Habari za Punde

Waandishi Pemba wadhamiria kuanzia mfuko wa kujisomeshea 4/7/2017


NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba wamesema, umoja na mshikamano ndio ngao pekee ya kuendeleza upendo miongoni mwao, ambao utaweza kuipeleka mbele tasnia ya habari nchini.
Walisema hayo wakati wa kikao cha kujadili mfumo nzima wa kuanzisha mfuko wa kujisomeshea kwa waandishi wa habari waliopo kisiwani Pemba, unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Walisema kuwa, ili kuendeleza umoja huo na kuona tasnia ya habari inasonga mbele zaidi, ni vyema kwa waandishi hao kuacha tofauti zao na kuacha ubaguzi, jambo ambalo, litaweza kuwasaidia katika kuimarisha maendeleo ya habari.
Mkutano huo wa kuanzisha mfuko wa kujisomeshea kwa waandishi wa habari Pemba, ulifanyika katika ukumbi wa Jumuiya ya waandishi wa habari Pemba (PPC), ukiwa na lengo la kumuwezesha mwandishi kupata fedha zitakazomsaidia kujiendeleza na masomo.
Mmoja wa waandishi walihudhuria kikao hicho kutoka kituo cha redio Istiqama Salim Ali Msellem alisema kuwa, kuanzishwa kwa mfuko huo, utawafanya wanahabari kuwa wamoja na sio kufarikiana.
“Popote kwenye kheri na bilisi hutembelea, hivyo ni vyema tukaweka uaminifu katika mfuko wetu wa fedha, ili tuweze kujiendeleza kielimu”, alisema mwandishi huyo.
Kwa upande wake mwandishi Abdi Suleiman kutoka shirika la magazeti ya Serikali kisiwani humo, alileza kuwa, mfuko huo wa fedha wa kuwawezesha kujisomeshea, iwe ni chachu ya maendeleo na uweze kuzaa matunda, ili kuwanufaisha waandishi kisiwani Pemba.
Nae mwandishi na mpiga picha wa shirika la utangazaji Zanzibar (ZBC), Raya Ahmada Mohamed alisema kuwa, kuanzishwa kwa mfuko huo ni faraja kubwa kwao, kwani utawawezesha kuwasaidia waandishi wasio na uwezo wa kujiendeleza na elimu ya juu.
“Kwa kweli wengi wetu tunashindwa kujiendeleza kielimu kutokana na kukosa fedha za kujisomeshea, lakini tutakapoanzisha mfuko huu, tutajikwamua na hali hii”, alieleza Raya.
Mapema Mwenyekiti wa muda wa Mfuko huo huo Haji Nassor Mohamed alisema kuwa, lengo la kuanzishwa kwa mfuko wa kujisomeshea kwa waandishi wa habari, ni kumrahisishia mwandishi kujiendeleza kielimu, bila ya usumbufu pamoja na  kuipeleka mbele tasnia ya habari.
“Mfuko huu ni muhimu sana kwetu, iwapo tutakuwa tayari kujitolea kwa kuanzishwa kwake, tunaweza kusonga mbele katika kujiendeleza na masomo ya ngazi za juu”, alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha aliwataka waandishi hao, kuwa na msimamo madhubuti sambamba na kuwa waaminifu katika mfuko huo, ili kuweza kuwanufaisha wao na taifa kwa ujumla.
Akzungumza kwa njia simu, mshauri wa mfuko huo Ali Hji Hamad, alisema dhana hiyo ni mzuri na inafaa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo ya kielimu na wanahabari kwa ujumla.
“Mfukp mzuri hasa kwa hilo lengo kuu la kuwasomeshea waandishi, maana wapo walio na hamu ya kusonga mbele lakini wanakwaza na fedha za kujiendeleza hivyo jengeni moyo wa ujasiri na uaminifu”,alishauri.

Mfuko wa kuwaendeleza kielimu waandishi wa habari kwa kuwapatia fedha taslimu kisiwani Pemba, unaweza kuwa mwanzo Tanzania hasa katika siku za hivi karibuni, ambapo zaidi ya waandishi 30 wanatarajiwa kuwa wanachama, ambao watachangia kati ya shilingi 30,000 hadi shilingi 50,000 na wastani wa shilingi 1.5 milioni zinatarajiwa kukusanywa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.