STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.04.2018
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya Shirika la Ndege la Misri (Egyptair) ya
kuanzisha safari zake kati ya Misri na Zanzibar hatua ambayo itakuza uchumi na
kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Makamo wa Rais wa
Shirika la Ndege la Misri (Egyptair) Mohamed Alabbady, aliyefuatana na Balozi
wa Tanzania nchini Misri Meja Jenarali Issa Suleiman Nassor pamoja na Maafisa
wa Shirika hilo na kumueleza jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ilivyoipokea kwa mikono miwili azma hiyo.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
iko tayari kutoa ushirikiano wake mkubwa kwa Shirika hilo la ndege la Misri
(Egyptair), kama inavyoendelea kutoa kwa mashirikia mengine makubwa ambayo
tayari yanafanya safari zake na Zanzibar likiwemo Shrika la Ndege la Qatar,
Ethiopia, Kenya, Afrika Kusini, Uturuki, Oman, Izrail, Ukraine na Mashirikika
mengine kutoka nchi kadhaa duniani.
Aliongeza kuwa
kuanzishwa kwa safari za ndege kati ya Misri na Zanzibar pia, kutaimarisha sekta
ya utalii hapa Zanzibar, sekta ambayo imeleta mafanikio makubwa katika kukuza
uchumi wa nchi ambapo inachangia pato la taifa kwa asilimia 20 na asilimia 80
za fedha za kigeni.
Dk. Shein alieleza
kuwa mbali ya kuimarika kwa sekta ya utalii hapa Zanzibar pia, kuanza kwa
safari kwa Shirika hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya
biashara kati ya pande mbili hizo sambamba na kuwaweka karibu wananchi wa
Afrika Kaskazini na Afrika ya Mashariki.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza jinsi ya mashirika kadhaa ya ndege duniani ambayo yameonesha dalili za kutaka kuanza safari
zake hapa Zanzibar likiwemo Shirika la ndege la Abudhabi la Etihad na Shirika
la ndege la Arabia (Air Arabian) la Sharjah.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa hatua ya shirika hilo kuonesha azma yake hiyo
kutaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya
Zanzibar na Misri ambapo nchi hiyo iliweza kuiunga mkono Zanzibar katika sekta
za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, kilimo, habari na elimu.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alimueleza Makamo huyo wa Rais wa Shirika la Ndege la Misri
(Egyptair) juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuhakikisha huduma za uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid
Amani Karume zinaimarika ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la
abiria katika uwanja huo wa ndege.
Mapema, Makamo wa Rais
wa Shirika la Ndege la Misri (Egyptair) Mohamed Alabbady alimueleza Rais Dk.
Shein azma ya Shirika hilo ya kuanza safari zake za ndege kati ya Misri na
Zanzibar.
Makamo huyo wa Rais wa
Shirika la Ndege la Misri alimueleza Rais Dk. Shein kuwa tayari Shirika hilo
limeshatoa uwamuzi wake huo na limo katika mchakato wa mwisho katika
kuhakikisha safari hizo za ndege zinaanza haraka iwezekanavyo.
Alabbady alieleza kuwa
anaamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Misri na Zanzibar
utaimarika kwa kiasi kikubwa baada ya kuanza kwa safari za ndege za Shirika
hilo sambamba na kutoa fursa zaidi kwa wananchi wa pande mbili hizo kutembeleana.
Aidha, Makamo huyo wa
Rais wa Shirika la Ndege la Misri alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa kuanza
kwa safari za ndege za (Egyptair) kutaimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar
kutokana Zanzibar kuwa na vivutio vingi vinavyowavutia watalii ambavyo maeneo
mengine duniani havipo.
Pia, aliongeza kuwa
watalii kutoka nchini Misri nao pia, watapata fursa za kuja Zanzibar kiurahisi
baada ya kurahisishwa safari za ndege na Shirika hilo ambalo lina hamu kubwa ya
kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano zikiwemo
safari za ndege kupitia Shirika hilo kati ya pande mbili hizo zinaimarika.
Sambamba na hayo,
kiongozi huyo alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Wizara yake ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Ofisi ya Ubalozi
wa Tanzania nchini Misri kwa mashirikiano mazuri aliyoyapata hatua ambayo
imeweza kurahisisha kwa kiasi kikubwa azma ya Shirika hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment