Habari za Punde

Mbunge wa Kiwengwa akabidhi vifaa vya Sh Mil 37 jimboni

NA IS-HAKA  OMAR-ZANZIBAR.

JUMLA ya Pikipiki 14 aina ya Vespa zenye thamani  ya shilingi milioni 37 zimetolewa na Mbunge wa jimbo la Kiwengwa, Khamis Mtumwa kwa Makatibu wa Matawi ya CCM ya jimbo hilo.

Akizungumza katika hafla ya  kukabidhi vitendea kazi hivyo huko katika uwanja wa mpira wa kwa Gube, mbunge huyo  alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.

Alieleza kwamba lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuwarahisishia huduma za usafiri  watendaji hao ambao muda mwingi wanakuwa na majukumu mbali mbali yanayohitaji usafiri wa haraka ili yaweze kutekelezwa kwa wakati.

Aliahidi kuwa hiyo ni sehemu tu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jimbo hivyo ataendelea kutatua kero mbali mbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

“ Nitaendelea kumarisha huduma mbali mbali za kijamiii kadri mwenyezi mungu atakavyonijaalia, wito wangu kwenu ni kwamba miradi ambayo kwa sasa naitekeleza katika jimbo hili mnatakiwa kuitunza ili iweze kuwanufaisha watu wote.”, alisisitiza Khamis.

Akizungumza  Naibu Katibu  Mkuu wa  CCM Zanzibar  Dkt. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’  mara baada ya kukabidhi  Pikipiki  hizo  kwa  watendaji  hao  aliwataka viongozi wa majimbo ya chama hicho kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi.

Alisema kwa sasa viongozi wanatakiwa kuongeza kasi ya  utekelezaji wa ilani ya  Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa vitendo ili wananchi  waone maendeleo yanayofanywa na viongozi wao.

Alisisitiza kuwa ni lazima viongozi wa majimbo waende na wakati Kwa kutangaza na kutoa taarifa za uhakika juu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM , hatua itakayosaidia kujenga imani za wananchi waliowachagua katika uchaguzi mkuu uliopita.

“ Naendelea kuwakumbusha baadhi ya wabunge, wawakilishi na madiwani ambao bado utekelezaji wao wa Ilani ya Chama chetu unasuasua katika majimbo yao kuwa waanze kurudi kwa wananchi kutekeleza yale waliyowaahidi kabla ya uchaguzi mkuu ujao”, alisema Dkt. Mabodi.

Nao baadhi ya makatibu mbali mbali waliokabidhiwa vifaa hivyo wameahidi kuvitumia vizuri kwa lengo la kuimarisha shughuli mbali mbali za chama hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.