Habari za Punde

Wanaoyatunza Mashamba ya Serikali Watoa Neno Pemba

Na.Haji Nassor. Pemba.
WANANCHI wanayoyatunza mashamba ya  mikarafuu ya serikali, wamependekeza kuwepo kwa utaratibu wa kuyafanyia tathimini mashamba hayo kila msimu wa uvunaji, na kisha kuwaelezwa wao, iwapo wanauwezo wa kuyakodi, kabla ya kuitisha minda ya hadhara kama ilivyo sasa.

Walisema kuitisha minada hiyo, huwa ni kikwazo kwao kutokana na ukosefu wa fedha za kukodia mashamba hayo, ambapo kama wakiyafanyai tathimini na kisha kukodisha kwa bei isiokuwa ya mnada, wanaweza kuyamudu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati taifauti, wananchi hao wanaoyatunza mashamba hayo walisema, lazima kwa serikali iwape kipaumbele cha pekee kwenye kuyakodi mashamba na sio kupitia minada ya hadhara kama ilivyo sasa.

Walieleza kuwa, wengi wao wanaoyatunza mashamba hayo, ni wanyonge kifedha na hutumia fedha nyingi kwa kuyafanyia usafi na wengine kupanda mikarafuu mipya, hivyo lazima kuwe na fungu la huruma, wakati wa azoezi la uvunaji unapofika.

Mmoja kati wananchi hao anaelitunza shamba lililokuwa la Suleiman Riyami lililopo shehia ya Chonga, Kombo Abdalla Kombo, alisema yeye amepanda mikarafuu mipya 100 kwenye shamba hilo, ambalo amekabidhiwa zaidi ya miaka 15 sasa.

Kombo, alieleza kuwa pamoja na kupanda mikarafuu hiyo, pia ametumia shilingi 600,000 kulifanyia usafi shamba hilo lenye mikarafuu mikongwe isiozidi 80.

“Mimi nimetumia gharama kwanza kulitunza, pia kupanda mengine na nimeweka watu hapa shamba walilinde, sasa ukiniambia nitoe shilingi milioni 18.1 ili nilikodi kama mnada ulivyofika ni kunionea”,alifafanua.

Nae Is-mail Haji Chuma wa Mizingani alisema kwa vile mashamba hayo, serikali ilikaa kwa muda mrefu bila ya kuyafuatilia, lazima wawaangalie kwa jicho la huruma hasa kufuatia msimu huu kuwa mkubwa.

“Sio vyema sisi tunaoyatunza mashamba haya, kutuunganisha kwenye minada wa jumla jumla, ingependeza kwanza yakafanyia tathimini na wizara husika na kisha tukagepewa bei na tukishindwa ikiitishwa minada”,alishauri.

Kwa upande wake Mmanga Makame Mmanga wa Wete, alisema kinyume chake cha kuwaweka kwenye minada, inaweza kusababisha manun’guniko kwao na hatimae mashamba hayo, kukosa washughulikiaji hapoa baadae.

Said Juma Ali akizungumza kwa niaba ya Afisa Mdhamini wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, alisema taratibu zinataka mashamba hayo kabla ya kukodishwa kuitishwa mnada wa hadhara na  kipaumbele kwa bei itakayofikiwa, huulizwa anaelitunza shamba na sio vyenginevyo.

Afisa Mdhamini huyo alisema, wanaoyatunza mashamba hayo iwe wamekubali kuyakodi wenyewe kwenye mnada huo wa hadhara au yamekodiwa na mtu mwengine, hupewa asilimi 40  ya bei iliofikiwa.

“Bei inayofikiwa kwenye mnada wa hadhara iwe anaelitunza kakubali yeye kulikodi au mtu mwengine, asilimia yake 40 kama kifuta jasho iko pale pale, lakini sio kuyakodisha siri siri”,alifafanua.

Wakuu wa wilaya za Mkoani na Chake chake wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema serikali haifanyia zoezi hilo kwa kumuonea mtu, bali ni kuhakikisha mali yale haishii kwenye mikono ya wachache.

“Zipo eka tatu tatu ambazo zilitolewa na rais wa kwanza wa Zanzibar au zile hati zilizotolewa na rais Aboud Jumbe Mwinyi, kwa walionazo, wala zoezi hili haliwagusi, lakini hati nyengine kwenye eka tatu haziotambuliki”,alisema Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman.

Nae Mkuu wa wilaya ya Chakechake Salama Mbarouk Khatib, alisema anaamini zoezi hilo, linaweza kuyaibua mashamba kadhaa ya serikali, yaliokuwa mikononi mwa wananchi kinyume na sheria.


Wakati zoezi la ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu ya serikali ukiendelea, tayari zaidi ya mashamba 580 yameshagundulika, ambayo mengi yao yalikuwa mikononi mwa wananchi kinyume na tataribu, huku wilaya ya Mkoani ikigundua zaidi ya 80 pekee.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.