MCHEZAJI Ng'ombe maarufu Kisiwani Pemba, Mzee Azani Salim Suwedi kutoka Uwandani, mwenye flana ya mikono mirefu, akimpiga chenga Ng'ombe wakati wa mchezo wa ngombe, uliofanyika Pujini Wilaya ya Chake Chake ikiwa ni shamra shamra za Tamasha la 22 la Utamaduni wa Mzanzibari (PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
NA ABDI
SULEIMAN, PEMBA.
WANANCHI
mbali mbali Kisiwani Pemba, wamejitokeza kushuhudia mchezo wa Ng’ombe, ikiwa ni
shamra shamra za Tamasha la 22 la Utamaduni wa Mzanzibari.
Mchezo huo uliofanyika katika kijiji cha Pujini
Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, huku ukihudhuriwa wananchi na
Viongozi mbali mbali wa Serikali.
Mchezo huo ulianza saa kumi za Jioni na kumalizika
saa 12 za jioni, huku ngombe watatu wakichezwa katika mchezo huo akiwemo
Kiburungo kutoka Uwandani Vitongoji, Toba Roho yangu kutoka Pujini, Pua mbovu
kutoka Vitongoji.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kumalizika kwa
mchezo huo, Naibu Waziri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mmanga
Mjengo Mjawiri, alisema ipo haja kwa wizara ya habari kurudisha utamaduni wa
mchezo wa ng’ombe kama ulivyokuwa ukichezwa zamani.
Alisema mchezo wa Ng’ombe ni moja ya vivutio vikubwa
vya kutangaza utalii wa Zanzibar, wareno wanautumia mchezo wa ngombe kwa kuitangaza
nchi yao na ndio waanzilishi wa mchezo huo.
“mchezo huu ni mmoja kati ya michezo mashuhuri kwa
Zanzibar, mchezo unapendwa na wananchi wengi hasa katika kisiwa cha Pemba, sasa
ni wakati Serikali kuurudisha tena mchezo huu katika asili yake’alisema.
Alifahamisha ipo haja kwa michezo yote ya asili ya
Zanzibar kurudishwa katika hadhi yake, ili vijana waweze kufahamu tamaduni zao.
Naibu Waziri huyo, alisema Serikali inapaswa
kuwawezesha wananchi, kuimarisha mchezo huo wa ng’ombe ili vijana na waweze
kufuata nyayo za mchezo huo.
Afisa mdhamini Wizara ya Habari Utalii, Utamaduni na
Michezo Pemba, Khatib Juma Mjaja, alisema lengo la tamasha hilo ni kuzifanya
shuhuli mbali mbali za Utamaduni na kuona zinapata nafasi kubwa.
Alisema tamasha hilo limeweza kuvuta hisia za
wananchi wengi kuweza kujitokeza na kuangalia utamaduni wao ambao, vijana wameanza
kuupa kisogo kwa kufuata tamaduni za kimagharibi
No comments:
Post a Comment