Habari za Punde

Wazazi watolewa hofu kambi ya wanafunzi skuli ya Mauwani

Na.Haji Nassor. Pemba.
WAZAZI na walezi wenye watoto wao skuli ya sekondari ya Mauwani Kiwani wilaya ya Mkoani Pemba, walioweka kambi kwa jili ya matayarisho ya mitihani, wametolewa hofu na uongozi wa skuli hiyo, na kusema lengo ni kuongeza ufaulu na sio vyenginevyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi skulini hapo, Kaimu Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Mussa Mohamed Abass, alisema wazazi waondowe wasiwasi juu ya kambi hiyo, kwani uongozi wa skuli, una lengo zuri na sio vyengine kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

Alisema, anachokiomba kwa wazazi na walezi hao, ni kuendelea kushirikiana na uongozi wa skuli hiyo na kamati yake, ikiwa ni pamoja na kufikisha michango yao waliokubaliana kwa wakati.

Kaimu Mwalimu Mkuu huyo, alisema baada ya kumaliza kikao na wazazi hao, na kukubaliana kuweka kambi, sasa wasiwe tayari kusikiliza maneno ya nje yasio kuwa na hoja, na badala yake wawaamini juu hilo.

“Wazazi wasikubali kupotoshwa juu ya uwepo wa kambi hii, ambayo sio mara ya kwanza, na badala yake wao waendelee kutoa michango na hata wakati mwengine watutembelea kutushauri, kutukumbusha na kutupa nguvu”,alifafanua Mwalimu mkuu huyo.

Katika hatua nyengine Kaimu huyo, aliwataka wanafunzi hao wanaojitayarisha na mitihani ya taifa, kufahamu malengo ya wao kuwepo kwenye kambi hiyo, ambayo hasa inawategenezea mazingira yao mema ya baadae.

“Niwatake wananfunzi waelewa kuwa, wazazi na walezi wanatumia nguvu na fedha nyingi kuidumisha kambi hiyo, sasa wasikubali kucheza cheza, maana mitihani imekaribia, na hata waalimu wenyewe wa baadhi ya masomo ya sayansi hatuna”, alifafanua.

Baadhi ya wanafunzi wasiopenda majina yao yachapishwe, walisema kambi hiyo ni muhimu na hasa kama yengeanza tokea mwanzoni mwa mwaka huu wa mitihani ya taifa.

Walisema, linalohitaji kwa wizara husika ni kuhakikisha inawapatia waalimu wa masomo ya sayansi, ambapo kwa sasa mwalimu wao tegemeo anadaharura ya kibinadamu.

Hata hivyo wanafunzi hao wa madarasa ya kumi na kumi na mbili, wameahidi kuongeza idadi ya ufuulu, ikilinganishwa na miaka mengine, hasa kwa moyo na ari walionao wa kusoma kwa ushindani.

Skuli hiyo ya Mauwani iliopo Kiwani wilaya ya Mkoani, ambayo ilioasisiwa mwaka 2013, kwa mwaka huo ilitokezea ya mwisho kwa Zanzibar kwenye mitihani ya darasa la kumi (FII).

Ingawa mwaka 2015 ilishika nafasi ya pili kwa Zanzibar kwa kupasisisha wanafunzi wote waliokubali kukaa kambini, ambapo kwa mwaka huo walipata wanafunzi 19 waliokosa vyeti wa darasa la kumi na mbili na mwaka 2016 walipunguza na kuwa na wanafunzi wanne pekee.


Wilaya ya Mkoani kwa sasa imeanzisha utaratibu wa kambi nne kuu za pamoja ikiwa ni Kengeja ufundi, Maendeleo Mngwachani, Mauwani na skuli ya Juma Khamis Pindua, kwa kuungana skuli tano tano na kuwatumia vijana waliomaliza, kuendesha kambi hizo na waalimu wengine.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.