amani iliyopo.

Aidha, Mama Shein aliwataka viongozi hao kudhamiria katika kuzuia vitendo vya udhalilishaji kwa kuelimishana na kuwakanya vijana na watoto badala ya kungojea mpaka litokee jambo ambalo linaleta madhara makubwa baadae.

Alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili jamii kwa hivi sasa ni kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji na kusisitiza kuwa taarifa za kushamiri kwa vitendo vya aina hii, havitowi taswira nzuri katika jamii hivyo lazima mashirikiano ya pamoja yawepo katika kuvikomesha vitendo hivyo vya aibu ambavyo ni kinyume na mafundisho ya mwenyezimungu, malezi na utamaduni wa zanzibar.

Mama Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi kwa niaba ya Umoja wa wake wa viongozi kwa kuchaguliwa na wananchi kushika nyadhifa walizonazo pamoja na kukipatia chama cha CCM uwezo wa kuongoza katika nafasi zote za uongozi kuanzia ngazi ya wadi, majimbo hadi katika ngazi ya Urais.

Sambamba na hayo, Mama Shein alisema kuwa kwa vile uchaguzi mkuu umekwisha, na Serikali iliyochaguliwa na wananchi kwa mujibu wa katiba imeshaingia madarakani na kilichobakia ni kuungana na kushikamana katika kuwatumikia wananchi na kuwaondolea changamoto zinazowakabili.

Nae Mama Asha Balozi, Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wake wa Viongozi aliwaeleza Wajumbe hao umuhimu wa Umoja huo sambamba na malengo na madhumuni yake katika kuisaidia jamii, kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi na kuileta nchi maendeleo.

Mapema Mama Fatma Karume alieleza haja kwa viongozi hao wa Majimbo kufanya vikao na mikutano na wananchi wao ili kujua changamoto zinazowakabili sambamba na azma ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Nao Wawakilishi hao waliahidi kutoa ushirikiano wao mkubwa katika kuhakikisha Umoja huo wa Wake wa Viongozi unaimarika huku wakiahidi kutoa michango yao mbali mbali ya hali na mali kwa umoja huo ambayo hatimae hurudi katika Majimbo yao.

Akitoa neno la shukurani Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alitoa pongezi kwa viongozi na wajumbe wote wa Umoja huo na kueleza kuwa kazi kubwa waliyoifanya tokea mwaka 2010 ni ya kupongezwa na kuungwa mkono na kuahidi kuwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi wako pamoja nao.

Alisema kuwa juhudi hizo ni miongoni mwa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwasaidia wananchi wake wote wa Zanzibar kwa kutambua kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki hivi sasa ni kujiletea maendeleo sambamba na kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2020.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822  
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.