Habari za Punde

Katibu tawala Micheweini awajia juu viongozi wa vyama vya wafanyakazi

Na.Haji Nassor. Pemba.
KATIBU tawala wilaya ya Micheweni Pemba, Hassan Abdalla Rashid, amesema lazima viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini, wawe makini kufuatilia na kulilia haki za wafanyakazi, badala ya kuvifanya vyama hivyo kama mtaji wa kujipatia fedha kwa maslahi yao binafsi.

Alisema, vyama hivyo havikuanzishwa kwa ajili ya wachache kwenda kwenye mikutano, makongamano na semina kujipatia fedha, bali ni kujenga misingi imara na endelevu katika kuwatetea wanachama wao.

Katibu tawala huyo, alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya haki za binadamu, kwa wanachama wa vyama vya wafanyakazi, yalioandaliwa na kufanyika Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba.

Alieleza kuwa, wanfanyakazi hasa kwenye sekta binafsi, wamekuwa wakikoseshwa haki zao na wakati mwengine kufanya kazi zao bila ya kuagalia usalama wao, hivyo ni nafasi kwa viongozi hao kuyafuatilia hayo.

“Mimi naamini vyama vya wafanyakazi kama vikiwa makini kweli kweli na kufanya kazi zao kwa kuangalia misingi ya haki na sheria zinavyotaka, basi vitawasaidia sana wanachama wao”,alieleza.

Katika hatua nyengine, Katibu tawala huyo wa Wilaya ya Micheweni amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo, kuifanyia kazi elimu watakayopewa, ili wapunguze manung’uniko miongoni mwao.

Mapema Mratibu wa mafunzo hayo Siti Habib Mohamed, alisema ZLSC, iliamua kuwapatia mafunzo hayo wanachama wa vyama vya wafanyakazi, ili kuwajengea uwelewa zaidi.

“Kituo chetu kimekuwa kikitoa mafunzo kwa makundi mbali mbali, lakini na wanachama wa vyama vya wafanyakazi nao tukaona umuhimu wa kukutanao nao”,alifafanua.

Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, ZLSC Fatma Khamis Hemed, alisema kituo kimekuwa kikihakikisha kila kundi ndani ya jamii, linapata uwelewa wa masuala ya kisheria, ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.

Wakichangia mada hizo, washiriki hao walisema bado vyama vya wafanyakazi havijatekeleza wajibu wake ipasavyo kwa wananchama wake, ikiwemo kuwaelimisha.

Makame Suleiman alisema bado vyama hivyo vinahitaji ushawishi wa hali ya juu, ili kwa wale ambao hawajajiunga waone umuhimu wake na faida.

Nae Marzuku Khamis Sharif, alisema lazima hata kwa wananchama wenyewe waone umuhimu wa kujisomea sheria mbali mbali kwa faida yao.


Katika mafunzo hayo mada sita zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na ufafanuzi wa sheria ya mahusiano kazini no 1 ya mwaka 2005, sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF no 2 ya mwaka 2005, sheria ya fidia, sheria ya afya na usalama kazini no 8 ya mwaka 2005 na sheria ya uajiri no 11 ya mwaka 2005.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.