Habari za Punde

Watendaji Wizara ya afya wakagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Kijitoupele

 Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele Ali Sleiman Shihata akitoa maelezo ya ujenzi wa kituo kipya cha Afya kwa timu ya watalamu kutoka Wizara ya Afya walipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho. Wa katikati ni Mkurugenzi kinga na elimu ya afya Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla na (kulia) ni Diwani wa Kijitoupele Saleh Kinana.

 Mkurugenzi kinga na elimu ya afya Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla akisoma ramani ya kituo hicho na kutoa maelekezo kwa mafundi wanaojenga kituo hicho (katikati) Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele Ali Sleiman Shihata na wapili (kulia) ni Msaidizi daktari dhamana kanda Unguja Ali Kassim Amour.



Muonekano wa jengo jipya la kituo cha Afya cha Kijitoupele linalojengwa na Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Shamsi Vuai Nahodha na Mwakilishi Mhe. Ali Sleiman Shihata kwa kushirikiana na wananchi wao.

Picha na Makame Mshenga.

NA Mwashungi Tahir                       Maelezo
            
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amesema kujengwa vituo vya afya katika maeneo mbali mbali kutaweza kusaidia kupungua msongomano wa wagonjwa  katika Hospital kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja .

Hayo amesema Dkt Fadhil Mohammed Abdullah mkurugenzi wa kinga na elimu ya afya  kwa niaba ya waziri wa afya  wakati alipokuwa akikaguwa  kituo cha afya kilichokuwa meli nne katika jimbo la kijitoupele.

Amesema kituo hiki cha afya kilichojengwa hapo kina umuhimu mkubwa  sana hasa ukizingatia katika jimbo hilo  linaishi watu wengi sana hivyo kitakapokamilika na kuanza kazi kutaweza kupunguza idadi ya wagonjwa wengi wanaokwenda katika hospitali ya Fuoni au Mnazi mmoja.

Dr Fadhil amesema wananchi katika majimbo yao wana chachu kubwa ya kupatiwa maendeleo hivyo amewashukuru viongozi wa jimbo hilo kwa kuamua kujenga kituo hicho.

“labda niwashukuru viongozi wa jimbo hili kwa uamuzi walioufanya kwa kujenga kituo hiki cha afya katika eneo hili kwani kutaweza kuwaletea faraja kubwa wananchi wa jimbo hilo,” alisema mkurugenzi huyo.

Pia amesema kituo hiki kitakapokamilika kitakuwa kinatoa huduma zote muhimu ambazo zinatolewa katika hospital kuu ya mnazi mmoja ikiwemo sehemu ya kujifunguliya akinamama , ushauri nasaha, chanjo kwa akinamama na watoto, meno, na kupima presha na baadhi ya maradhi mengine.

Vile vile amewashauri wananchi hao kuwa na utaratibu wa kwenda vituo vya afya kwenda kupima afya zao kila baada ya muda na kupata kujua afya zao kwani kinga bora kuliko kutibu.

Nae mwakilishi wa jimbo hilo Ali Suleiman Shihata akitoa shukurani zake kwa viongozi wa jimbo hilo wakiwemo waliopita na wa sasa hivi kwa kukamilisha kituo hichi ikiwa ni moja ya ahadi zake alizoziahidi wakati wa kampeni  na sasa wanatimiza ahadi zao akiwemo mbunge na mwakilishi wa jimbo hilo.

Pia mwakilishi huyo ameahidi kuwa kitakapomaliza kituo hicho madaktari na manesi pamoja na wahudumu wengine watatoka katika jimbo hilo ili kupunguza usumbufu wa kwenda masafa marefu.

Jumla ya million 84 na laki nne zimetolewa na viongozi wa jimbo hilo wakiwemo mwakilishi na mbunge katika kukamilisha kituo hicho.
Nao wananchi wa jimbo hilo wametoa pongezi zao kwa viongozi wao wa jimbo kwa kupatiwa kituo cha afya  ndani ya jimbo lao na kusema kuwa watapunguziwa kwenda masafa marefu kuifata huduma hiyo hasa akinamama na watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.