Habari za Punde

Dhoruba ya upepo na mvua yaathiri nyumba shehia ya Mbuyuni kisiwani Pemba

Na Salmin Juma, Pemba

FAMILIA tatu zenye watu 18 za shehia ya Mbuyuni Wilaya ya Mkoani Pemba, zinaendelea kuishi kwa ndugu, jamaa na majira, baada ya nyumba walizokuwa wakiishi, kuezuka mapaa na kushindwa kukalika, kutokana na dhoruba ya upepo ulioambana na mvua.

Upepo huo uliyoambatana na mvua za mwanzo za masika, ulitokea Machi 3, majira ya saa 10:00 alfajiri wakati familia hizo, zikiwa zimelala ndipo waliposikia kishindo na kushuhudia mapaa ya nyumba zao yakiezuka.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema,walisikia kishindo kikubwa kilichoambatana na upepo kilichokuwa kikisokota na kisha kuangusha migomba na kuhamia kwenye mapaa ya familia hizo.

Walisema upepo huo mkali ambao ulidumu wastani wa dakika moja kasorobo, uliezua mapaa ya familia tano, ingawa familia tatu ndio ambazo nyumba zao, walilazimika kuzihama kabisa.

Ali Hassan Bakar, alisema baada ya kishindo hicho kutulia, walishindwa waanzie kwa nani kumsaidia kuokota vitu kama bati na maguzo, kutokana na kila familia kati ya hizo tatu, kupata hasara inayofafana.

“Kwa kweli mimi nilikuwa chooni najitayarisha kwa ajili ya sala ya alfajiri, lakini ule upepo ulivyoaanza nilijua hata nyumba yangu imeshaelemewa na Mnazi kumbe mabati ya nyumba ya jirani,”alisema.

Nae Mwajuma Kassim, alisema baada ya tukio hilo hata yeye alilazimika kukimbia kitanda na kisha kumsaidia jirani yake kuhifadhi watoto wake.

Kwa upande wake Omar Himid Sultan, alisema wakati upepo huo unaza kuvuma alikuwa nje ya nyumba yake, na ulipochanganya aliogopa hata kutoka nje.

“Mimi nilikuwa nje nataka kwenda baharini, lakini baada ya kusikia upepo unavuna na kisha kuangusha migomba, nilirudi ndani, lakini kisha tukatoa msaada kwa wenzetu,”alieleza.

Mmoja kati ya waathirika hao, akizungumza kwa niaba ya wenzake Ameir Abdalla, alisema hayo ni mipango ya Muungu, ambapo aliwahukuru majirani kwa kutoa msaada wao wakati huo.

“Sisi twashukuru sana maana tumehifadhiwa na hata na mali zetu, na tunaomba misaada ili kurejesha utengenezaji wa nyumba zetu na kuhamia,”alisema.

Sheha wa shehia ya Mbuyuni Nassor Juma Kombo, alizitaja familia zilizokosa makaazi kabisa, kutokana na dhoruba hiyo ni ya Ameir Abdalla yenye waakazi 10, Fatma Juma Shoka watano na Hassan Issa Sultan yenye watu watatu.

Aidha sheha huyo, alizitaja familia za Asha Saleh yenye watu sita na Rashid Omar Faki yenye watu wanane kwamba, nazo nyumba zao zilipata athari ndogo, ingawa wenyewe hawakulazimika kuhama.

Katika hatua nyengine sheha huyo, aliwapongeza wananchi wake wa Mbuyuni kwa kuendelea kuonesha umoja na mshikamano kutokana na kutoa msaada mkubwa kwa wahanga hao.

Hata hivyo sheha huyo, alisema hadi juzi Machi 11 ilikua hakuna hata kiongozi mmoja aliewatembele waathirika hao, ambao kwa sasa wanaishi kwa ndugu na jamaa zao, na tayari taarifa hizo ameshazitoa kwa ngazi husika.

Awali Katib Tawala wilaya ya Mkoani Pemba, Miza Hassan Faki akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu hizi juzi alikuwa hajapata taarifa za tukio hilo.

Mwezi Mei mwaka 2017, Mkoa wa kusini Pemba, ulipata waathirika zaidi ya 186, ambao nyumba zao ziliharibika na hazitengenezeki na nyengine zilianguka kuta au kufanya nyufa kufutia mvua ilionyesha.

Aidha mwaka huo pia familia sita za shehia ya Changaweni wilaya ya Mkoani, zilikosa makaazi baada ya nyumba zao kukumbwa na dhoruba, pamoja na kuanguka kwa miti kama Mifenesi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.