Habari za Punde

Bodi ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wameangamiza Tani tisa za Dawa za meno aina ya Aloe

  Wafanyakazi wa Bodi ya Wakala na Dawa Zanzibar  wakiteremsha dawa za msuaki tani tisa zilizoharibika katika jaa la kibele Wilaya ya Kati Unguja kwa ajili ya kuangamizwa
 Maboksi yaliyokuwa na dawa za msuaki zilizoharibika yakichomwa moto na wafanyakazi wa Bodi  ya Wakala na Dawa Zanzibar katika jaa la Kibele, Wilaya ya Kati Unguja.
 Gari aina ya kijiko likisaga dawa zilizoharibika ili kuziangamiza baada ya kuingia maji wakati wakusafirishwa katika jaa la Kibele Wilaya ya Kati Unguja.
Picha na Ramadhani Ali – Maelezo.

Na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.                          

Wafanyakazi kutoka Bodi ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wameangamiza Tani tisa za Dawa ya meno aina ya Aloe zilizoharibika katika jaa la Kibele Wilaya ya Kati Unguja

Dawa hizo ziliingizwa nchini na Kampuni ya Bacelona Interprises Limited zikiwa zimeharibika baada ya kontena lilikuwa na dawa hizo kuinga maji wakati wa kusafirishwa kuja Zanzibar .

Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Chakula Dawa Zanzibar Mwadini Ahmadi Mwadini alisema walibaini kuwa dawa hizo zimeharibika wakati wa kuzitoa bandarini na kumshauri mmiliki wa dawa hizo kuzirejesha zilikotoka au kuziangamiza na alikubali ziangamizwe ili kujiepusha na gharama nyengine.

Mwadini alisema Bodi inaendelea kufanya ukaguzi kwa bidhaa zinazoingizwa bandarini na  maduka mbali mbali ili kuhakikisha zinakuwa salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Aliwataka wafanyabiashara kuwa waangalifu wanapoagiza Bidhaa na kujenga ushirikiano wa karibu na Bodi yake kwa kutowa taarifa wanapoona bidhaa zao zinamashaka kuuzwa kutokana na kuharibika au kupitwa na muda wake wa matumizi.

Aidha aliwaomba wananchi wanaponunua bidhaa madukani  na kuzigundua kuwa hitilafu watowe taarifa katika Bodi ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa kwa usala wao.       

“Kama mukigundua kunafanyika udanganyifu kwa bidhaa mnazonunua kama kuharibika au kupitwa na wakati musisite kutoa taarifa kwetu, tupo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi.” alisema Mkaguzi Mkuu.  

Nae mtoa mzigo Bandarini aliesimamia kontena hilo Omar Kombo Sharif alisema mzigo huo uliingia Zanzibar mnamo mwezi wa nane na baada ya kubainika umeharibika walitoa taarifa kwa mmiliki na walikubaliana uzuiliwe kwa ajili ya kuuangamiza.

Wakati huo huo Mkuu wa Uchunguzi wa Chakula na Dawa Zanzibar Mohamed Shadhil alisema wamekamata Nyama ya ngombe kilo 180 iliyokuwa inasafirishwa kinyume na taratibu zilizowekwa na Bodi hiyo.

Alisema bidhaa hiyo imekamatwa wakati inasafirishwa kutoka machinjioni kwa kutumia Baskeli pamoja na vespa bila ya kuwa na kibali cha daktari na nikinyume cha utaratibu. Bidhaa za nyama zinatakiwa kusafirishwa kwa kutumia gari kwa ajili ya usalama wa watumiaji.

Nyama hiyo wameamua kuifukia baada ya kufanyika uchunguzi na kuwaita wamiliki ambao walikubali kuwa wamefanya kosa licha ya kulalamika kuwa utaratibu wa kusafiri bidhaa hiyo kwa kutumia baskeli na vespa umekuwapo kwa muda mrefu.

Mkuu huyo wa uchunguzi aliwataka wananchi wanaochinja nyama kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia vyombo vinavyotakiwa vyakuchukulia bidhaa hiyo ili kuepuka usumbufu na hasara katika biashara zao

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.