Habari za Punde

Rais Dk Shein amtumia salamu za pongezi Rais wa Misri Abdel Fattah El Sisi kwa ushindi mkubwa kwenye uchaguzi


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                              23.04.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi kwa ushindi  mkubwa alioupata kufuatia uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 March mwaka huu.

Katika salamu hizo, Rais Dk. Shein alimpongeza Rais Abdel Fattah El- Sisi kwa ushindi wake  mkubwa wa kura milioni 21 sawa na asilimia 97.08 ya kura zote na hivyo kupata ridhaa ya kuongoza tena nchi hiyo kwa muhula wa pili, ushindi ambao umeonesha wananchi wa Misri jinsi walivyofarajika na uongozi wa Rais El-Sisi.

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Misri wameweza kuishuhudia nchi yao ikiendelea kupata maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Rais El-Sisi katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi wake baada ya kuingia madarani mnamo mwaka 2014.

Aidha, Dk. Shein alieleza katika salamu hizo kuwa ushindi wake huo mkubwa itakuwa ni njia moja wapo muhimu ya kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Misri.

Rais Dk. Shein alimuhakikishia Rais Abdel Fattah El-Sisi kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Misri sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa pande mbili hizo.

Pia, Rais Dk. Shein alimtakia uongozi mwema kiongozi huyo pamoja na kuendeleza maendeleo endelevu yaliopatikana nchini mwake huku akimtakia afya njema sambamba na kuendelea kuimarisha amani na utulivu nchini humo kwa manufaa ya nchi hiyo na wananchi wake.

Rais Abdel Fattah El-Sisi mwenye umri wa miaka 63 alichaguliwa tena kuwa Rais wa Misri baada ya kuibuka na ushindi huo mkubwa ambapo alimshinda mpinzani wake Moussa Mustapha Moussa kutoka chama cha upinzani cha El Ghad ambaye baada ya matokeo hayo mpinzani wake huyo alieleza jinsi alivyoridhishwa na matokeo ya uchaguzi na hatimae alimpongeza Rais El-Sisi kwa ushindi wake huo mkubwa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.