Habari za Punde

Serikali yapiga marufuku uokotaji wa karafuu (mpeta)

NA/ SAID ABDULRAHMAN ----   PEMBA

KATIKA kupambana na vitendo vya udhalilishaji, Serikali imepiga marufuku uokotaji wa karafuu (mpeta) wakati wa zoezi la uchumaji wa zao hilo litakapo anza rasmi Kisiwani Pemba.  

Hii itaondosha ile dhana ya ‘mali kwa mali’ ambapo katika kipindi kama hichi cha msimu wa uchumaji wa zao hilo baadhi ya wananchi huitumia nafasi hiyo kufanya vitendo visivyo na maadili.

Akizungumza katika mkutano wa mapambano ya vitendo vya udhalilishaji na mapambano dhidi ya ukimwi huko katika ukumbi wa mkutano katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba,Ofisa tawala Mkoa huo, Ahmed Khalid Abdalla, alisema   kwa mwaka huu mikoa yote miwili imepeleka mapendekezo hayo Serikalini ili waokotaji wasiruhusiwe.

Alisema kuwa kwa mwaka huu mchumaji atalazimika kuokota karafuu zake mwenyewe au mtu aliyemo katika familia hiyo ndie tu atayeweza kuachiliwa kuokota ili kuepusha vitendo ambavyo vimekuwa vikitendeka.

‘Tayari tumeshapitisha mapendekezo yetu sisi na wenzetu wa Mkoa wa Kusini na tumeyapeleka Serikali kuu ili kuzuia mara moja wale wananchi wanaokota Karafuu kwa msimu huu wasiruhusiwe kwani mara nyingi huwa kunajitokeza vitendo viovu,”alisema Khalid.

Akiwasilisha mada juu ya muongozo wa mwitiko wa jamii  juu ya mapambano ya Ukumwi, Ofisa kutoka Tume ya Ukimwi, Jokha Mohamed, alisema kuwa tume imeandaa muongozo mpya ambapo umekamilika na lengo lake ni kusaidia kurahisisha utekelezaji wa mkakati wa tatu (3) wa Ukimwi kwa wadau wanaofanya kazi katika ngazi ya jamii.

 Alieleza kuwa mbali na hayo lakini pia utaimarisha uwezo wa kamati na Uratibu,Halmashauri,Mabaraza ya miji, Wilaya na Shehia katika kupanga,utekelezaji na kufuatilia na kutathmini muitiko wa jamii.

‘Lakini pia utafanikisha upatikanaji wa taarifa za VVU na ukimwi katika ngazi ya jamii,’alisema Jokha.

Hata hivyo Ofisa huyo alieleza kwa sasa hatua mbazo zinahitajika kuchukuliwa kwa haraka ni pamoja na kuharakisha uundaji wa kamati za uratibu katika ngazi zote pamoja na kutoa mafunzo kwa kamati kuu ili nao wawafunze SHACCOM zao.

Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Abeid Juma Ali, aliihakikishia kamati hiyo kuwa kwa upande wa Wilaya yake, itachukua jitihada za makusudi ili kuhakikisha DACCOM na SHACCOM zinafufuliwa na kufanya kazi zake.

“Niwahakikishie kwa upande wa wilaya ya Micheweni kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tutazifufua daccom na shaccom zote kwani  hapo awali tulikuwa hatuna bajeti hiyo ili kwa sasa tunashukuru tumepata,”alisema Abeid.

Hivyo alisema kila mmoja anawajibu wakutekeleza majukumu juu ya mapambano ya VVU na Ukimwi bila ya kuoneana haya na mapambano ya udhalilishaji wa kijimsia ulioenea katika maeneo mbali mbali .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.