Habari za Punde

Wana Diaspora wa Marekani Watoa Huduma za Matibabu ya Ngozi Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Bwana. Amiri Muhammed Amiri akimuonesha fangas Daktari bingwa wa ngozi Mamotheo alipokuwa akitoa matibabu katika hospitali ya Mnazi mmoja Mjini Zanzibar. 
Baba wa mtoto Abdulmajid akiwaonesha madaktari bingwa wa maradhi ya ngozi namna mwanawe alivyodhurika kwa kufanya mabaka mwilini katika hospitali ya Mnazimmoja mjini Zanzibar.  
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la kutoa huduma za Elimu ya afya Nchini Marekani Bi. Asha Mustafa  Nyang’anyi akizungumza na wandishi wa habari kuhusu ujio wao hapa Zanzibar.

Na Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar.
Wananchi wa Tanzania wanaoishi Marekani wanadiaspora wakishirikiana na Madaktari bingwa wapo nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya  maradhi mbalimbali yanayowasumbua wananchi.

Zoezi la kutoa huduma hizo za matibabu bure linafanyika kwa muda wa siku tatu katika Hospitali ya Mnazi mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari huko katika kitengo cha maradhi ya ngozi  kwenye hospitali kuu ya Mnazi mmoja,  Mwanadiaspora Idi Seif Sandaly amesema wameamua kuja nchini hapa kutoa huduma hizo ili kuwasaidia wananchi  wenye matatizo mbalimbali.

“Tumekuja Zanzibar kwa lengo la kuwasaidia wananchi ambao wana maradhi mbali mbali na kuwapatia matibabu kwa kupitia jumuiya yetu ya marekani Health Education Development  kwa kutibu maradhi ya ngozi , sukari  na pressure  pamoja na maradhi ya akinamama.” Amesema Mwanadiaspora huyo.

Sandaly  amesema wapo kwa muda wa siku tatu na wamekuja na dawa za kutibia maradhi hayo ambapo dawa hizo wanazitoa bure bila ya gharama zozote kwa wananchi.

Amesema katika matibabu yao wanatarajia kutoa huduma kwa zaidi ya Wananchi 3,000 watakaofika katika Hospital hiyo ya Mnazi mmoja.

Akifafanua kuhusu gharama za Dawa hizo ambazo wamekuja nazo kutoka Marekani amesema zaidi ya Dola Million moja  za Marekeni zimetumika kwa ajili ya kununulia Dawa hizo.
Hata hivyo ameongeza kuwa Nusu za Dawa hizo zitatumika Zanzibar na Nusu yake zitapelekwa Mkoa wa Bukoba kwa lengo la kusaidia matibabu mkoani huko

Nae Daktari wa maradhi ya Ngozi kutoka Marekeni Dkt Mamotheo Lepheana amesema amefarijika kuona wananchi wamejitokeza kwa wingi hasa wa maradhi ya ngozi.

Sambamba na hayo mgonjwa aliyepata matibabu hayo ya ngozi Masika Juma Mussa  mkaazi wa Mwera amesema ameshukuru kupatiwa huduma hiyo na kuiomba serikali iendeleze kuleta wataalam kama hao wanaotaka kusaidia jamii .

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo la kutoa huduma za Elimu ya afya Asha Mustafa  Nyang’anyi amesema ameamua kuja Zanzibar  kwa sababu wananchi wa hapa ni wakarimu na wanaojali kusaidiwa.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.