Habari za Punde

Ifahamu tangawizi na faida zake


Na. ALI M KHAMIS


Katika maisha ya kila siku kimekuwa ni kiungo muhimu na maarufu sana Duniani ambacho hupendwa na Watu wengi. Hukitumia katika matumizi mbali mbali ya kutia ladha na harufu nzuri kwenye chakula na vinywaji mbali mbali.

Kiungo hicho matumizi yake hukua siku hadi siku kutokana na umuhimu mkubwa unaopatikana ndani yake.

Kimekuwa maarufu sana katika shughuli za maisha ya kila siku, ambapo kila mtu amekuwa akikitamani kukipata kiungo hicho kila wakati kwenye kinywaji au chakula chake.

Watu wengi hupendelea kukitumia Kiungo hicho kama dawa ya kutibu maradhi mbali mbali. Hutumika pia Mikahawani kutengenezewa kinywaji maalumu ambapo kimekuwa ni azizi kwa wakaazi wa Zanzibar. Kinywaji hicho hunywewa asubuhi, jioni na usiku kama ni kiburudisho kinachokonga nyoyo za wanywaji.

Kwa jina la kitaalamu kiungo hicho kinaitwa Zingiber Officinale. Ni jina geni masikioni kwetu, lakini unapotaja kwa jina la Tangawizi, kila mtu anafahamu kuwa ni kiungo muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku.

Tangawizi ni aina ya zao la kiungo ambalo sehemu inayotumika ni ya tunguu (rhizone), ambalo huonekana kama mizizi ya mmea na inafanana na zao la Manjano au jina jengine Bizari.
Asili ya zao hili ni maeneo ya kitropiki ya bara la Asia na hasa katika nchi ya India na China.

Kwa upande wa Zanzibar zao hilo limekuwa halizalishwi ila huagizwa kutoka sehemu nyengine. Hata hivyo, Watu wa Zanzibar wamekuwa watumiaji wakubwa sana wa zao hilo. Wakati mwengine husema Chakula au kinywaji hakipiti rohoni bila ya kuisikia harufu ya Tangawizi ndani yake 

Zao hili linazalishwa kwa wingi katika nchi ya Jamaica na kwa hapa Tanzania hulimwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma , Tanga , Morogoro , Pwani na Mbeya.

Hakuna uthibitisho wa aina za Tangawizi ambazo hulimwa hapa nchini, lakini kuna dalili ya kuwa kuna aina za white Africa (Jamaica) na Cochin (Flint) ambayo huwa na tunguu ngumu yenye nyuzi.

Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya hewa ya Kitropiki kutoka usawa wa bahari hadi muinuko wa mita 1,500 au zaidi ambapo huhitaji mvua ya kiasi ya milimita (mm) 1,200 - 1,800 na joto la wastani wa nyuzi za sentigred 20 - 25.


Tangawizi hustawi vyema katika udongo wa tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.

Upandaji wa Zao la Tangawizi hutumia vipande vya tunguu vyenye kichipukizi kizuri angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sentimita (CM) 2.5 – 5. 

Wakati mwengine vichupikizi vinavyo patikana katika kumenya Tangawizi huweza kuhifadhiwa na kutumika kwa kupanda kiasi cha kilo 840 1,700 cha vipande vya tunguu ambayo huweza kutumika kupanda ni kati ya sentimita 23 -30 kwa 15 -23 na kina cha sentimita 5 10 na mara nyingi hupandwa katika matuta, na baadhi ya mazao huweza kupandwa katika shamba la tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa sio lazima kivuli kiwepo .

Vilevile hushauriwa kumwagilia maji endapo mvua inakosekana wiki moja hadi mbili. Kabla ya kupanda weka mbolea ya Samadi au Mboji kiasi cha kilo 25 -30 kwa hekta, kisha tandaza nyasi shambani ili kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapo kosekana. Pulizia dawa ya kuuwa magugu kama Round up.

