Habari za Punde

BODI MPYA YA UTAFITI WA MASUALA YA AFYA ZANZIBAR (ZAHRI) YAZINDULIWA.

KATIBU wa Bodi ya Utafiti wa masuala ya Afya Zanzibar, Mayasa Ali Salum akiwakaribisha Wajumbe wa bodi hiyo waliohudhurika katika uzinduzi uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 KATIBU MKUU Wizara ya Afya Zanzibar Asha Abdulla akimkaribisha Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed Kuizundua Bodi ya Utafiti wa masuala ya Afya Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed akitoa hutuba yake ya uzinduzi wa Bodi ya Utafiti wa Masuala ya Afya Zanzibar katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi mmoja Mjini Zanzibar.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed akimkabidhi Vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Utafiti wa masuala ya Afya Zanzibar Saleh Mohd Jidawi kwenye uzinduzi uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed akimkabidhi Vitendea kazi Katibu wa Bodi hiyo Mayasa Ali Salum katika uzinduzi uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 MWENYEKITI wa Bodi ya Utafiti wa masuala ya Afya Zanzibar Saleh Mohd Jidawi akizungumza machache katika uzinduzi uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 MJUMBE wa Bodi ya Utafiti wa masuala ya Afya Zanzibar Habib A Sharif akitoa neno la shukran kwa washiriki wa uzinduzi wa Bodi hiyo iliyofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
WAJUMBE wa Bodi ya Utafiti wa masuala ya Afya Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar. Picha na Abdallah Omar-Maelezo Zanzibar
Na Faki Mjaka.Maelezo Zanzibar.
Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Afya Zanzibar imetakiwa kuifikishia jamii matokeo ya Tafiti zao hususan kwa Wanafunzi wa Skuli na Vyuo ambao ni wepesi zaidi wa kuyakubali na kuyafanyia kazi matokeo ya Tafiti hizo. 
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameyasema hayo alipozindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi hiyo huko katika Ukumbi wa Wizara ya Afya, Mnazi mmoja mjini Zanzibar
Amesema tafiti za Afya ni jambo muhimu kwa taifa na taasisi hiyo itakuwa na jukumu la kulinda afya za Wananchi hao.
Amefahamisha kuwa Taasisi hiyo itakuwa na majukumu tofauti ikiwemo kuisadia jamii kubadili mtazamo wake katika mambo mbalimbali ambapo Taasisi inaweza kuanzia kwa kujikita zaidi kwa Wanafunzi wa ngazi tofauti.
“Tutakapofanya tafiti tuhakikishe kuwa kipaumbele kinakuwa kwa wanafunzi wa Skuli na Vyuo ambao watakuwa mabalozi wazuri wa leo na kesho” alisema Waziri Hamad.
Amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana afya za wananchi wake na kutoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Shein kwa muono wake thabiti wa kuanzisha Taasisi hiyo.
Waziri Hamad amefahamisha kuwa Wizara yake inatambua umuhimu wa kuwepo kwa vifaa vya kisasa na vya kipekee katika maabara ya taasisi hiyo na kuahidi kufanikisha ipasavyo.
Aidha ameahidi kuwapatia vijana elimu endelevu na kuwajengea uwezo katika nyanja za kitafiti Zanzibar.
Ametoa wito kwa Bodi hiyo kujifunza kutoka Taasisi zingine za Kitafiti Tanzania na nje ya Tanzania ili kukuza uwezo wake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Abdulla amefahamisha kuwa maabara ya Taasisi hiyo itakuwa na kazi nyingi za kufanya katika uchunguzi wa magonjwa ya kibinadamu na pia itashiriki katika tafiti za uvumbuzi wa dawa mpya zinazotokana na mimea kwa kutumia utaalamu wa kisasa.
Amefahamisha kuwa tunaamini kuwa kuna mimea mingi ya dawa za asili Zanzibar ambazo zimetumika toka enzi na sasa wakati umefika wa kuzifuatilia kwa ukaribu ili kupata ufanisi na usalama wa dawa hizo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Saleh Mohd Jidawi amesema Taasisi ya Maswala ya Utafiti wa Afya Zanzibar ilianza rasmi Januari 2, 2018 ambapo kuundwa kwake kunatokana na “Legal Notice” No. 125 chini ya kifungu 53 cha Katiba ya Zanzibar.
 Akitaja majuku ya Taasisi hiyo Jidawi amesema ni pamoja na kuratibu na kukuza utafiti unaolenga kutafuta suluhu kwa matatizo ya magonjwa katika jamii ya Zanzibar.
Jukumu jingine ni kusimamia na kusajili tafiti zote za afya zinazofanyika Zanzibar na nje ya Zanzibar kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Taasisi itahusika pia na mahusiano na taasisi za kimataifa katika masuala yanayohusu tafiti za afya na kuwasaidia Wanasayansi wa kizanzibari kuingia katika mahusiano ya kimataifa ya tafiti za afya kwa faida za Wazanzibari.
Hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo wa Wizara ya afya.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.