Habari za Punde

Balozi Seif Alaani Kitendo Cha Kinyama Kilichofanywa na Vijana Kumkata Kwa Mapanga Utingo wa Daladala.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Kijana Khamis Mgaya Juma  aliyelazwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmmoja baada ya kushambuliwa na Vijana Mtoni Kidatu  Jumanne ya Tarehe 11 Julai 2017.Wa kwanza kutoka kulia  anayemsaidia Mgonjwa Khamis ni Baba Mzazi  Mzee Mgaya Juma na kulia ya Balozi Seif ni Muuguzi wa Zamu ya Wagonjwa wa Wodi ya Mifupa Biubwa Hassan Juma.
Majeruhi Khamis Mgaya Juma aliyelala kitandani akimuelezea Balozi Seif Mkasa uliomkubwa wakati aliposhambuliwa kwa mapanga na Vijana wasiopungua Saba Eneo la Mtoni Kidatu na kumjeruhi sehemu za Kichwa, Mikono na Miguu.
Balozi Seif akiwaagiza wauguzi kuzingatia maadili yao ili kupunguza malalamiko yanayotolewa na wagonjwa wakati akimfariji Kijana Khamis Mgaya aliyejruhiwa kwa mapanga Jumanne iliyopita.(Picha na OMPR.

Na. Othman Khamis OMPR. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameliagiza Jeshi la Polisi Nchini kuwasaka  na kuwatia mikononi  mara moja Vijana Waliohusika na kitendo cha kinyama cha kumshambulia kwa Mapanga Utingo wa Dala dala ya  bara bara ya Mtoni Kidatu - Darajani  Kijana Khamis Mgaya Juma mnamo Tarehe 11 Julai 2017.

Alisema kitendo hicho ambacho hakikubaliki kibinaadamu hata kisheria kinastahiki kulaaniwa na Jamii nzima na Serikali Kuu kupitia vyombo vya Ulinzi haitakubali kuona tabia kama hiyo inaendelea kushuhudiwa Mitaani.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kumkagua na kumfariji Kijana Khamis Mgaya Juma mwenye umri wa Miaka 24 aliyepata mtihani huo akiwa kazini mwake Hapo Mtoni Kidatu Wilaya ya Magharibi “A”.

Khamis Mgaya licha ya kupata majeraha makubwa sehemu za Kichwa, Miguu pamoja na mikono yote miwili baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi za Mapanga na Vijana zaidi ya Saba hivi sasa anaendelea kupata nafuu licha ya kubakiwa na maumivu katika mwili wake.

Balozi Seif alisema polisi licha ya doria wanazoendelea kuzifanya sehemu mbali mbali Nchini lakini bado kuna haja ya kuafuatilia nyendo za watu wanaoripotiwa kwao kuhusika na vitendo viovu ikiwemo ujambazi.

Alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza ikatoa fursa kwa wananchi kuwa na amani pamoja na utulivu wa kuendelea na harakati zao za Kimaisha bila ya wasi wasi wote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtakia matibabu mema Kijana Khamis Mgaya Juma na kumuomba aendelee kuwa na subira wakati huu wa maumivu wakati Serikali kupitia vyombo vya Ulinzi vitahakikisha wale wote waliohusika na tatizo lililomkubwa wanaonja mkono wa sheria.

Balozi Seif  halkadhalika waliwakumbusha Madaktari na Wauguzi  kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili bila ya kujali wanao muhudumikia ana wadhifa au cheo gani.

Alisema baadhi ya Madaktari hasa wauguzi wamekuwa wakiripotiwa kuhusika na vitendo vya kunyanyasa wagonjwa mambo ambayo yako nje ya maadili yao ya kazi.
Balozi Seif  alisema Serikali imetoa msukumo wa kuwapatia Wananchi matibabu bure lakini bado wapo baadhi ya watu dhana hiyo wamekuwa wakiiwekea vikwazo visivyo na msingi kwa kuwasumbuwa Wananchi hao.

Mapema Majeruhi Khamis Mgaya Juma alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba  alipatwa na kasa huo Jumanne ya Tarehe 11 Julai baada ya Mmoja wa abiria aliowachukuwa kwenye Gari yake kukataa kulipa Nauli.

Kijana Khamis alisema licha ya kumsamehe Kijana huyo baada ya kubishana muda wote wa safari lakini Abiria huyo aliamua kutafuta Vijana wenzake na kupanga njama ya kutaka kumfanyia hujuma wakati akiendelea na harakati zake za kazi.

Alisema Vijana hao walilazimika kukodi gari kumfuatilia Utingo huyo na hatimae kufanikiwa kumavia wakati wakishusha Abiria katika maeneo ya Mtoni kidatu wakitokea Mjini Darajani.

Khamis alielezea masikitiko yake pale alipoomba msaada kwa wasamaria waliopo katika na eneo hilo la tukio wakati akiendelea kushambuliwa kwa mapanga lakini wazee waliokuwa karibu ya tukio hilo walihamasisha Vijana hao kuendelea kumpiga.

Kijana Khamis Mgaya Juma alimshukuru msaramia Mmoja aliyekuwa akipita eneo hilo alipofanya juhudi za kutafuta gari na kumpelekea Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja bila ya msaada wowote wa watu waliokuwa karibu na eneo hilo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.