Habari za Punde

Balozi Seif azungumza na Uongozi wa Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao Tanzania { TaGLA }

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akizungumza na Uongozi wa Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao Tanzania { TaGLA } kwenye Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni.

Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Bwana Charles Senkondo na wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa TaGLA Zanzibar Bwana Zahor  Mohamed.
 Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Bwana Charles Senkondo Kulia akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Picha na – OMPR – ZNZ

Othman Khamis OMPR

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao Tanzania       { Tanzania Global Learning Agency – TaGLA } Bwana Charles Senkondo alisema uwezo wa kutolewa mafunzo  kwa wanafunzi na Wananchi wa Tanzania hapa Nchini unawezekana kutokana na mabadiliko makubwa ya Teknolojia yaliyopo hivi sasa Duniani.

Alisema mfumo wa upelekaji wa wanafunzi  kupatiwa Taaluma  ya juu  Nje ya Nchi unaoendelea kufanywa na baadhi ya Taasisi na Mashirika ya Umma na hata watu binafsi tayari umeshapitwa na wakati kwa vile umekuwa ukipoteza fedha nyingi zinazoweza kutumiwa kwa shughuli nyengine za Kijamii.

Bwana Charles Senkondo alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi katika Ofisi ndogo ya Balozi Seif  iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema kazi kubwa inayofanywa na Taasisi yake kwa takriban miaka 17 sasa ya kuwaunganisha Wanafunzi wa Tanzania kupata Taaluma katika kada na fani mbali mbali kwenye vyuo vya Kimataifa imeleta mafanikio makubwa na kuanza kukubalika na watu wengi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TaGLA alitoa mfano wa Sekta ya Afya Nchini iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo katika kuhudumia Jamii kutokana na mfumo wa mtandao wa Madaktari unaowaunganisha na vitengo vyengine vya kimataifa katika utoaji wa huduma za Afya.

“ Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao { Tanzania Global Learning Agency } wana uwezo wa kuwaunganisha watu na wanafunzi mahali popote duniani iwapo vitakuwepo vifaa katika Taasisi au shirika husika ”. Alisema Bw. Senkondo.

 Alisema yapo mafunzo mbali mbali yaliyokwisha tolewa na TaGLA hapa nchini na kushirikisha Watumishi wa Umma na Viongozi katika kuwajengea uwezo wa uwajibikaji  katika maeneo yao ya kazi.

Bwana Charles alisema  TaGLA pia imewahi kuandaa mafunzo kwa watumishi wastaafu kujiandaa na maisha  yao baada ya kustaafu yaliyotoa maarifa, mbinu, kubadilishana ufahamu pamoja na uzoefu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba lengo halisi la kuasisiwa kwa Taasisi hiyo ni kuiona Tanzania na Watu wake wanaenda sambamba na mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano uliopo Duniani.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuiunga mkono Taasisi hiyo ya Teknolojia ya TaGLA katika  azma yake ya kubadilisha maisha ya Watanzania katika mfumo wa kisasa.

Balozi Seif alisema jamii imekuwa ikishuhudia kupitia mitandao ya Kimataifa jinsi wananchi wa Mataifa yaliyoendelea jinsi walivyokuwa  na uwezo kamili wa kukamilisha masuala yao ya kimaisha na hata yale ya kibiashara kwa kutumia mfumo wa mtandao wa Internet.

Alimueleza Mkurugenzi huyo wa Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao Tanzania kwamba Zanzibar  tayari imeshaanza kuingia ndani ya mfumo huo ambao kwa sasa unawawezesha Wanafunzi wa chuo cha Udaktari kati ya Unguja na Pemba kusoma kwa kutumia mtandao wa mawasiliano ya Internet.

Balozi Seif  aliuomba Uongozi wa Taasisi hiyo kufikiria njia za kujiunga na Taasisi za Afya za Nchini India  ili ipatikane  huduma  itakayotolewa katika viwango vinavyomuwezesha Mwananchi wa Kawaida kuvimudu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.