Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu wa Mauritius

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambae pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha Nchini Mauritius Dr. Ramakrishna Sithanen ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambae pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha Nchini Mauritius Dr. Ramakrishna  Sithanen kulia akizungumza na watendaji wakuu wa Sekta za Biashara, Viwanda, Mipango, Utalii na Uwekezaji Zanzibar. Kulia ya Dr. Ramakrishna ni Meneja Mkuu wa Hoteli ya Kimataifa ya Penny Royal ya Matemwe Saleh Mohammed Said Kushoto ya Dr. Ramakrishna ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Waziri wa Biashara Balozi Amina Salum Ali, Kamishna wa Mipango Zanzibar Nd. Juma Haasan Juma na Mkurugenzi Mkuu wa ZIPA Nd. Salum Khamis Nassor.
Balozi Seif kulia akimkabidhi zawadi za Viungo  Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambae pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha Nchini Mauritius Dr. Ramakrishna Sithanen mara baada ya mazungumzo yao.
Picha na – OMPR – ZNZ


Na Othmabn Khamis , OMPR
Uwajibikaji wa pamoja katika Sekta za Biashara, Viwanda, Mipango, Uwekezaji na Utalii ndio njia pekee  na sahihi inayotowa  muelekeo wa haraka wa kukuwa kwa Uchumi wa Nchi pamoja na ongezeko la Mapato ya Taifa lolote Duniani.

Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambae pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha Nchini Mauritius Dr. Ramakrishna Sithanen alieleza hayo katika mazungumzo ya pamoja na Watendaji Wakuu wa Sekta za Viwanda, Biashara, Utalii, Uwekezaji na Mipango chini ya Uwenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Dr. Ramakrishna Sithanen ambae ni Mtaalamu na pia  Mshauri Muelekezi katika Sekta ya Viwanda, Utalii, Biashara, Mipango na Uwekezaji alisema changamoto zote zinazoibuka katika harakati za Maendeleo hupata ufumbuzi wa haraka wa kukabiliana nazo katika njia ya uwajibikaji wa pamoja.

Alitanabahisha wazi kwamba ukuaji wa uchumi lazima uende sambamba na ujenzi wa miundombinu imara itakayosaidia pia kudhibiti ongezeko la idadi ya Watu ambalo linaweza kuvuruga mfumo mzima wa uchumi huo.

Dr. Ramakrishna alifahamisha kwamba Sekta ya Utalii ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya Tatu kwa Uchumi wa Dunia  ni sehemu kubwa inayoweza kusukuma kwa haraka Uchumi wa Zanzibar na kubadilisha ustawi wa Wananchi wake.

Alisema Mchezo wa Golf  unaojumuisha na kuchezwa na Watalii wenye kipato cha juu Duniani una nafasi pana ndani ya Sekta ya Utalii na akaitolea Mfano Nchi ya Mauritius ilivyokuwa Kiuchumi ndani ya kipindi kifupi baada ya kuamua kuimarisha Mchezo huo.

Naibu Waziri Mkuu Mstaafu huyo wa Mauritius aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia watendaji wakuu hao wa Taasisi za Kiuchumi na Uwekezaji kuangalia mbinu zitakazowezesha kuanzishwa huduma za Matibabu na pamoja na ujenzi wa Kumbi za Mikutano ya Kimataifa katika  lengo la kuufanya Utalii wa Zanzibar unakuwa wa Kimataifa.

Akitoa mawazo yake  katika Mkutano huo Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Balozi Amina Salum Ali alisema utekelezaji wa mipango katika miradi ya Maendeleo unakuwa wa kusuasua kutokana na ukosefu wa umakini kwa baadhi ya watendaji wa Taasisi za Umma.

Balozi Amina alisema hali hiyo pia imeleta usumbufu kwa uwajibikaji wa Watendaji wa Umma kutokana na baadhi ya vikwazo vya Wanasiasa vya kutowaamini wawekezaji wa sekta Binafsi wanaoamua kutaka kuwekeza miradi yao Visiwani Zanzibar.


Mapema asubuhi Dr. Ramakrishna Sithanen alikutana kwa mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambapo walikubaliana hoja ya Zanzibar na Mauritius kubadilishana uzoefu katika harakati za kuimarisha uchumi wa pande hizo mbili.

Balozi Seif alisema Zanzibar na Mauritius kwa vile ni visiwa vilivyomo ndani ya Bahari ya Hindi vinastahiki kufanya kazi kwa kushirikiana hasa katika uanzishwaji wa Viwanda vya kusindika samaki kutokana na kuzunguukwa na Bahari sehemu zote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Dr. Ramakrishna kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha Sekta ya Utalii inayotegemewa kuwa muhimili wa uchumi wa Taifa imekusudia  kuongeza nguvu zake katika uzalishaji wa mazao ya viungo ili kuwapa fursa watalii wanaoingia nchini kufaidika na mazao hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.