Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Hoteli ya Ras Nungwi na Kuufariji Uongozi Huo kwa Kuunguliwa Baada ya Kupata Ajali ya Moto.


Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Meneja wa Hoteli ya Ras Nungwi Bibi Dana baada ya baadhi ya majengo ya hoteli yake kuungua moto katika kipindi cha dakika 20 kutokana na upepo mkali ulikuwa ukivuma maeneo hayo.
Balozi Seif akikagua baadhi ya majengo ya Hoteli ya Ras Nungwi yaliyoteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa ambayo hadi sasa bado haijajuilikana.
Kushoto ya Balozi Seif ni Meneja wa Hoteli ya Ras Nyungwi Bibi Dana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Meneja wa Hoteli ya Sazan iliyoko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Bwana Muhsin Sheha Mohamed  baada ya baadhi ya majengo ya hoteli yake kuungua moto.




Baadhi ya majengo ya Hoteli ya Ras Nungwi yaliyotekelea kwa moto mkubwa ulioambatana na upepo mkali.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaomba wawekezaji wa Sekta ya Utalii Nchini kufikiri njia mpya za kubadilika katika mazingira ya uwekezaji wao kwenye ujenzi wa majengo yao ya kudumu.

Alisema mfumo wa  ujenzi wa  majengo ya Hoteli  na nyumba za kulala wageni kwa kutumia rasilmali ya makuti katika ujenzi huo utaendelea kuwatia hasara hasa pale yanapotokeze  majanga ya moto.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa Ombi hilo wakati akipofanya ziara fupi ya kuufariji Uongozi wa Hoteli ya Ras Nungwi na ule wa Sazana Hoteli zilizopo katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja kufuatia moto mkubwa uliotokea ghafla majira ya saa Nne za Asubuhi ya Jumamozi ya Tarehe 4 Januari 2017.

Moto huo umesababisha hasara kubwa kwa majengo ya Hoteli zote mbili ambazo ile ya Ras Nungwi imepoteza Mkahawa, Afisi ya Utawala pamoja na jiko lote wakati nyumba Tatu za Kulala Wageni za Hoteli ya Sazana  zimeathirika na moto huo.

Balozi Seif alisema Serikali na Jamii zimekuwa zikishuhudia matukio mengi yanayoibuka kutokana na  majanga ya moto  kwenye sekta ya Utalii jambo ambalo linarejesha nyuma ile dhana nzima ya Serikali Kuu ya kutegemea Sekta hiyo katika kuongeza mapato ya Taifa.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isingependa kuona wawekezaji wa Sekta hiyo wanaendelea na mfumo wa matumizi ya makuti katika uwezekaji wa majengo yao kwa vile rasilmali hiyo imeshaonyesha wazi athari yake wakati unapotokea moto wa ghafla.

Akiupa pole uongozi wa Hoteli hizo za Ras Nungwi na Sazana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwakumbusha kuzingatia umuhimu wa kuweka Bima ya Moto itakayowasaidia wakati yanapotokea maafa ya moto kwenye maeneo yao ya uwekezaji.

Mapema Meneja wa Hoteli ya Ras Nungwi Bibi Dana alimueleza Balozi Seif kwamba  moto huo ulioambatana na upepo mkali ulisababisha hasara hiyo katika kipindi kifupi cha dakika 20.

Bibi Dana alisema Uongozi wa Hoteli hiyo uko katika kutafakari hatua ya kuijenga upya hoteli hiyo katika kipindi kifupi kijacho kutokana na Hoteli hiyo kuwekewa Bima ya Moto.

Meneja huyo wa Ras Nungwi alielezea faraja yake kutokana na Uongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vikiwemo vikosi vya ulinzi kufika eneo hilo la maafa kwa kuwafariji kitendo ambacho kimewapa matumaini mazuri ya kuendelea na uwekezaji wao ndani ya Visiwa vya Zanzibar.

Naye kwa upande wake Meneja wa Hoteli ya Sazana Bwana Muhsin Sheha Mohamed alieleza kwamba moto huo wa ghafla ambao bado haujajuilikana chanzo chake ulivamia nyumba Tatu za Kulala wageni katika Heteli hiyo na baada kutokana na upepo mkali ukarukia hoteli ya Jirani yao ya Ras Nungwi.

Bwana Muhsin alisema wafanyakazi wa Hoteli hiyo walilazimika kubomoa mapaa ya nyumba hizo kwa kuepuka hasara kubwa zaidi ambayo ingetokezea licha ya kwamba nyumba hizo alikuwemo Mgeni Mmoja tu kwa wakati huo.

Akiwa Mbia wa Hoteli hiyo na wenzake sita wa Mradi huo wa Hoteli ya Sazana Bwana Muhsini alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mipango ya baadaye ya mradi utazingatiwa baada ya kikao cha pamoja cha majadiliano kati ya wabia hao ambao wengine wako nje ya Nchi.

Kijiji cha Nungwi kilioko Kaskazini Mashariki ya Kisiwa cha Unguja kimekuwa kikikumbwa na matukio ya majanga ya moto hasa katika kipindi cha kiangazi kinachoambatana na upepo Kaskazi na kusababisha hasara kubwa ya mali na majengo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.