Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein awapongeza akinamama na wanawake kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura uchaguzi uliopita

Na Rajab Mkasaba

MKE wa Rais wa  Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein ametoa pongezi kwa wanawake wote wa Unguja na Pemba kwa kujitokeza kwa wingi kwenda kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kupiga kura katika uchaguzi uliopita, licha ya baadhi yao kukumbana na vitisho mbali mbali mitaaani na hata katika familia zao.

Mama Mwanamwema Shein alitoa pongezi hizo huko katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji, Chake Chake Pemba katika mkutano maalum kati yake na Wanachama na Viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Katika hotuba yake Mama Shein, aliwapongeza akina mama hao kwa kusimama kidete katika kuitumia haki yao hiyo bila ya woga na kusisitiza kuwa ujasiri wao ni wa kupigiwa mfano.

Alisema kuwa kazi iloyopo mbele yao hivi sasa ni kuendeleza shughuli za ujenzi wa wa nchi  kwa kushirikiana na UWT na kuhakikisha kwamba wanawake hawaachwi nyuma.

Mama Shein alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanawake na wananchi wote kwa ujumla kuongeza bidii katika kuunga mkono juhudi za Serikali zenye lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi, ili waweze kujiajiri wenyewe.

Alieleza kufarajika kwake kwa kuwepo mwamko mkubwa wa kuanzisha vikundi vya Ushirika, SACCOS na kuongeza nguvu katika kilimo hasa cha mboga mboga.

Katika mkutano huo Mama Shein aliwakabidhi kadi wanachama wapya 30 wa Jumuiya ya UWT wa katika Wilaya hiyo ya Mkoani.

Nae Mama Asha Balozi, Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliwapongeza akina mama hao kwa juhudi walizozichukua katika kuhakikisha chama chao cha CCM kinaendelea kuongoza huku akiwasisitiza wanajumuiya hao kuwa kitu kimoja na kuondokana na ubinafsi.

Mapema Mama Fatma Karume, Mjane wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliwataka akina mama wasirudi nyuma na  badala yake wawe kitu kimoja na washirikiane kama akina mama wenzao walivyoshiriki katika harakati za kudai uhuru wa Zanzibar.

Nae Kaimu Katibu Mkuu, alitumia fursa hiyo kuwahamasisha akina mama hao kuchukua fomu za kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika Jumuiya hiyo katika uchaguzi ujao wa chama na kuwaeleza kuwa wanachama wote wa chama hicho sifa za kuongoza.

Akiwahutubia viongozi na wanachama wa Jumuiya ya UWT, Wilaya ya Wete, Mama Shein aliwaomba mashehe, walimu, wanasiaasa na wale wote wenye nafasi za uongozi katika Taasisi na Jumuiya mbali mbali wasimame kidete na kukemea vitendo vya udhalilishaji.

Alisema kuwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto bado vinaendelea kuriopotiwa katika Mkoa huo wa Kaskazini Pemba pamoja na Mikoa yote ya Zanzibar.

Mama Shein alisisitiza kuwa vita dhidi ya vitendo hivyo havitoweza kufanikiwa iwapo hawatochukua nafasi yao katikajamii kwa kuelimishana na kuwaelimisha watoto juu ya madhara ya udhalilishaji kwa kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atakeleze wajibu wake.

Nao Viongozi wa UWT, Wilaya ya Wete walimpongeza Mama Shein kwa utaratibu aliouchukua wa kwenda kuwashukuru na kuwapongeza akina mama hao kwa kushiriki vyema katika uchaguzi mkuu uliopita ambao umeendelea kuiweka CCM madarakani.

Viongozi hao walitunmia fursa hiyo kueleza baadhi ya changamoto walizokumbana nazo ikiwa ni pamoja na kususiwa kuuziwa bidhaa, misiba, harusi pamoja na kusisiwa katika masuala mengine ya kijamii.

Walimpongeza Dk. Shein kwa hatua anazozichukua za kusimamia mafisadi pamoja na jinsi anavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM huku wakieleza kuwa umoja wao ndio ngao kubwa iliyosababisha kupatikana kwa ushindi mkubwa wa uchaguzi uliopita katika Majimbo ya Wilaya na Mkoa huo.


Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Castico aliwaeleza akina mama hao juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kupambana na vitendo vya unyanyasaji, jinsi inavyowasaidia wazee, vijana, pamoja na wanawake na watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.