Habari za Punde

ADC Yapokea Wanachama Wapya 25 Kutoka Chama cha ADA-TADEA Zanzibar.

Na Abdi Shamnah
Wanachama wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) wametakiwa kushirikiana na serikali zilizoko madarakani, ili kufanikisha azma ya kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii wananchi.
Changamoto hiyo imetolewa na mwanachama wa Chama hicho Mussa Jangwa Bohero katika hafla ya kupokea na kukabidhi kadi mpya kwa wanachama 25 wa chama cha TADEA waliojiunga na chama hicho, iliofanyika katika makao makuu ya ADC Bububu.

Miongoni mwa waliokihama chama hicho, wapo viongozi watatu ambao walishiriki katika kugombea nafasi za uongozi ngazi za tofauti, katika uchaguzi mkuu  wa 2015.

Akizungmza katika hafla hiyo, mwanachama huyo aliefika kwa madhumuni ya kushudia tukio hilo, alisema ni wajibu wa wanachama wa chama hicho kushirikiana kikamilifu na serikali zilioko madarakani, kwa kuelewa kuwa ndizo zenye jukumu la kuwahudumia wananchi na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Alisema katika kufanikisha jambo hilo, wanachama wa ADC wana jukumu a kudumisha amani na utulivu uliopo nchini pamoja na kujenga mshikamano na wanachama wa vyama vyengine, ili kuleta ustawi wa Taifa.

‘‘ Tunapaswa kuhirikiana na serikali zilizoko madarakani, hizi ndio zenye dhima ya kuongaza Taifa hili hadi mwaka 2020, hivyo tuna wajibu wa kuzitii na kudumisha aman  iliopo’’, alisema.

Nae Issa Ame Issa, aliekuwa Katibu wa TADEA Mkoa wa Kusini Unguja, aliahidi kushirikiana an wanachama wa chama hicho (ADC) katika kuendeleza harakati za kukiimarisha chama hicho, ili kukiweka katika mazingira bora ya uchaguzi mkuu ujao .

Alisema yeye pamoja na wanachama wengine 25, wameamuwa kwa hiari yao kujiunga na ADC baada ya kuridhika na utendaji wake na kubaini kuwa ni chama chenye malengo ya kweli na sera zinazotekelezeka.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa ADC Zanzibar, Khamis Mohammed  Kombo alipokea kadi 25 za wanachama hao kutoka TADEA, sambamba na kukabidhi kadi mpya za ADC.

Miongoni mwa wanachama wapya wa ADC ambapo kabla walikuwa  Viongozi wa TADEA na kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa 2015 jimbo la Mtopepo ni pamoja na Hamad Rashid Kombo(Ubunge), Amana (Uwakilishi) pamoja na Khadija nafasi ya Udiwani.


Katika siku za hivi karibuni Chama cha TADEA kimekumbwa na jinamizi la kuondokewa na viongozi pamoja na wanachama wake na kujiunga na ADC, ambapo Julai, 4  mwaka huu, kundi kubwa lilikihama chama hicho. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.