Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk. Shein, Azungumza na Mkurugenzi Mkuu wa FAO Ikulu Zanzibar.j

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                              07.09.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo  leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dk. Jose Graziano da Silva, ambaye amefika Zanzibar kwa lengo la kuongeza mashirikiano baina ya Shirika hilo na Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa FAO ni miongoni mwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yalio na historia kubwa katika kuisaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo pamoja na mazao yanayohusiana na chakula.

Aliongeza kuwa FAO imeweza kutoa misaada mbali mbali ya kuendeleza sekta ya kilimo hapa Zanzibar na kumueleza Mkurugenzi Mkuu huyo jitihada za wananchi wa Zanzibar katika kuliendeleza zao la mwani na kusisitiza haja kwa Shirika hilo kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha kilimo hicho kinawanufaisha wakulima wake.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi za pekee kwa Shirika hilo kwa ushirikiano wake mkubwa unaotoa katika kupambana na athari za kilimo zinazosababishwa na wadudu waharibifu wa matunda ikiwa ni pamoja na utafiti wa maradhi ya zao la mwani.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo na uvuvi pamoja na azma ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo malighafi zake zitatokana na rasiliamali za sekta hizo ili kwa pamoja ziweze kuwa na mchango mkubwa katika soko la ajira hasa kwa vijana.


Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya  Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya kilimo, uvuvi na uvugaji ili sekta hizo ziweze kuleta tija na kutoa ajira hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya wananchi wa Zanzibar wanajihusisha katika sekta hizo.

Hivyo, alimshauri Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa katika ziara yake ijayo ni vyema akatembelea kisiwani Pemba kwa lengo la kuangalia juhudi za wananchi wa kisiwa hicho katika kuendeleza sekta ya uvuvi na ufugaji hasa ufugaji wa samaki.

Sambamba na  hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Kilimo na Chakula Duniani pamoja na kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wake Dk. Graziano da Silva kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kusaidia katika kuhakikisha sekta ya kilimo inazidi kuimarika.

Nae Dk. Graziano da Silva alimuhakikishia Dk. Shein pamoja na kuihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono na kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya Kilimo na kulipokea wazo la Rais Dk. Shein la kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wa kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo Kizimbani.

Mkurugenzi Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa uongozi wa Wizara husika ya Kilimo pamoja na ziara aliyofanya katika maeneo mbali mbali yakiwemo mashamba ya viungo na maeneo ya utafiti Kizimbani.

Hivyo, alieleza kuwa baada ya ziara yake hiyo ameweza kugundua utajiri mkubwa ulionao Zanzibar wa mazao ya viungo ambayo Shirika lake la FAO litaangalia namna ya kusaidia ili bidhaa hizo za viungo ziweze kutengenezewa dawa za tiba asilia.

Dk. Graziano da Silva alisema kuwa umefika wakati wa kuelekeza nguvu zote katika mageuzi ya kilimo hatua ambayo itaimarisha zaidi uzalishaji wa mazao ambayo yataimarisha sekta ya biashara sambamba na sekta ya viwanda hapa nchini.

Dk. Graziano da Silva alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Zanzibar kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano mwema uliopelekea mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo hapa nchini kwa kuimarisha uhakika wa chakula na maendeleo ya ya sekta hiyo.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO aliipongeza Zanzibar kwa kuendeleza na kusimamia vyema miradi yote inayoendeshwa na Shirika hilo na kusisitiza kuwa limefarajika na juhudi hizo na itaendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo, alimueleza Dk. Shein juhudi zinazochukuliwa na Shirika hilo la FAO katika kuhakikisha usalama wa chakula unakuwa ni ajenda muhimu kwa nchi za bara la Afrika kwani ni jukumu moja wapo la Shirika hilo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.