Hata hivyo, Tangawizi huadhiriwa na magonjwa mbali mbali ya wadudu, kama madoa ya majani yanasababishwa na viini vya magonjwa ya Colletotrichum Zingiberis na Phyllosticta Zingiberis. Kuoza kwa tunguu kunasababishwa na viini viitwavyo Pithium SSP na mizizi fundo husababishwa na Meloidegyne SSP.

Katika suala la uvunaji, tangawizi huweza kuvunwa kati ya miezi 9 -10 baada ya kupanda wakati majani yake yanapogeuka kuwa rangi njano na mashina kunyauka.
Tangaizi inayo hitajika kwa kuhifadhi kwenye( preserved ginger in braine ) huvunwa kabla haijakomaa kabisa wakati ile iliyokomaa kabisa huwa kali zaidi na yenye nyuzi na hufaa zaidi kwa kukaushwa na kusagwa.

Hata hivyo, tangawizi husindikwa na kupata unga au mafuta maalumu (essial oils), vilevile Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa na kukatwa na kukaushwa juani au mara nyengine huchovywa kwenye maji yalio chemshwa kwanza na ndipo kukaushwa au kukamuliwa mafuta.

Pia Tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa zimechanganywa na sukari au chumvi bila kutia kitu chochote. Hata hivyo tangawizi ina kiasi cha mafuta (essial oil) cha 16 .0 18.0 %.

Tangawizi ni mmea kati ya mimea mingi yenye maajabu na huweza kutumika kama dawa na kutibu magojwa mengi mwilini zaidi ya 72 yaliyo ndani ya miili yetu na kutuacha tukiwa wazima na kutekeleza majukumu ya kila siku. 

Tafiti za kitaalamu zilizofanyika Duniani na kupitia mtandao wa Mitiki.blogspot.com imeonekana kuwa kiungo hicho kina faida zaidi katika mwili wa Binaadamu.

Tangawizi hutumika kama kiungo kwenye chakula au kinywaji na kuongeza ladha katika chai, soda na juisi na vyakula vyengine kama mikate, biskuti na keki.

Aidha hutumika katika dawa mbali mbali ambazo hutibu magojwa kama ya meno, kikohozi, muwasho wa ngozi na kuondoa mchafuko wa tumbo.


Vilevile tangawizi hutumika kutengenezea vipodozi kama vile Poda, Sabuni na katika manukato mbali mbali.

Wataalamu wamegundua kuwa Tangawizi husaidia kupunguza gesi tumboni, na kuimarisha utendaji kazi wa utumbo mdogo na mzunguko wa damu.

Hata hivyo wataalamu wanathibitisha kuwa tangawizi inaimarisha mfumo wa kinga ya mwili (Immune System), na huharakisha mgonjwa kurejea na nguvu baada ya matibabu.

Aidha wataalamu wanasema tangawizi huimarisha mfumo wa fahamu (Nervous System) na kutia madini joto mwilini.
  
Matumizi mengine ya zao hilo ni kuondoa harufu mbaya ya kinywa.

Pia wataalamu wa Afya wamegundua kuwa Tangawizi hurekebisha sukari ya mwili, pia huengeza hamu ya kula.

Faida nyengine ya Tangawizi ni kuyeyusha mafuta mwilini na kuondoa sumu pia mwilini.

Kama Waswahili wanavyosema kuwa Kinga ni bora kuliko Tiba hivyo tunapaswa kukitumia kiungo hicho kwa siku japo mara moja katika vyakula vyetu au vivywaji vyetu ili kuweza kupata faida kubwa inayopatikana kwenye kiungo hicho.

Hata hivyo, kiungo hichi kina faida zaidi kwa wagonjwa wa hasa walioathirika na ugonjwa wa UKIMWI. Hivyo kwa wale wenye matatizo kama haya wanaweza kupata faida zaidi ya maajabu ya Mmea huu wa tangawizi.

Makala hiyi imeandikwa kwa msaada wa vyanzo vya mitandao ya Mitiki.blogspot.com na globalpublishers.inform

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.