OFISA
Mkuu wa Idara ya Makumbusho Abdalla Magofu (aliyeshika mwamvuli), akitoa
maelezo kwa ujumbe kutoka serikali ya Oman juu ya hali ya jengo la Ngome Kongwe
lililoko Forodhani mjini Zanzibar. Kulia kwa ofisa huyo ni Katibu Mkuu wa
Wizara ya Urithi na Utamaduni nchini Oman, Salum Mohammed Mahruki.
MSHAURI
Elekezi na mtaalamu wa uhifadhi majengo kutoka Wizara ya Urithi na Utamaduni
nchini Oman Dk. Enrico d’Errico (kushoto), akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa
wizara hiyo Salum Mohammed Mahruki na wajumbe wengine, walipolitembelea jengo
la Beit El Ajaib mjini Zanzibar, ambalo serikali ya Oman inakusudia kulifanyia
matengenezo makubwa.
MKURUGENZI
wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe Zanzibar Issa Sariboko
Makarani, Katibu Mkuu wa Urithi na Utamaduni wa Oman, watendaji wakuu wa Wizara
ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, wakiliangalia kwa nje jengo la
Makumbusho ya Kasri Forodhani mjini Unguja, walipofanya ziara kukagua majengo
ya kihistoria yanayohitaji kufanyiwa matengenezo.
Na
Salum Vuai, WHUMK
MAANDALIZI
ya matengenezo ya jengo la Beit Al Ajaib lililoko Forodhani mjini Zanzibar
yameanza kufuatia ziara ya ujumbe kutoka Wizara ya Urithi na Utamaduni ya
serikali ya Oman.
Ujumbe
huo unaoongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Salum Mohammed Mahruki, uliwasili
nchini jana Mei 11, na leo ulitembelea jengo hilo kujionea hali halisi ya
uchakavu uliosababisha lisite kutumika kama kivutio cha utalii kwa zaidi ya
miaka mitano sasa.
Msafara
wa timu hiyo pia umemjumuisha mshauri mwelekezi ambaye ni mtaalamu wa uhifadhi
majengo Dk. Enrico d’Errico, ambaye
amekuja mahsusi kushauri njia bora ya kulitengeneza jengo hilo na mengine ya
kihistoria nchini.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo iliyowashirikisha watendaji wakuu wa Wizara ya Habari,
Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Urithi na Utamaduni
ya Oman Salum Mohammed Mahruki, aliomba jengo hilo lisafishwe haraka, wakati
wataalamu wakifanya tathmini ya kina ili kujua ukubwa wa kazi hiyo.
“Kwa
namna tulivyoliona jengo hili, ni lazima kazi ya kulitengeneza ianze haraka
iwezekanavyo, vyenginevyo tutazidi kuchelewa kwani tayari muda mwingi umepotea
tangu lilipopata hitilafu,” alisisitiza.
Alifahamisha
kuwa, sura ya Mji Mkongwe wa Zanzibar inaongezewa haiba na kuwepo kwa jengo
hilo, ambalo kila mtalii anayefika anastaajabishwa na kuvutiwa na utaalamu
pamoja na malighafi zilizotumika kulisimamisha tangu mwaka 1883.
Aliongeza
kuwa, serikali ya Oman chini ya uongozi wa Sultan Qaboos bin Said, na kwa
mahaba aliyonayo kwa Zanzibar na watu wake, imedhamiria kwa dhati kusaidia kwa
asilimia 100 ujenzi wa jengo hilo na kulifanya liwe la kisasa zaidi bila
kuathiri taswira yake ya kale.
Aliomba
ushirikiano wanaoupata kutoka serikalini na wananchi wa Zanzibar uendelee ili
kuifanya kazi hiyo iwe nyepesi ingawa inaonekana kuwa ngumu kutokana na sanaa
ya ujenzi wake.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa
Zanzibar Issa Sariboko Makarani, mpango wa kulifanyia matengenezo jengo hilo
umepata baraka zote kutoka Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambako Mji Mkongwe wa
Zanzibar umeorodheshwa miongoni mwa miji ya urithi wa kimataifa.
Alisema
ukaguzi wa jengo hilo na mengine matatu waliyoyatembelea, ni sehemu ya
makubaliano ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Oman yaliyofikiwa mjini
Muscat takriban wiki mbili zilizopita juu ya mpango wa kuyatengeneza majengo
hayo.
Alieleza
kuwa, matengenezo ya Beit El Ajaib yanahitaji utaalamu mkubwa, hivyo pande zote
mbili zimekubaliana kuwa wakandarasi watakaopewa kazi hiyo ni wale wanaokidhi
viwango vinavyohitajika, ambao huenda wakawa wengine kwa kila mmoja kupewa eneo
lake.
“Tunatarajia
matengenezo haya yatakapokamilika, jengo hili litakuwa na muonekano wa kisasa
na mvuto wa ziada, ambao tunaamini litavutia watalii wengi zaidi kuliko wale
waliokuwa wanakuja kabla,” alieleza Mkurugenzi huyo.
Ujumbe
huo pia ulitembelea jengo la Makumbusho ya Kasri, Ngome Kongwe na iliyokuwa
nyumba ya kulelea watoto yatima Forodhani ambayo yote yanakabiliwa na uchakavu
mkubwa.
Hata
hivyo, kwa sasa serikali inaifanyia matengenezo nyumba iliyokuwa ya kulelea
watoto yatima, ili itumike kuhifadhi vitu na kumbukumbu zote zitakazohamishwa
kutoka Beit El Ajaib kupisha matengenezo hayo.
Kwa
mara ya kwanza, baadhi ya kuta za Beit El Ajaib ziliporomoka mwezi Disemba
2012, na baadae Novemba 2015, na tangu hapo serikali imelifunga kwa matumizi
yoyote, hali inayochangia kukosa mapato kutokana na ziara za kitalii zilizokuwa
zimezoeleka kuonekana pahala hapo.
No comments:
Post a Comment