NA/ SAID ABDULRAHMAN PEMBA.
WAAJIRI wa sekta binafsi wapatao saba (7) wamefikishwa Mahakamani na
mfuko wa hifadhi ya Jamii (Z.S.S.F) kutokana na makosa ya kutowasajili
wafanyakazi wao katika mfuko huo pamoja na kutowalipia ada zao.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Tibirinzi
Chake Chake Pemba,Meneja wa Mfuko huo Tawi la Pemba, Rashid Mohamed
Abdulla, alisema kwa mwaka 2016 – 2017 ni waajiri saba tu ndio
waliyoweza kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alieleza mfuko huo hauna nia ya kuwapeleka Waajiri Mahakamani ,bali
kuna baadhi ya waajiri wanakwepa sheria ya kuzisajili taasisi zao
pamoja na kuwasajili na kuwalipia wafanyazi wao waliowaajiri katika
sekta zao.
“Kuna baadhi ya waajiri ambao wanakwepa Sheria za kusajili taasisi zao
hivyo kwa upande wetu tunatumia Sheria ya mwaka 2005, ambayo inatupa
uwezo wa kuwapeleka Mahakamani ila tu kwa wale wakaidi ambao hawataki
kufuata sheria lakini hatuna lengo la kufanya hivyo,”alieleza Meneja.
Rashid, alifahamisha kwa sasa kesi ambazo zimeshafikia makubaliano ni
kesi nne (4) ambapo tayari waajiri wa sekta hizo, wamekubali
kuzisajili taasisi zao pamoja na wanyakazi wao na kuwalipia ada zao na
kesi tatu (3) tu ndizo bado wanaendeleana nazo huko Mahakamani.
“Kwa vile sisi mara nyingi huwa hatutaki kesi hivyo tunapofika kule
mahakamani huwa tunajaribu kutafuta suluhu kwa upande wetu na kwa
waajiri na anaekubali tu sisi tunaondosha shauri hilo
Mahakamani,’alisema Meneja Rashid.
Meneja huyo, alisema kuwa endapo mwajiri huyo atakubali kulipia ada
hizo hulazimika kulipa na faini japo kidogo kama ni adhabu yake.
Hivyo alitoa wito kwa wenye taasisi binafsi kuzisajili taasisi zao
pamoja na kuwalipia ada wafanyakazi wao na wasisubiri kusukumwa na
kufikishana katika vyombo vya sheria kwani hilo sio zuri.
No comments:
Post a Comment