Habari za Punde

Mudathir Yahya asema waliomchagua kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba hawakukosea

Mudathir Yahya akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza dhidi ya Rwanda

 Na Abubakar Khatib Kisandu, Machakos Kenya.

Siku moja mara baada ya kutangazwa kuwa mchezaji Bora wa Mwezi Novemba, 2017 wa Ligi Kuu Soka ya Tanzania Bara msimu wa 2017/2018 Mudathir Yahya amesema amezipokea kwa furaha taarifa hizo kwani yeye alistahiki kuipata nafasi hiyo.

Mudathir amesema alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu kila siku ili Mwezi huo achaguliwe yeye kwani alionyesha kiwango cha hali ya juu kabisa.

“Namshukuru Mwezi Mungu kwa kunijaalia kuchaguliwa mimi kuwa mchezaji bora wa Mwezi, nilikuwa namuomba Mungu kila siku nikisali ili nichaguliwe mimi, namshkuru kocha wangu Hans pamoja na wachezaji wenzangu wote wa Singida United, na pia nilistahiki kuchaguliwa kwani nilicheza vizuri sana mwezi Novemba”. Alisema Mudathir.

Mudathir alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Beki Asante Kwasi wa Lipuli ya Iringa na Mshambuliaji Danny Usengimana pia wa Singida United, alioingia nao fainali ya kuwania nafasi hiyo.

Jopo la makocha na wachambuzi wa habari za michezo walipendekeza jina la Mudathir kutokana na mchango alioutoa kwa timu yake katika mechi tatu ambazo walicheza kwenye uwanja wa Namfua Singida ambazo zote timu yake ya Singida United iliibuka na ushindi.
Singida United ilitoka 0-0 na Yanga, iliifunga Mbeya City mabao 2-1 na pia iliifunga Lipuli bao 1-0, ambapo Mudathir anayecheza nafasi ya kiungo alicheza dakika zote 270 sawa na michezo mitatu na hakuwa na kadi yoyote.

Kwasasa Mudathir yupo Machakos nchini Kenya akiitumikia timu yake ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwenye Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup yanayoendelea nchini Kenya ambapo Heroes inaendelea kufanya vyema kwenye kundi lake A.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.