Habari za Punde

Zanzibar yaadhimisha siku ya kinywa na meno duniani

 Dkt dhamana kanda ya Unguja Muhidini Abdalla akizungumza katika maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno Duniani maadhimisho yaliofanyika Wizara ya afya Mnazimmoja  Mjini Zanzibar.
  Waziri wa afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza naTimu ya wataalamu wa afya ya kinywa na meno kutoka nchi za Ulaya katika kilele cha maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno Duniani.

 Dkt.  Mkuu wa meno HIP2 Dr. Feroz Jafferji akizungumza katika kilele cha maadhimisho  ya  siku ya afya ya kinywa na meno Duniani yaliofanyika Wizara ya afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.


Waziri wa afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed katikati alievalia suti rangi ya krimu akipiga picha ya pamoja na timu ya madaktari bingwa kutoka nchi za Ulaya wakishirikiana na madaktari wazalendo  katika maadhimisho hayo.(Picha na Abdalla Omar – Maelezo Zanzibar)

Na Faki Mjaka-Maelezo

Imeelezwa kuwa mabadiliko ya tabia na ulaji yameongeza wimbi la maradhi ya kinywa na meno hapa nchini.

Hali hiyo huwaathiri watu wengi hasa watoto na kuongeza mzigo mkubwa wa matibabu kwa taifa.

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed ameyaeleza hayo katika kilele cha siku ya Afya ya Kinywa na Meno duniani iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazi mmoja mjini Zanzibar.

Amesema kutibu maradhi ya meno ni jambo la gharama kubwa na hivyo njia pekee ni kuweka msisitizo kwenye program za kinga ili kupunguza mzigo wa matibabu.

Hata hivyo Waziri Hamad amesema Serikali inajitahidi kuboresha huduma za afya kwa ujumla ikiwemo huduma za meno ili kila mwananchi afurahie huduma zitolewazo katika vituo vya afya.

Ametahadharisha kuwa ulaji wa mara kwa mara wa vitu vya sukari unaongeza kasi ya meno kutoboka.

“Meno yasiyotibiwa yako kwenye hatari ya kupotea kwa kufikia mahali kulazimika kung’olewa na mtu aking’olewa meno licha ya usumbufu anaoupata lakini haiba yake pia nayo hupotea”alisema Waziri Hamad

Amesema kung’olewa kwa meno kunapunguza ubora wa maisha na kuleta usumbufu mwingi katika maisha ya kila siku.

Aidha waziri huyo ameishukuru wadau wote ikiwemo Jumuiya ya HIPZ, wataalamu kutoka nchini Austria na Ujerumani kwa mchango wao katika huduma za afya ya meno na kuwaomba waendelee na juhudi zao kwa faida ya wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Daktari dhamana Muhidin Abdallah amesema maradhi ya kutoboka kwa meno na fizi yanaepukika kwa kudhibiti ulaji wa vitu vya sukari na kupiga mswaki kwa kutumia dawa ya meno.

Hata hivyo amesema licha ya juhudi zinazofanywa kuboresha matibabu bado Hospitali nyingi zinakabiliwa na changamoto katika uapatikanaji wa huduma za matibabu ya meno.

Dkt Muhidin amesema hali hiyo inachangiwa na upungufu mkubwa wa madaktari wa meno, vifaa tiba hali inayopelekea baadhi ya vituo vya matibabu kutokuwa na huduma za afya za meno.

Maadhimisho hayo pia yameenda sambamba na mafunzo ya kupiga mswaki, kugawa miswaki na Dawa kwa Wanafunzi wa skuli mbalimbali kutoka Jumuiya ya HIPZ.

Kwa upande wake Daktari mkuu wa meno HIPZ Dkt. Feroz Jaffarji amesema wananchi wengi wa Zanzibar wameanza kuwa na uelewa kwamba suluhu ya ugonjwa wa meno siyo kung’olewa badala yake wagonjwa wanatakiwa wafike katika vituo vya afya kupatiwa matibabu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.