Habari za Punde

Taifa yaendeleza uteja kwa Jang'ombe Boys yalala 2-0

Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.

Timu ya Jang'ombe boys imeendeleza wimbi lake la ushindi mbele ya kaka zao Taifa ya Jang'ombe baada ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu soka ya Zanzibar uliopigwa jana jioni katika uwanja wa Amaan.

Mabao ya Boys yamefungwa na Hafidh Barik (Fii) dakika ya 6 na Juma Ali (Mess) dakika ya 66.

Kwa matokeo hayo rikodi bado inawapendelea Boys ambapo timu hizo zimeshakutana mara 8 katika historia huku mara 5 Boys akishinda, mara 2 kafungwa na mara 1 sare ambapo Dabi hiyo ya Jang’ombe kati ya Taifa ya Jang’ombe na Jang’ombe Boys ndio dabi inayoongoza kukutana mara nyingi msimu mmoja kuliko dabi zote Dunia nzima ambapo dabi hiyo imekutana mara 6 hii haijawahi kutokea Dabi yoyote Duniani kukutana mara 6 ndani ya msimu mmoja.

Ndani ya msimu huu wa mwaka 2016-2017 ambao kwa Zanzibar bado unaendelea dabi hiyo walikutana Novemba 19, 2016 katika Bonanza la Coconut FM ambapo matokeo Taifa 2-0 Boys huku mabao ya Taifa yalifungwa na Mkongo Baraka Ushindi na Mkenya Mohd Said “Mess.

Disemba 10, 2016 walikutana tena kwenye Ligi kuu soka ya Zanzibar Mzunguko wa kwanza na mataokeo Taifa 2-2 Boys ambapo mabao ya Taifa siku hiyo alifunga Omar Yussuf Chande dakika 9 na Abdallah Mudhihir (Mido) dakika 60 wakati mabao ya Boys yote alifunga Khamis Mussa (Rais) dakika ya 45 na 53.

Disemba 30, 2016 pia walikutana tena kwenye Kombe la Mapinduzi 2017 na matokeo Taifa 1-0 Boys kwa bao pekee lililofungwa na Hassan Seif “Banda”.

Aprli 25, 2017 walikutana tena kwenye ligi kuu soka ya Zanzibar Mzunguko wa pili na matokeo Taifa 0-1 Boys kwa bao pekee limefungwa na Khamis Mussa “Rais”.

Mei 14, 2017 walikutana tena kwenye ligi kuu soka ya Zanzibar hatua ya 8 bora Mzunguko wa kwanza na matokeo Taifa 0-3 Boys ambapo mabao ya Boys yalifungwa na Khamis Mussa “Rais”, Khatib Ng’ombe alijifunga mwenyewe na Juma Mess la tatu.

Na jana Jumapili ya July 30, 2017 kwenye mzunguko wa pili ligi kuu soka ya Zanzibar hatua ya 8 bora wamekutana mchezo wao wa sita katika msimu mmoja ambapo Boys alishinda 2-0 kwa mabao ya Hafidh Barik (Fii) dakika ya 6 na Juma Ali (Mess) dakika ya 66.

Msimu wa Mwaka 2012-2013 Boys aliwafunga Taifa mara mbili wakati huo timu zote zipo ligi Daraja la Pili Wilaya ya Mjini baada ya Boys kushinda 2-1 kwenye ligi hiyo, na mchezo mwengine Kombe la Waamuzi Boys tena kupata ushindi baada kushinda kwa penalti 5-4 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare ya 0-0 michezo yote hiyo ilisukumwa katika Uwanja wa Mao Tsi Tung.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.