Habari za Punde

Balozi Seif Awataka Wananchi wa Kijiji Cha Tumbe Kuunda Timu ya Kuliongoza Soko la Samaki na Mboga mboga Tumbe.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Omar Shomar  mwenye shati la maua akifafanua hatua zilizochukuliwa katika maandalizi ya ujenzi wa Banadari ya Tumbe  wakati wa ziara ya Balozi Seif Kisiwani Pemba.
Mkuu wa Idara ya Uvuvi Kisiwani Pemba Nd. Sharif Mohamed Faki  mwenye shati rangi ya Buluu akimpatia maelezo Balozi Seif  juu ya juhudi za kulitafutia ufumbuzi tatizo la kusita kwa huduma za Soko la Tumbe.

Mandhari wa Eneo la Pwani ya Tumbe lililopendekezwa kujengwa Bandari ili ikidhi mahitaji ya Usafiri wa Baharini ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.(Picha na OMPR ZNZ)Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Mkoa Kaskazini Pemba, Taasisi zinazosimamia Sekta ya Uvuvi Kisiwani humo kukaa pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Tumbe ili kupata Timu itakayosimamia uendeshaji wa Soko la Samaki na mboga mboga la Kijiji hicho.


Alisema Soko hilo limejengwa maalum kwa lengo la kutoa huduma za upatikanaji wa samaki na mboga mboga na Serikali Kuu itapendelea kuona huduma zilizokusudiwa kutolewa katika soko hilo zinaanza mara moja.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipolitembelea Soko la Tumbe akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya ziara ya Siku Mbili Kisiwani Pemba kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kujua changamoto zinazoathiri shughuli hizo katika Mikoa Miwili ya Kisiwa hicho.

Soko la Tumbe lililojengwa na Serikali kupitia mradi wa Macemp lilizinduliwa na Rais wa Zanzibar Mwaka 2015 na kutoa huduma Miezi Miwili tu na baadae kusita kutumiwa katika muda wote hadi hivi sasa baada ya kutokea mivutano baina ya Wananchi na Taasisi zinazosimamia Soko hilo.

Balozi Seif alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haiwezi kuona fedha nyingi ilizotenga zinapotea bure bila ya sababu   maalum katika miradi iliyoelekezwa kutoa huduma kwa Jamii.

Alisema ufumbuzi wa soko hilo lazima upatikane, vyenginevyo Serikali Kuu italazimika kuangalia njia nyengine ya kuyatumia majengo ya soko hilo badala ya lengo ililokusudia kwa ajili ya Soko la kuwahudumia Wavuvi kufanya biashara zao kwa makini na usahihi.

Alifahamisha kwamba ni vyema Wananchi wakaendelea kujenga mazingira ya kuvumiliana na kuacha ushabiki unaoonekana kutenganisha Watu na kupelekea hata familia moja kutofautiana katika harakati zao za kimaisha za kila siku.

Mapema Mkuu wa Idara ya Uvuvi Kisiwani Pemba Ndugu Sharifu Mohamed Faki alisema Soko la Tumbe lilianza ujenzi wake mnamo mwaka 2012 likilenga kusaidia Wavuvi wa Kisiwa cha Pemba.

Nd. Sharif alisema  huduma za soko hilo zilitolewa miezi miwili tuu baada ya uzinduzi na baadae Wavuvi wa eneo hilo waliamua kuendeleza mnbada nje ya majengo hayo kitendo ambacho Uongozi wa Serikali ya Wilaya, Mkoa na Taasisi zinazosimamia Sekta ya Uvuvi kufanya vikao na Wavuvi hao ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Akizunguma na Uongozi wa Hospitali ya Wete pamoja na Wizara ya Afya mara baada ya kukagua huduma za afya zinazotolewa kwenye Hositali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuwagiza uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha wananunua vifaa muhimu vya hospitali kwa ajili ya kuhudumia wananchi.

Alisema inasikitisha kuona hospitali kubwa ya Wete  inakosa vifaaa muhimu kama Mashine ya Ultrasound , BP vifaa ambavyo ni muhimu katika kuwafanyia uchunguzi wa kina wagonjwa kila wakati.

