Habari za Punde

Mfumo Ligi kuu Zanzibar 2017-2018 kujulikana Jumamosi


 Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Vilabu 28 ambavyo vimo katika mchakato wa upatikanaji wa timu 12 za ligi kuu soka ya Zanzibar msimu mpya wa mwaka 2017-2018 watakutana na kupanga mchakato mzima wa upatikanaji wa timu kumi na mbili za ligi kuu msimu wa 2017-2018, kikao ambacho kitafanyika Jumamosi hii ya July 8, 2017 saa 3:00 za asubuhi katika Ukumbi wa Mikutano wa uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba.

Hayo yote yamekuja baada ya ZFA kuwa mwanachama wa 55 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF” ambapo moja ya agizo lao CAF ni kutaka msimu ujao wa mwaka 2017-2018 ligi kuu soka ya Zanzibar iwe na jumla ya timu 12 kwa Zanzibar nzima ambapo katika msimu huo wa mwaka 2016-2017 ulikuwa na jumla ya timu 36 kwa kila kanda ilikuwa ina timu 18, yani Kanda ya Unguja 18 na Kanda ya Pemba 18, huku zimeshashuka timu 12 kati ya hizo 36 kwa kila kanda zimeshuka timu sita (6).

Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kiliwatumia vilabu 14 vya Unguja barua ya kikao hicho ambapo ndani ya barua hiyo viongozi wawili kwa kila klabu kati ya Vilabu hivyo vya Unguja watahudumiwa na timu zao gharama zote za kwenda huko Pemba zikiwemo Usafiri, Kula na Malazi jambo ambalo kidogo limeleta mshtuko kwa timu hizo.

Viongozi wawili wawili wa Timu 14 za Unguja watakaokwenda  Pemba katika Mkutano huo ni kutoka JKU, Zimamoto, Jang’ombe Boys, Taifa ya Jang’ombe, Mafunzo, KMKM, Black Sailors, Polisi, Chuoni, Kipanga, Kilimani City, KVZ , Miembeni City na Charawe ambapo watashirikiana na vile vilabu 14 vya Pemba ili kupanga  mchakato mzima wa upatikanaji wa timu kumi na mbili za ligi kuu msimu wa 2017-2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.