Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Balozi wa India

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Balozi wa India Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar  {ZAWA} Dr. Mustafa Garu.
Balozi Seif akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa India Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyomshirikisha Waziri wa Elimu Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Dr. Mustafa Garu.
Balozi Seif  wa Pili kutoka Kulia akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa India Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya aliyeko upende wa Kulia yake.
Wa kwanza kutoka Kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma, wa kwanza kutoka Kushoto ni Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana Setandar  Kumar na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Dr. Mustafa Garu.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa India Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao yaliyohudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki  Pembe Juma na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Dr. Mustafa Garu  Balozi wa India Bwana Sandeep alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa miradi mipya itakayostawisha Jamii kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili.

Balozi Sandeep alisema India hivi sasa imejipanga kuona miradi iliyoahidi kuitekeleza kwa Tanzania ya huduma za Maji safi na Salama upande wa Zanzibar pamoja na vifaa kwa ajili ya Vituo vya kazi za amali inakamilika kwa wakati.

Alisema uimarishaji wa Vituo vya Amali utatoa nafasi kubwa kwa Vijana kupata mafunzo ya vitendo yatakayowajengea uwezo mpana wa kujipatia ajira badala ya kusubiri kutoka Serikali Kuu.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru Serikali ya India kwa uamuzi wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzani kwa ujumla katika kusaidia miradi ya Maendeleo.

Balozi Seif alisema Miradi ya Maji safi na Salama Visiwani Zanzibar pamoja na Msaada wa Vifaa kwa ajili ya Vituo vya Amali  Nchini ni masuala ya msingi kwa wakati huu katika kuimarisha ustawi wa Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa India Nchini Tanzani kwamba Zanzibar bado inaendelea kuhitaji vifaa vya Kilimo kama Matrekta kwa lengo la kusaidia nguvu za Wakulima katika sekta ya kilimo.

Balozi Seif alieleza kwamba asilimia kubwa ya Wananchi wa Zanzibar wanaendelea kutegemea Sekta ya Kilimo katoka kujipatia riziki zao na kupunguza ukali wa maisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.