" Inasikitisha sana kuona Wizara nzima ya Afya inashindwa kununua mashine ya Ultrasound yenye tahamani ya Milioni 15 japo ndogo tu,mashine ya BP Elfu 45,000/= hali hii inauma sana kama kifaa hichi pia hatuwezi kununua”alisema.

Aliwasisitiza watendaji kuwa na lugha nzuri wakati wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa, kwa kufuata maadili ya kazi na taaluma zao zinavyoelekeza na sio kuwatolea maneno yasiofaa wagonjwa.

“Simamieni maadili ya taaluma zenu wakati wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa, yoyote atakaekwenda kinyume na taaluma yake tutamsamehe” Alisisitiza Balozi Seif.

Akizungumzia suala la Posho kwa muda wa ziada Balozi Seif  aliutaka Uongozi wa Wizara ya Afya kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi fedha zao za muda wa ziada zote wanazodai kabla ya kuondoka Kisiwani Pemba.

Alifahamisha kuwa baadhi ya wafanyakazi wanadai fedha zao za tokea Mwezi wa Januari, wameweza kulipwa miezi Mitatu Januari na Machi jambo ambalo linarudisha nyuma utendaji wa wafanyakazi hao.

Hata hivyo akizungumzia upungufu wa Wafanyakazi, alisema inasikitisha kuona wafanyakazi wanaajiriwa Pemba, baadae wanaomba uhamisho kwenda kufanya kazi Unguja, wakati ajira zao ziko Pemba.

“Mfanyakazi yoyote atakae ajiriwa Pemba na kuomba uhamisho kwenda Unguja, Wizara isimpokee na bora tumsamehe aende kufanya kazi popote anapotaka hata Tanzaiabara” Alisema Balozi Seif.

Aidha alipongeza wafanyakazi wa Hospitali ya Wete, kufanya kazi kwa kufuata Sera ya Serikali matibabu bure kama ilivyoanzishwa na muasisi wa Mpainduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi msaada wa Mashuka 50, Mipira 500, Geleni Tisa  za Dittol, Vigari vya Wagonjwa vitano na Mashuka ya Vitanda Tisa.

Mapema Naibu Waziri wa Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Harous Said Suleiman, alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, kwa msaada aliutoa kwa Hospitali ya Wete.

Alisema msaada huo umefika kwa wakati na utatumiwa kwa lengo lililokusudiwa, kwani utaweza kupunguza tatizo la vifaa katika hospitali hiyo.

Akisoma  Risala ya Wafanyakazi wa Hospitali ya Wete, Daktari dhamana wa Hospitali hiyo Othman Maalim alisema  hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa 150, huku vitanda vinavyotumika ni 120 kutokana na
upungufu wa wafanyakazi.

Alisema hospitali inawafanyakazi 185, ikikabiliwa na upungufu wa madawa wanazoagiza kutoka bohari kuu ya dawa Zanzibar, pamoja na baadhi ya Vifaa Tiba ambavyo hunuliwa kutoka katika Mfuko wa Wizara ya Afya
Pemba.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua eneo la Bandari ya Shumba Mjini lililopendekezwa kujengwa Bandari rasmi katika Mkoa wa Kaskazini Pemba. Mkurugenzi wa Huduma za Bandari Pemba Kepteni Makame Hassan Ameir alimueleza Balozi Seif kwamba kina cha maji katika eneo hilo kinafikia
Mita 20 hadi 30 ikilinganishwa na maeneo mengine ya Kisiwa cha Pemba hali inayoifanya kuweza kukidhi kiwango kinachohitajika.

Kepteni Makame alisema wakati vikao vya Viongozi wa Taasisi zinazosimamia sekta ya Bahari katika Pwani ya Mwambao wa Tanzania kuanzia Mkoa wa Mtwara, Zanzibar, Bagamoyo hadi Tanga vikiendelea juhudi zinafanywa kupitia Wizara ya Ardhi kulipima eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.