Habari za Punde

Kliniki ya Methadone Zanzibar yapatiwa vifaa vya kuchunguza wateja wao

 Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la dawa za Kulevya na Uhalifu  (UNODC) Bi. Immaculate Nyoni  akimkabidhi boksi lenye vifaa vya kupimia mkojo watumiaji dawa ya Methadon ambao wanatumia  aina nyengine ya dawa kinyume na taratibu katika hafla iliyofanyika Kliniki Methadone Kidongochekundu.
 Rais wa watumiaji dawa ya Methadon Zanzibar Hilal Nassor akizungumza na wandishi wa habari baada ya kukabidhiwa vifaa vya kuwatambua watumiaji wa tiba ya Methadone na baadae kutumia dawa aina nyengine.
Baadhi ya watumiaji dawa za Methadone wakisubiri kupatiwa huduma katika Kliniki yao iliyopo Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo- Chekundu Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo    
       
Wagonjwa wanaotumia dawa aina ya Methadone kama tiba baada ya kuathirika kutokana na dawa za kulevya na wanaoutumia aina nyengine ya dawa  kwa njia za siri wamepatiwa muarubaini baada ya kupatikana vifaa maalumu vya kumgundua mtumiaji kwa kumpima mkojo.

Vifaa hivyo vinavyojulikana kwa jina la DOAKIT vimetolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC).

Mratibu wa Mradi wa Taifa wa kupambana na HIV/AIDS kwa wafungwa, Immaculate Nyoni ambae ni afisa wa UNODC Tanzania amemkabidhi vifaa hivyo Mratibu wa huduma za ukimwi kwa watu wa makundi maalum Zanzibar Dkt. Shaaban Hassan katika hafla iliyofanyika Kliniki ya Methadone iliopo ndani ya hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo- chekundu.

Immaculate alisema UNODC itaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia tiba sahihi wagonjwa walioathirika na dawa za kulevya.

Alisema kwa kuanzia wameleta DOAKIT 1500 ambazo zinaweza kutumika kwa kipindi cha miezi mitatu kwa mujibu wa idadi ya wagonjwa wanaotumia Methadone waliosajiliwa katika kliniki hiyo.

Daktari dhamana wa hospitali ya Kidogochekundu Dkt. Khamis Othman alilishukuru shirika la UNODC kwa kuwapatia msaada huo ambao kwa kipindi cha mwaka mmoja walikuwa na upungufu mkubwa na kupelekea baadhi ya wagonjwa kutumia aina nyengine ya dawa bila kujulikana.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za kutumia tiba ya Methadone mgonjwa hatakiwi kutumia aina nyengine ya dawa za kulevya na akifanya hivyo hupata madhara makubwa kwa kuongeza kiwango cha dawa mwilini.

Alisema DOAKIT ni viifaa vyenye uwezo wa kugundua aina sita ya dawa za kulevya kwa kuchunguza mkojo wa mtumiaji na vinaweza kutumika katika maeneo mbali mbali kuwachunguza watumiaji wa dawa hizo.

Dkt. Khamis alieleza kuwa Kliniki ya Methadone ya Kidongochekundu ilianzishwa mwaka 2015 na imesajili wagonjwa 434 ambao wanapatiwa  tiba kamili na imekuwa mkombozi wa vijana wengi waliokubali kujiunga.

Alisema kazi ya Methadone ni kusaidia kuondosha hamu ya kutumia Heroine na dawa nyengine za kulevya hatimae mtumiaji huacha kidogo kidogo kutumia dawa hizo.

Hata hivyo amekiri kuwa bado wanakabiliwa na changamoto kubwa kwani baadhi ya wagonjwa wanaotumia Methadone hukosekana baadhi ya siku na wanatumia dawa nyengine za kulevya kwa siri.

Wagonjwa wanaotumia Methadone wamekiri kuwa inawasaidia  kujitambua na imewarejesha katika mfumo bora wa maisha na wanaaminika ndani ya jamii zao.

Amina Omar mkaazi wa Jangombe, alietumia dawa za kulevya kwa miaka 25, alisema wakati anatumia dawa hizo alikuwa hajitambui na alidhoofu kufikia uzito wa chini ya kilo 40 na baada ya kutumia Methadone hivi sasa uzito wake umefikia kilo 80.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.