Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dkt.Mabodo Ashiriki Mazishi ya Watoto Wanne Waliofariki Baada ya Kujifungia Ndani ya Gari.

Wananchi na Waumini wa dini ya Kiislam wakiwa na mmoja wa Mwili wa Watoto waliofarika katika ajali ya kujifungia katika gari wakati ikiwa katika maegesho katika eneo la kidongochekundu Unguja baada ya kumaliza kuomba dua na kusaliwa kwa ajili ya hatua ya maziko yaliofanyika katika makaburi ya mwanakwerekwe Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla akishirikiana katika mazishi ya watoto waliopata ajali ya kujifungia katika gari na kupoteza maisha yao, maziko hayo yamefanyika katika makaburi ya mwanakwerekwe Zanzibar.


Na Is-haka Omar, Zanzibar. 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ ameshiriki katika mazishi ya watoto wanne waliofariki dunia  jana (juzi) baada ya kuingia kwenye gari iliyokuwa sehemu ya maegesho na likajifunga hali iliyopelekea watoto hao kukosa hewa na kufariki huko Kidongo Chekundu Unguja.  

Marehemu hao waliotambuliwa kwa majina ya Mwatma Mohamed Malawi (2), Haisam Mustafa(2), Munawar Ahmed Khamis (3) na Muslim Hamza bakar (2) wote wamezikwa leo katika maeneo tofauti ya Makaburi ya Mwanakwere na Kiembe samaki Mbuyu Mnene Unguja. 

Akizungumza mara baada ya maziko hayo Naibu Katibu huyo huko katika makaburi ya Mwanakwerekwe, alisema CCM imepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa ya vifo vya watoto hao na inatoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia zilizopata msiba huo na kuwasihi waendelee kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki cha msiba huo.

Alisema watoto hao walitarajiwa kuwa ni miongoni mwa viongozi na wataalamu wa fani mbali mbali wa baadae hivyo msiba huo umeacha pengo kubwa  kwa familia na taifa kwa ujumla.

Aidha Dkt. Mabodi aliwataka wazazi na walezi nchini kuwa karibu na watoto wao kwa kuhakikisha mazingira yanayotumiwa na watoto kucheza yanakuwa katika hali ya usalama ili kuepuka athari zinazoweza kusababisha majeraha ama vifo kwa watoto wao.

“ Kwa niaba ya CCM Zanzibar nawaomba wanafamilia wote wawe wavumilivu kwa kipindi hichi cha msiba huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya kubaini chanzo halisi cha vifo hivi na kutoa taarifa kwa umma.”, alisema Dkt. Mabodi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya ndugu na wazazi wa marehemu hao walifafanua kuwa (jana) juzi majira saa 5:00 asubuhi watoto hao walikuwa wakicheza katika maeneo ya nyumbani kwao ghafla hawakuonekana mtaani hali iliyozusha hofu kwa familia za watoto wao na wakachukua juhudi za kuwatafuta katika maeneo mbali mbali hasa katika bandari na maeneo mengine kwa kuhofia kuwa wameibiwa na watu wasiojulikana.

Akieleza zaidi Bw. Ahmed Khamis ambaye ni baba mzazi wa mtoto aliyefariki  ambaye ni Munawar, alidai kuwa katika harakati za kuwatafuta watoto hao walifanikiwa kuwapata  majira ya saa 2:00 usiku wa july 16, Mwaka huu wakiwa ndani ya gari moja lililokuwa limeegeshwa katika maegesho ya gari za mtaani ambalo mmiliki wake aliliweka kwa muda mrefu na alikuwa amesafiri.

Bw. Ahmed alieleza kwamba baada ya hapo yeye kwa kushirikiana na majirani mbali mbali walishirikiana kuvunja milango ya gari hilo na kufanikiwa kuwatoa watoto hao wakiwa wamezimia na kupelekwa hospitali kuu yaMnazi Mmoja ambapo baada ya kufanyiwa vipimo na madaktari wakaambiwa kuwa tayari wamefariki dunia kutokana na kukosa hewa kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa maelezo ya shuhuda mmoja aliyehusika na harakati za kuwatoa watoto ndani ya gari walipokutwa wamefariki alisema mazingira yake yanaonyesha kuwa kabla ya watoto hao kufariki walikuwa wakichezea gari hilo na walipoingia ndani mlango ulijifunga na kushindwa kutoka nje hali iliyosababisha kukosa hewa na kufariki dunia.

Viongozi mbali mbali wa serikali na Chama Cha Mapinduzi waliudhuria katika mazishi hayo wakiwemo Katibu wa Kamati Maalum, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bi. Waride Bakari Jabu, Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe  Ali Hassan Omar ‘King’ na  Waziri wa Kazi,uwezeshaji, wazee, vijana wanawake na watoto Maudline Castico.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.