Habari za Punde

China Yaipatia Tanzania Msaada wa Bilioni 146, Kujenga Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Usafirishaji

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Wang Ke wakitia saini mkataba wa msaada wa kifedha ambapo serikali ya China itaisaidia Tanzania jumla ya shilingi Bilioni 146.47  kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji pamoja na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard gauge. Hafla hii fupi imefanyika Ofisi za Hazina jijini Dar es salaam leo  Jumamosi Mei 19, 2018 ..
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. wang Ke wakibadilishana mikataba baada ya kuitia saini makubaliano ambapo serikali ya China itaisaidia Tanzania jumla ya  shilingi Bilioni 146.47  kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji pamoja na  upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard gauge. Hafla hii fupi imefanyika Ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam leo
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Wang Ke baada ya wawili hao kutia saini kwa niaba ya nchi zao wa mkataba wa msaada wa kifedha ambapo serikali ya China itaisaidia Tanzania jumla ya shilingi Bilioni 146.47 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji  pamoja na  upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard gauge. Hafla hii fupi imefanyika Ofisi za Hazina jijini Dar es salaam leo  Jumamosi Mei 19, 2018. Picha na IKULU.

Na Benny  Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imetiliana saini na Serikali ya China mkataba wa msaada wa kiasi cha Shilingi Bilioni 146.47. Mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James na Balozi wa China nchiniWang Ke  Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo Katibu Mkuu alisema kuwa fedha hizo ni msaada na siyo mkopo na zitatumika katika miradi miwili ya miundombinu. Mradi wa kwanza ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) ambacho kitajengwa Mabibo Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 62 sawa na takriban Shilingi bilioni 138.3.
Mradi wa pili ni kwa ajili ya kusaidia upembuzi yakinifu na upembuzi sanifu wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ambapo kiasi cha Sh. bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili hiyo.
Bw. Doto James alisema kwa sasa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa umeanza kwa awamu mbili ambazo moja ni kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, na kuanzia Morogoro hadi Makutopora-Dodoma, upembuzi yakinifu utakaofanywa na Serikali ya China ni kwa maeneo mengine ya ujenzi wa Reli hiyo kuanzia Dodoma, Tabora hadi Mwanza na Kuanzia Kaliua hadi Kigoma.
"China imetusaidia miradi mingi ikiwemo mradi wa maji Chalinze, Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Taifa, Mradi wa teknolojia za Kilimo mkoani Morogoro, Kituo cha upasuaji wa moyo na mafunzo, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Nyerere pamoja na misaada ya dawa na vifaa tiba" alieleza Bw. James
Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, Alisema kuwa China inategemea kuona kuwa msaada huo utasaidia kuimarisha maendeleo na kuisaidia Tanzania kupata maendeleo haraka.
Aidha alisema China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo itawasaidia Watanzania na kuendeleza urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Balozi Wang Ke, amesema Pia Serikali ya China na Tanzania zinaendelea majadiliano kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, na kuongeza kuwa majadiliano hayo yatakapokamilika nchi yake itasaidia ujenzi wa bandari hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Taifa (NIT) Prof. Zacharia Mganilwa ameishukuru Serikali ya China kwa msaada huo na kusema kuwa msaada huo utaisaidia chuo hicho kuweza kutoa wataalamu wa kutosha kuweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo sekta ya anga.
Amebainisha kuwa Chuo hicho Kikuu kitatoa mafunzo kwenye fani muhimu na zinazohitajika ikiwemo ufundi wa reli, masuala ya anga na sekta nyingine mtambuka kwa kutoa wataalamu waliobobea watakao changia kufanikisha azma ya Serikali ya uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania-TRC, Bw. Focus Msasani ameeleza kuwa msaada huo wa shilingi bilioni 3.22, utasaidia kuipunguzi serikali gharama ilizokuwa izitumie kwa kazi hiyo kenye mradi mkubwa wa kihistoria wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.