Habari za Punde

Baadhi ya Maeneo ya Skuli ya Raudha Hayaridhishi Yanahitaji Kufanyiwa Marekebisho.

Na. Takdir Ali na Rahma Khamis, Maelezo  

OFISA wa kitengo cha Afya na Mazingira kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Rahimu Shaha Bakari, ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa skuli ya Raudha kurekebisha matatizo yaliyomo ili kunusuru kufungiwa kwa skuli hiyo.

Amesema baadhi ya maeneo ya skuli hiyo hayako salama kwa wanafunzi, jambo alilosema  linaweza kusababisha maradhi ya mripuko hasa katika kipindi hichi cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha.

Amezitaja sehemu zisizoridhisha kuwa ni jikoni, kukosekana kwa karo ya kuhifadhi kinyesi, pamoja na kutokuwepo kifaa maalumu cha kuzimia moto (Fire extinguisher).

Kasoro nyengine alizozitaja ni mwangaza mdogo madarasani, mazingira machafu ya vyoo na uhaba wa vitanda vya kulalia wanafunzi.

Ofisa huyo pia alieleza kukerwa kwake kwa baadhi ya wafanyabishara kutopima afya zao, na wale waliopima kutokuwa na vyeti vinavyothibitisha kuwa wamefanya hivyo kutoka kitengo cha afya na usalama wa wafanyakzi hospitali ya Mnazimmoja.

Aidha amesema kitengo cha Afya na Mazingira kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa Wilaya Magharibi ‘B’, wanashugulikia masuala ya afya,  hivyo wameamua kufanya ukaguzi huo kwa mujibu wa sheria nambari 11 ya mwaka 2012.

Alisema kufuatia kuzuka kwa maradhi ya kipindupindu mwaka jana ambacho kilichukua muda mrefu kudhibitiwa, lazima jamii ichukue tahadhari ikiwemo kufuata kikamilifu maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Rahimu amefahamisha kuwa ili kuhakikisha magonjwa hayo hayatokei tena, ni lazima kila taasisi, maskuli, sehemu za wafanyabishara, maeneo ya kutupia taka na  mitaro inakuwa safi kwa muda wote.

Nae Mwalimu Mkuu wa Raudha Academy Bilali Badruddin Khamis, amekiri kuwepo kwa baadhi ya matatizo katika skuli hiyo na kuahidi kuyafanyia marekebisho ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Alisema katika kujikinga na maradhi ya mripuko, wameamua kuchukua tahadhari kubwa kwa kuajiri watu wa afya, kununua vitanda, mafeni na kuwapima afya wafanyabiashara na wafanyakazi.

Kwa upande wa wanafunzi wa skuli hiyo wamesema kuwa mazingira wanayoishi si ya kuridhisha  hasa kipindi hichi cha mvua.

Kwa hivyo wameuomba  uongozi wa skuli hiyo kuyafanyia marekebisho ili waweze kusoma katika mazingira yanayoridhisha.
                IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO –ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.